• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Dunia na Ukimya juu ya mgogoro wa kibiashara

  (GMT+08:00) 2018-04-18 15:22:47

  Majaliwa Christopher

  Mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani umefika pabaya. Si pazuri kwa China. Si pazuri kwa Marekani. Si pazuri kwa dunia.

  Dunia imekaa kimya. Jumuiya za kimataifa zimekaa kimya. Bila shaka suala limeachwa kwa mataifa haya mawili wamalizane wenyewe kwa wenyewe.

  Kwa muelekeo na majibizano kati ya pande zote mbili ni dhahiri kuwa ufumbuzi wa karibu juu ya hili suala halipo. Dunia sasa inashuhudia kutunishiana misuli, kulipiza visasi na kufikiria vikwazo vikali zaidi.

  Swali kubwa ambalo pia si rahisi kupata jibu ni kwanini dunia iko kimya?

  Hofu inazidi kutanda, Marekani inasema itaendelea zaidi, China inajibu, iko tayari kwa namna yoyote na kwa njia yoyote, dunia bado iko kimya! Mataifa makubwa yapo kimya, hayakemei, hayaingilii kati wala hayashauri.

  Ni hofu? Ni fursa? Au ndo ile dhana ya kufa kufaana? Majibu yapo lakini labda hakuna taifa hata moja lenye uthubutu wa kusema chochote, kukemea au kushauri, kwa sababu labda madhara ya chochote kitakachosemwa kinaweza kuwa na muitikio tofauti.

  Hakuna asiyejua nguvu za mataifa haya mawili kiuchumi na hata kiushawishi kwani ndizo zinashikilia nafasi mbili za juu kiuchumi.

  Hapa ndipo hasa hofu na wasiwasi unapoegemea, kutokana na nguvu kubwa ya kiuchumi na mchango wao katika uchumi wa dunia, bila shaka jambo lolote linalowahusu linahusu dunia.

  Lakini je, dunia yote ni 'Marekani na China'? Kwanini dunia iko kimya? Vyombo vya habari duniani kote vyenye ushwishi na visivyo na ushawishi vimeandika, vimeonya na kushauri umuhimu wa kujenga ukuta kabla ya kuziba ufa yaani kutatua hii changamoto kabla haijawa tatizo kubwa.

  Wachambuzi na wataalamu wamepaza sauti, hakuna kilichosaidia. China na Marekani wameachwa waamue itakavyowapendeza?

  Cha ajabu Shirika la Biashara la Dunia (WTO) limeishia kuonya, baada ya kuonya imekaa kimya. Limetulia. Halisemi tena. Je kazi ya WTO ni kuonya tu na kukaa kimya huku ikichungulia dirishani mambo yanavyoteleza?

  Shirika la Biashara la Kimataifa ni chombo cha kimataifa chenye madaraka na mamlaka ya juu kabisa kuangalia na kusimamia taratibu na kanuni namna ya kufanya bisahara baina ya mataifa mbalimbali.

  Mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani unaota mizizi, shirika limeishia kuonya bila kuchukua hatua.

  Kuonya huko na kuishia kuwa mtazamaji ndiyo sasa dunia iamini kuwa WTO haina nguvu na mamlaka ya kusimamia kanuni zinazoongoza biashara?

  Au dunia, mamlaka, jumuiya za kimataifa pamoja na mashirika kama WTO yanasubiri hadi mambo yawe magumu zaidi ndiyo yaingilie kati na kuchukua hatua?

  Au tunaaminishwa kuwa dunia imegawanyika tayari kibiashara, hali inayosababisha kutokuwepo na msimamo wa jumla juu ya China na Marekani.

  Ingawa hatua zimechelewa kuchukuliwa lakini bado nafasi ipo kwa Shirika la Biashara Duniani kutekeleza majukumu yake ya msingi ili kuweka mambo sawa kabla hayajawa magumu zaidi.

  Pamoja na majukumu mengine, shirika hili llianzishwa kwa sababu mahususi ya kusimamia kanuni na taratibu za biashara za kimataifa, kusimamia majadiliano huru ya kibiashara na kutatua migogoro mbalimbali ya kibiashara.

  Ni muda muafaka sasa, ni vema na ni haki pia, WTO ikafanya kazi yake ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kuibuka kutokana na huu mgogoro.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako