• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Vijiji 800 nchini Kenya kufaidika kutokana na mradi wa digitali inayofadhiliwa na China

    (GMT+08:00) 2018-04-26 20:33:02

    Na Eric Biegon

    USHIRIKIANO kati ya Kenya na China kwa mara nyingine utahakikisha kuwa jumla ya vijiji 800 kote nchini vitapata kuunganishwa kupitia mradi wa utoaji wa runinga ya kunasa mawimbi ya digitali bila malipo.

    Hii ni sehemu ya mpango wa serikali ya kutaka kuziba pengo lililopo kati ya maeneo ya vijijini na mijini na kutimiza hitaji la kikatiba la kuakikisha haki ya kupata habari kwa raia.

    Akizungumza wakati wa uzinduzi wa semina ya kitaifa ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya uandisi, Katibu Mkuu katika wizara ya mawasiliano wa Kenya Sammy Itemere alifichua kuwa mkenya mmoja kati ya sita hana uwezo wa kufikia mawasiliano ya digitali hasa katika maeneo ya vijijini.

    "Kufuatia uhamiaji kutoka mfumo wa analogi hadi kwenye mawimbi ya digitali katika mwaka 2015, idadi kubwa ya Wakenya bado hawajanufaika na mawasiliano hayo. Takwimu kutoka Mamlaka ya mawasiliano ya Kenya (CA) mwaka 2017 zinaonyesha kuwa mawimbi ya mawasiliano ya digitali imewafikia asilimia 83.6 ya wakenya."Alieleza Itemere.

    Afisa huyo wa serikali alisema kuwa mradi wa vijiji 800 kutoka China itatoa runinga mbili zinazotumia nishati ya jua, na seti moja ya sahani ya setilait (dish) na vifaa vingine katika vituo vitatu vya umma kama vile mashule, vituo vya vijana au maeneo mengine ya umma katika vijiji vinavyolengwa.

    "Tunataka kushukuru serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuratibu Kenya kama nchi mojawapo ya mataifa yatakayofaidika na mradi wa usambazaji wa televisheni za kunasa mawimbi ya digitali unaolenga vijiji 10,000 Afrika." alisema Itemere.

    Alisema kuwa teknologia imechukua nafasi bora nchini Kenya kwani haitoi tu msukumo katika sekta muhimu ya uchumi bali pia imejikita katika mpango wa kuendeleza taifa almaarufu Ruwaza 2030 (Vision 2030).

    "Mafanikio ya mradi huu itasababisha kuongezeka kwa uhamisho wa maarifa na uzalishaji wa mali, mshikamano wa kitaifa na kuwezesha kufanikishwa kwa ajenda kubwa nne za serikali kupitia utoaji wa huduma za mawasiliano na masoko." Alisema Itemere.

    Aliongeza kuwa serikali ina nia ya kufanikisha mradi huo huku akidokeza kuwa wizara ya mawasiliano imebuni kamati ya kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo. Aidha, alisema wizara hiyo inahakikisha kuwa masuala yote muhimu ikiwa ni pamoja na msamaha wa kodi, uteuzi wa vijiji, na kutiwa saini kwa mkataba na kampuni ya StarTimes Group ya China imeshughulikiwa ipasavyo.

    Kansela wa kibiashara kwenye Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Kenya Dkt. Guo Ce alisema kuwa lengo la mradi huo ni kupunguza pengo lililopo la mawasiliano kwa kuhakikisha kuwa jamii iliyoko vijijini imepata fursa sawa ya kupokea mawimbi ya digitali.

    Dkt. Guo alisema kwamba Kenya imepiga hatua kubwa barani Afrika kwani tayari imemaliza uteuzi wa vijiji 800 vitakavyofaidika na mradi huo.

    Afisa huyo kutoka China alieleza kwamba mradi huo ni sehemu ya maazimio ya ya mkutano wa ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), iliyofanuika jijini Johannesburg, Afrika Kusini 2015, ambapo rais wa China Xi Jinping aliahidi kutoa masaada wa runinga za setilaiti katika vijiji 10,000 barani Afrika.

    "Kenya ipo kwenye eneo bora kimkakati na hii imevutia makampuni mengi kutoka China yanayotafuta kuwekeza Afrika na imekadiriwa kuwa miongoni mwa mataifa matatu makubwa yanayopokea wawekezaji wakuu kutoka China." Alisema Guo.

    Alifichua kuwa makampuni ya Kichina yameshiriki katika ujenzi wa miradi zaidi ya 100 nchini Kenya ikiwa ni pamoja na mradi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Nairobi (SGR).

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako