• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Tanzania Yawakumbuka Wachina waliofariki ujenzi wa Tazara na kubainisha kutumia FOCAC kujitangaza

  (GMT+08:00) 2018-04-17 09:04:07

  Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

  USHIRIKIANO baina ya Tanzania na China ulianza siku nyingi wakati wa waasisi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong wa China ambao umeendelea mpaka sasa kwa viongozi wan chi hici mbili Rais John Magufuli na Rais Xi Jinping wa China.

  Uhusiano huo unaoendelea katika masuala mbalimbali ya kiuchumi,kisiasa na kijamii ulinza miaka mingi kwa kuanzia na ujenzi wa reli ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) iliyogeuka kuwa kichocheo kikubwa cha ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Afrika.

  Wananchi wa China walikubali kutoa michango ya hali na mali ili kufanikisha ujenzi wa reli hiyo huku wakikabiliwa na ufukara wao na serikali yao na wameendelea kuwa marafiki wa kweli kwa Watanzania bila kuwageuka, hadi Taifa hilo lilipofanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na kuwa moja ya nchi tajiri duniani.

  Mbali na hiyo, Mwalimu Nyerere akishirikiana na Dk Salim Ahmed Salim walifanikisha kuifanya China kuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

  Wakati wa ujenzi wa Tazara,wananchi wa China 70 walifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wachina yaliyopo eneo la Gongo la mboto kambi ya jeshi la wananchi huku yakiratibiwa na taasisi ya Tanzania China Friendship Promotion Association chini ya Mwenyekiti wake Dk. Salim A.Salim kwa kushirikiana na ubalozi wa China nchini.

  Maazimisho ya kumbukumbu ya mashujaa wa China waliopoteza maisha wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara,yamefanyika hivi karibuni katika maeneo hayo ya makaburi.

  Raia hao wa China walifariki kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kuuliwa na wanyama wakali, wadudu na hali ya hewa,hivyo kubainisha kuwa urafiki uliopo wan chi hizi mbili umeunganishwa na damu ya wachina ambao walipoteza maisha wengine walipata vilema vya maisha wakati wa ujenzi wa reli hiyo.

  Katika kuonesha kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili Rais Xi Jinping alipoingia madarakani, mwaka 2013 nchi ya kwanza kutembelea katika bara la Afrika ni Tanzania na kubainisha kuwa moyo uliooneshwa na nchi yake wakati wa ujenzi wa Reli ya Tazara unapaswa kuendelezwa.

  Katika maadhimisho hayo, Tanzania ilitangaza rasmi kuwa miongoni mwa nchi zitakazoshiriki mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) utakaofanyika mwezi Septemba mwaka huu.

  Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga alitangaza hayo kuwa ni fursa pekee kwa kujitangaza kimataifa kwani mkutano huo unafungua milango katika nyanja za elimu,uchumi na kijamii na utanufaisha si tu Tanzania bali pia nchi za kiafrika kwa ujumla.

  "katika Ukanda mmoja, njia moja, Tanzania ina nafasi ya kuwa kiunganishi kwa nchi sita zinazotuzunguka, hivyo tunahitaji upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, reli, viwanja vya ndege na barabara kama kiunganishi, ni fursa nzuri kwenye kuitumia nafasi ya mkutano huu ambao utafungua milango kwa nchi za Afrika katika kupiga hatua za kimaendeleo."anasema Maiga.

  Pia Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji wa bidhaa yatakayofanyika mjini Shanghai yametajwa kuwa yatatoa fursa kwa nchi za Afrika kuonyesha bidhaa zao na kutafuta soko nchini China.

  Naye Balozi wa China nchini, Wang Ke anaweka bayana kuwa taifa la China linaikumbuka Reli ya Tazara kama moja ya miradi yao mikubwa Afrika na ya kujivunia.

  "Tazara inajulikana duniani kama reli ya uhuru na urafiki, nusu karne iliyopita, wachina wafanyakazi na mainjinia waliungana na dada na kaka zao wa Tanzania na Zambia, walifanya kazi ya ujenzi wa reli ya Tanzara katika mazingira magumu."

  Anasema kutokana na mazingira magumu ya kazi, wachina 70 walipoteza maisha, katika kuwaenzi kila mwaka wanakumbukwa kwa kuwapa heshima heshima ya kipekee,urafiki wa Tanzania, Zambia na China umeunganishwa na damu na utaishi kwenye maisha ya wachina daima dumu kizazi na hata kizazi.

  "China tunauchukulia mradi huu kama moja ya alama ya uhusiano wa kindugu baina yetu na bara la Afrika….. "Hii ni reli iliyokuwa inahitajika sana wakati huo baina ya nchi za Tanzania na Zambia ili kupambana na kero za makaburu waliokuwa wakitawala Afrika Kusini, hususani katika kusafirisha mizigo ya Zambia ambayo haipakani na bahari."anabainisha.

  Akimnukuu Rais Xi Jinping, Balozi Wang Ke anasema urafiki kati ya China, Tanzania na nchi za Afrika utaendelea kuwa imara na China haiwezi kuwasahau marafiki zake wa Afrika. China inatambua kuwa changamoto kwa nchi za Afrika kwa sasa ni kulinda amani na usalama.

  Alisema China itashirikiana na nchi za Afrika kukabiliana na matishio ya usalama kama ugaidi, uharamia na majanga ya asili, na itahimiza ushiriki wake kwenye utatuzi wa migogoro.

  Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku akitoa historia ya reli hiyo anasema Wachina, chini ya mwasisi wa taifa lao, Mwenyekiti Mao Zedong, walikubali kuijenga katika kipindi ambacho uchumi wao ulikuwa bado mdogo sana kulinganisha na sasa na kuijenga kwa ufanisi mkubwa.

  "Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliomba msaada kwa nchi moja ya Magharibi ilikataa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo, misimamo tofauti kati ya China na nchi za magharibi iliwafanya watu wa Afrika wafahamu China ndiyo rafiki ya kutegemea"anasema.

  Anaeleza wazi kuwa baada ya kukwama huko kwenye nchi za Magharibi wakaenda China, alielezea matatizo ya ukombozi kwa nchi za Afrika lakini akashindwa kuomba fedha za ujenzi kwa vile zilikuwa ni nyingi.

  " lakini wakati wa kuondoka Mao akimsindikiza alipofika mlangoni alimuliza kweli unahitaji reli, Mwalimu Nyerere akasema ndio nahitaji nikipata wa kunijengea nitashukuru, Mao akamwambia, umepata, nitakujengea, hiyo ilikuwa ni mwaka 1968 na mwaka 1969 ujenzi ukaanza"anaeleza

  Alisema mbali na ujenzi wa reli pia wamesaidia katika masuala ya usalama, kwani Tanzania haikuwa na silaha wakatupatia na vingine ambavyo si vema kuweka hadharani.

  Waziri wa Sheria na Katiba, Paramagamba Kabudi naye anasisitiza mahusiano mazuri ya nyakati hizo kwani walijenga viwanda kama cha Keko Phamacetically, Ufi, na Urafiki, achilia mbali miradi mbali mbali ambayo wametusaidia na wanaendelea kutusaidia, yote hiyo ni alama nzuri ya urafiki uliojengwa na waasisi wetu, ambao unadumu kizazi na kizazi.

  mkutano wa Ushirikiano kwa nchi za Afrika na China (FOCAC)uliofanyika mwaka 2015, Johannesburg, nchini Afrika Kusini na kuongezewa dola milioni 60 ambayo ni mkopo na Ujenzi wa Miundombinu ikiwa ni lengo la kwanza,kwa ajili ya kuunganisha nchi zote 54 za Afrika kwa kupitia miradi mbalimbali ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa barabara za kisasa, Viwanja vya Ndege ,Reli kwa ajili ya Treni za Mwendo kasi na Bandari.

  Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China ,Geng Shuang amebainisha kuwa mkutano wa kilele wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC mwaka huu utafanyika hapa Beijing, China.

  amesema, katika mkutano huo, viongozi wa China na nchi za Afrika watajadili mpango wa ushirikiano wa kirafiki kati ya pande hizo mbili, na kutunga mustakabali wa ushirikiano kati ya China na Afrika kwenye enzi mpya, ili kutimiza ushirikiano wa kunufaisha pande zote mbili na maendeleo ya pamoja kwenye kiwango cha juu zaidi.

  pia utatangaza hatua kubwa zinazolenga kuongoza maendeleo na ushirikiano kati ya China na Afrika na kuhimiza ushirikiano na mawasiliano kati ya pande mbili katika nyanja mbalimbali..

  Mwisho

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako