• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Serikali China haitengenezi, haisafirishi bidhaa feki

    (GMT+08:00) 2018-05-02 09:00:01

    NA Majaliwa Christopher

    China imezitaka nchi za Afrika kuhimarisha ulinzi na ukaguzi mipakani na maeneo yote muhimu ikiwemo bandari na viwanja vya ndege ili kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.

    Ushauri huo umetolewa wakati nchi za bara la Afrika zikiwa katika mapambano ya kuhakikisha kuwa zinaondokana na bidhaa feki zilizotapakaa katika masoko yake.

    China ni moja kati ya nchi za bara la Asia ambazo zimekuwa zikitajwa kuwa hutengeza bidhaa hizo zilizo chini ya viwango na kuzisambaza barani Afrika.

    Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Bw. Dai Bing amekanusha kuwa serikali ya China kwa namna yoyote haihusiki na utengenezaji wala usafirishaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.

    Akizungumza na waandishi wa habari kutoka barani Afrika, Bw. Dai amesema China ni moja kati ya mataifa makubwa yenye sayansi na teknolojia ya hali ya juu na "haiwezekani nchi hiyo ikahimiza na kuipa nafasi utengenezaji na usafirishaji wa bidhaa za namna hiyo."

    Hata hivyo amezitupia lawama nchi za bara la Afrika kutokana na kushindwa kudhibiti wafanyabiashara wake wanaojihusisha na uingizwaji wa bidhaa zisizokidhi viwango.

    Bw. Dai amesema kuwa bidhaa hizo zinazolalamikiwa na nchi za Afrika ambazo pia kwa kiasi kikubwa huchangia sana kuharibu 'brand' ya China, zinaingizwa na wafanyabiashara wa Afrika wenyewe na wala siyo Wachina.

    Hata hivyo amekiri kuwepo kwa baadhi ya wananchi wa China wasiokuwa waaminifu wanaoshirikiana na hao wafanyabishara kufanikisha iyo njama, akisisitiza kuwa wanaendelea kuchukua hatua stahiki kulinda viwango vya bidhaa zake na kulinda jina lake katika anga za kimataifa.

    "Serikali ya china haiwezi kutengeneza bidhaa feki wala zilizo chini ya viwango. Hatuungi mkono pia shughuli kama hizi wala hatutafumbia macho wafanyabiashara wetu wachache wasio waadilifu wanaoshirikiana na wafanyabiashara kutoka Afrika kusafirisha bidhaa za aina hiyo," alisema.

    Bw. Dai aliongeza kuwa nchi yake inasikitishwa sana na taarifa zinazoendelea kuenea kuwa inatengeneza bidhaa za aina iyo, huku ikataka nchi za Afrika kushirikiana na China kulipatia ufumbuzi wa kudumu janga hilo.

    Shirikisho la Viwanda nchi Tanzania (CTI) katika utafiti wake mwaka jana juu ya hali ya bidhaa zisizokidhi viwango, ilionyesha kuwa Tanzania na Kenya zinaongoza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na bidhaa zilizo chini ya viwango.

    Katika nchi hizo mbili, asilimia kubwa ya bidhaa hizo (takribani asilimia 80) huingia kwa njia ya bandari.

    Bw. Dai alisisitiza kuwa dhana kwamba China inatengeneza bidha feki imekuwa ikiichafua hadhi yake, akiongeza kuwa kama nchi hawatahusika kamwe na shughuli za namna hiyo popote pale duniani.

    Aliongeza kuwa ushirikiano wa kibiashara kati ya China na Afrika umejengwa katika misingi ya urafiki, undugu na kuaminiana na endapo kuna changamoto zozote pande hizo mbili si budi zi kae mezani na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hizo.

    Aidha, Bw. Dai aliongeza kuwa China ikiwa ni nchi kubwa sana kuna muda inapata changamoto katika kudhibiti kila kinachotoka nje ya nchi.

    Amesema sheria na hatua kali pamoja na ushirikiano baina ya pande mbili—Afrika na China, zitasaidia kupata matokeo chanya katika vita dhidi ya bidhaa zilizo chini ya viwango.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako