• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China yaonya usafirishaji pembe za ndovu

  (GMT+08:00) 2018-05-02 08:50:15

  Na Majaliwa Christopher

  Huku ujangili ukiripotiwa kupungua katika nchi za Afrika, China imetoa onyo kali kwa raia wake watakaobainika kujihusisha na usafirishaji wa pembe za ndovu kutoka barani humo.

  Serikali ya China imetangaza na kusisitiza kuwa, kwa namna yoyote ile, haitamvumilia raia wake atakaebainika kujihusisha na biashara hiyo haramu.

  China imeweka wazi kuwa iko tayari na inaendelea kuunga mkono juhudi za nchi za Afrika katika kupambana na mauaji ya tembo na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu.

  Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Dai Bing, akizungumza na waandishi wa habari kutoka barani Afrika walioko nchini China kwa mafunzo maalum, amesema bishara ya pembe za ndovu ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

  Bw. Dai ametoa msimamo wa China miezi michache baada ya serikali kuharamisha biashara ya pembe za ndovu. Kabla ya hapo, China ilikuwa moja ya masoko makubwa duniani ya pembe za ndovu.

  Biashara iyo ilisitishwa rasmi mwishoni mwa mwaka jana, hali ambayo ilisifiwa kama hatua muhimu katika kulinda tembo barani Afrika ambao hapo mwanzoni walikuwa wakiuawa na majangili na pembe zao kusafirishwa nje.

  Tanzania ni moja kati ya nchi za Afrika ambazo zina idadi kubwa ya tembo, lakini tembo hao wamekuwa wakipungua kutokana na kushamiri kwa shughuli za ujangili uliokuwa ukichochewa na mahitaji makubwa ya pembe zao hususan katika nchi za bara la Asia.

  Bw. Dai alisema kuwa China imedhamiria kwa dhati kusaidia kulinda wanyamapori katika bara la Afrika, huku ikichukua hatua muhimu kuhakikisha vita dhidi ya ujangili unakuwa na mafanikio makubwa.

  "Najua mna taarifa kwamba kuna baadhi ya Wachina wanashiriki katika biashara hii haramu. Napenda kuwataarifu kwamba serikali yetu haitamvumila raia wake yeyote anaejishugulisha na shuguli hizi, tunachukua hatua muhimu na madhubuti kwenye hili," alisema.

  Bw. Dai alisisitiza kwamba usafirishaji haramu wa pembe za ndovu siyo tu kwamba ni ukiukwaji wa sheria za Afrika na sheria za dunia bali pia ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za China.

  Katika hatua nyingine, Bw. Dai alisema kwamba China inachukua tahadhari kubwa kuhakikisha shughuli zake barani Afrika haziichangii katika uchafuzi wa mazingira.

  "Tunachukua tahadhari na hatua stahiki kuhakikisha hatuleti uchafuzi wa mazingira barani Afrika. hatuna nia wala mpango wa kuchafua anga za bluu za Afrika, milima mizuri wala maji safi yaliyopo barani humo," alisisitiza.

  Mkurugenzi huyo aliendelea kueleza kuwa miaka 20 iliyopita, serikali ya China iliweka wazi kuwa haitaki kufata mfumo wa mataifa mengine yaliyoendelea ambayo huchafua mazingira kwanza na baadae kuanza kushugulikia namna ya kutatua.

  Ameongeza kuwa kama nchi, wameweka sheria na sera mbalimbali kuhakikisha kuwa wanatekeleza dhamira hiyo kwa dhati.

  Bw. Dai alitolea mfano jiji la Beijing, kwa kusema kuwa miaka saba iliyopita jiji hilo ambalo ni mji mkuu wa China ulighubikwa na uchafuzi wa hewa kwa kiasi kikubwa.

  Kutokana na hali hiyo, Bw. Dai alisema limekuwa funzo kubwa sana kwao na sasa wanachukua hatua stahiki kabla, kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo popote pale wanapoendesha shughuli zao za uzalishaji.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako