• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Uwazi wa China utachochea ufanisi wa kichumi katika mataifa mengi

  (GMT+08:00) 2018-04-26 09:46:18

  Na Eric Biegon - NAIROBI

  Wakati ulimwengu ulikuwa unakaribisha mwaka wa 2018, Rais wa China Xi Jinping alitoa hotuba muhimu kuhusiana na nchi hiyo kufungua milango yake na kuwa wazi kwa dunia kati ya maswala mengine. Hii ilikuwa ni muhimu sana kwani haikuwa tu inahusu taifa la China bali ililenga binadamu kwa ujumla.

  "Kama nchi inayowajibika pakubwa, China lazima izungumze. China itakuwa mstari wa mbele kulinda hali na mamlaka ya Umoja wa Mataifa na kutimiza wajibu wake kikamilifu katika masuala ya kimataifa." Alisema Rais Xi

  Alihitimisha hotuba yake kwa kutangaza kwamba "Wote chini ya mbingu ni familia moja."

  Sasa ni miaka 40 tangu China kuzindua mpango wa mageuzi ya kiuchumi ambayo ilianzishwa mwaka 1978 na wakereketwa ndani ya Chama cha Kikomunisti cha China wakiongozwa na Deng Xiaoping. Bila shaka hii imekuwa njia ya uhakika ya kuafikia maendeleo katika China ya sasa.

  Si siri kwamba mkakati huu wa maendeleo ya nchi umeleta mabadiliko makubwa kwenye taifa la China. Kwa kweli, China imenawiri na kuwa uchumi wa pili kwa ukubwa duniani, taifa lenye uwezo mkubwa zaidi viwandani, nchi yenye biashara kubwa ya bidhaa, na mmiliki mkubwa wa fedha za kigeni.

  Katika kipindi hiki wa kupanua milango yake, China imepata pato la taifa la wastani wa ukuaji wa asilimia 9.5 huku rekodi zikionyesha kuwa biashara yake ya nje imekuwa na ukuaji wa kila mwaka wa asilimia 14.5.

  Matokeo ya mpango huu kwa raia wa China inakadiria kwamba zaidi ya wananchi bilioni 1.3 wa nchi hiyo sasa wanafurahia maisha ya mafanikio kiasi.

  Wakati wa Kongamano kuu la 19 la chama cha kikomunisti ya China, kiongozi wa China Xi Jinping aliweka wazi kwamba zaidi ya watu milioni 700 nchini humo wameondolewa kutoka kwenye umaskini.

  Taifa hilo la Kikomunisti linakadiria ya kwamba kufikia mwaka 2020, umaskini utatokomezwa kutoka ndani ya mipaka yake.

  Lakini uwazi na mageuzi yaliyofanywa China haikubadili hali ya taifa hilo pekee kwani kwa kiasi kikubwa imeguza dunia nzima. Ulimwengu kwa sasa umekuwa kijiji ya mataifa ambapo maslahi yanahusiana. Ili kukuza ustawi, mataifa hayana budi ila kujiunga na jumuia ya mataifa.

  Aidha, kuna haja ya mwingiliano bora kwa kushirikiana kwa ajili ya kupata mafanikio ya pamoja. Bila shaka, China imekuwa mstari wa mbele katika suala hili.

  Taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Asia imekuwa ikiongoza kampeni ya kufanya utandawazi wa kiuchumi kuwa wazi, yenye uwiano na manufaa kwa wote.

  Tangu alipochukua hatamu za uongozi, Rais Xi amekuwa akihimiza kujengwa kwa jamii yenye ufanisi wa pamoja. Hii imekuwa nguzo mahususi ya uongozi wake. Pendekezo hili limepokelewa vyema na kupokea uungwaji mkono kutoka mataifa mengi duniani, na sasa imeratibiwa katika nyaraka muhimu ya Umoja wa Mataifa.

  Kwa mujibu wa utawala wa China ulioko Beijing, China kufungua milango yake ni uamuzi wa kimkakati na hatua madhubuti ya kuboresha utandawazi wa kiuchumi kwa namna ambayo watu wengi watafaidika duniani kote.

  Chini ya mfumo mpya wa Rais Xi, China imeingia awamu mpya ya ufunguzi. Ameahidi kwamba China itapanua masoko yake, kujenga mazingira ya kuvutia ya uwekezaji na kupanua soko ya bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa ya nje.

  Mipango muhimu yatazinduliwa mwaka huu. China imeelezea nia ya kuongeza bidhaa zinazoagizwa na pia kuafikia usawa wa biashara ya kimataifa. Taifa hilo pia limetangaza kwamba litapunguza ushuru wa forodha na ulete bidhaa zaidi ambazo ni za ushindani na zinazohitajika kwa watu wa China.

  Hili kufanikisha haya, matukio mawili muhimu yatafanyika katika China mwaka huu.

  Mnamo Septemba, China itakuwa mwenyeji wa Jukwaa la mkutano wa ushirikiano kati ya China na Afrika, FOCAC mjini Beijing. Mkutano huu utawaleta pamoja marais na viongozi wa serikali kutoka Afrika na maafisa wa serikali ya China ambao watakuwa wakijadili mapendekezo juu ya mafanikio yaliyopatikana tangu uzinduzi wa mipango kumi ya ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka 2015. Viongozi hao pia wanatarajiwa kuweka mkakati mpya wa maendeleo na ushirikiano mpana ili kuafikia mafanikio ya pamoja.

  Muda mfupi baada ya mkutano huu muhimu, China itafanya maonyesho ya kwanza kabisa ya kimataifa mjini Shanghai, mwezi Novemba. Haya hayatakuwa maonyesho ya kawaida kwani China itakuwa ikizindua sera ya mpango na dhamira ya kufungua soko lake kwa mataifa ya nje. Mataifa marafiki wa China kote duniani wamealikwa kushiriki maonyesho hayo bila ya vikwazo vyovyote.

  Mataifa kutoka Afrika kama vile Kenya, Tanzania na Uganda yamealikwa na hivyo bidhaa kutoka Afrika Mashariki kama vile kahawa, chai, maua na maeneo ya kuvutia ya utalii yatapata nafasi ya kutangazwa katika soko la China.

  Afrika kwa upande wake, inaonekana kukumbatia mpango huu ya uwazi. Mwezi Machi, nchi 43 za Afrika zilitia saini makubaliano ya kihistoria ya kuanzisha Biashara Huria la Afrika. Hatua hii muhimu sana itawezesha usafirishaji huru wa bidhaa, huduma na watu katika Afrika.

  China ni mfano mzuri wa jinsi kufungua milango inaweza kuwa kichocheo cha mabadiliko na maendeleo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako