• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Hadithi yangu Afrika: Maisha mapya mbali na nyumbani

  (GMT+08:00) 2018-05-25 08:56:27

  Binadamu yeyote hupenda maisha mazuri, furaha, kuishi karibu na familia, ndugu, jamaa na marafiki --na zaidi ya yote kuishi na kufanya kazi nyumbani.

  Pale mtu anapokuwa mbali na kwao, kwa sababu yoyote ile, iwe ukimbizini, masomoni au katika majukumu yoyote ile ya kimataifa hujisikia mnyonge, kukosa furaha na amani.

  Inahitaji moyo wa ziada, kujitolea, upendo na undugu kukubaliana na hali halisi ya kuishi mbali na nyumbani hasa pale mtu anapoweka rehani kila kitu ikiwemo uhai wake ili kufanikisha lile jambo lenye faida kwa jamii nyingine kuliko kwake mwenyewe.

  China na watu wake ni moja kati ya mataifa na watu wa kutolea mfano linapokuja suala la kujitoa mhanga ili kuhakikisha dunia ,hususan Afrika, inazidi kuwa pahala salama pa kuishi kwa watu wote.

  Bara la Afrika na taifa la China kimsingi zina historia ndefu katika mawanda mazima ya mahusiano unaozidi kuimarika siku baada ya siku.

  Wapo Wachina, mbali na taifa lao kuwa katika mstari wa mbele katika kuhakikisha ushirikikiano wake na Afrika unadumishwa na kuimarishwa, wamejitoa nafsi zao, kwa hali na mali kutumika katika ujenzi wa jamii iliyo imara na endelevu barani Afrika.

  Mwezi Mei 24, 2018, Sekretarieti ya Kamati ya utekelezaji wa miradi ya Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika na Radio China Kimataifa ( CRI) zilitoa tuzo kwa raia wa China waliojitoleaa kuishi barani Afrika wakiwa katika majukumu mbalimbali.

  Utoaji wa tuzo ulitanguliwa na mashindano kupitia njia ya mtandao uliojulikana kwa jina la 'Hadithi yangu Afrika', ambayo yalihusisha makala, picha, na video kutoka nchi zaidi ya 40 barani humo.

  Kihistoria, kujitoa kwa raia wa China kuhakikisha bara la Afrika linakuwa sehemu salama na huru kuishi hakujaanza leo wala jana.

  China kama taifa na raia wake walijitolea kwa hali na mali kuhakikisha bara la Afrika linakuwa huru kutoka katika mikono ya wakoloni na makaburu.

  Kama hili halitoshi, zipo roho zilizopotea wakati China ilipojitolea katika kujenga reli yenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,800 kutoka jijini Dar es Salaam, Tanzania hadi Lusaka, Zambia (TAZARA).

  Mashindano haya yaliyoendeshwa kwa siku 11, kimsingi yalilenga kudumisha urafiki, undugu na uhusiano mwema uliopo kati ya China na Afrika.

  Lakini pia yalilenga kuelezea namna maisha barani Afrika yalivyo na vile hawa 'mashujaa' walivyoweza kuhimili kwa kugeuza changamoto za kimaisha barani humo kuwa fursa na kupafanya kuwa 'nyumbani'.

  Naibu Mhariri Mkuu wa CRI Bw. Ren Qiang anaamini kuwa mbali na shindano la 'Hadithi yangu Afrika' kuwafanya raia wengi wa China kufahamu Afrika, lakini pia inakuwa ni kichocheo muhimu cha ushirikiano baina ya pande zote mbili.

  Moja kati ya washindi wa tuzo la mashindano ya 'Hadithi yangu Afrika', ni mwanajeshi alieshiriki katika kulinda amani nchini Sudan Kusini.

  Huyu aliacha familia yake China na kwenda Sudan Kusini, zaidi ya kilomita 9,000, kuhakikisha amani inatamalaki katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

  Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kwamba hadi sasa raia wa China watatu wamekwishapoteza maisha katika harakati za kulinda amani barani Afrika.

  Baadhi ya walionyakua tuzo za katika mashindano haya, wanasema walipokuwa wanaenda barani Afrika waliamini uwepo wao huko kungeleta mabadiliko makubwa miongoni mwa wakazi wa barani humo lakini badala yake wao ndio wamebadilika na kujisikia furaha na faraja kufanya kazi na wakazi hao.

  Uhusiano kati ya Afrika na China ulianza miaka 1960 na bado kuna kila jitihada kwa pande zote mbili kuhakikisha ushirikiano huu unazidi kuwa na faida maradufu.

  Maeneo ambayo Afrika na China hushirikiana ni pamoja na biashara, uwekezaji, afya, elimu, utamaduni, ulinzi na amani, ujenzi na rasilimali watu.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako