• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Nafasi ya FOCAC utekelezaji wa Agenda 2063

    (GMT+08:00) 2018-05-28 10:51:54

    Na Majaliwa Oswero

    Afrika haina budi kutumia vizuri fursa zilizopo kwenye Jukwaa la Ushirikiano wa bara hilo na China (FOCAC) ili iweje kufanikisha agenda yake ya 2063 uliopitishwa na Umoja wa Afrika (AU).

    Agenda 2063 ilipitishwa mwaka 2015 na Umoja wa Afrika huko Addis, Ababa nchini Ethiopia kutaka Afrika yenye Amani, Maendeleo na utangamano na kuwa na Afrika wanayoitaka.

    Katika kutekeleza Agenda hiyo Umoja wa Afrika uliandaa mpango wa kwanza wa miaka kumi ya utekelezaji wa miradi ya kwanza muhimu iliyojikita kwenye sekta za nishati, usafirishaji, usafiri wa anga, sayansi na teknolojia pamoja na kukuza utangamano barani humo.

    Akizungumza katika Jukwaa la mabalozi wa Afrika nchini China, balozi wa Cape Verde nchini China Bi. Tania Romualdo alisema malengo mengi yaliyopo katika agenda hiyo pia yapo katika maeneo ambayo China na Afrika wamekubaliana kushirikiana chini ya mwamvuli wa FOCAC.

    Balozi Tania alisema wakati Afrika ikiendelea kushirikiana na nchi zingine katika kutekeleza malengo yake makubwa hususan Dira ya Maendeleo ya Afrika hususani Agenda 2063, lazima pia waweke kipaumbele cha pekee katika utekelezaji wa maazimio na malengo ya FOCAC.

    "FOCAC itatupatia nafasi nzuri ya kuhakikisha malengo yetu tuliyojiwekea kama bara kufikia 2063 yanafanikiwa kwa kiasi kikubwa," alisema balozi Tania.

    Alisema mradi wa mabilioni ya dola za Kimarekani uliohasisiwa na Rais wa China, Xi Jinping --Ukanda Mmoja, Njia Moja, pia ni fursa nyingine ambayo Afrika ikitumia vizuri itayafikia malengo yake kirahisi.

    "Ukiangalia vizuri haya mambo yote ya Ukanda Mmoja, Njia Moja, Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika zinaendana kwa kiasi kikubwa na agenda 2063 ambayo bara letu limejiwekea kufikia Afrika tunayoitaka," alisisitiza.

    Nchi za bara la Afrika pia kwa sasa, kama ilivyo kwa nchi zingine katika mabara mengine, zinatekeleza malengo ya maendeleo endelevu.

    Utekelezaji wa malengo haya umekuja baada ya kumalizika kwa Mpango wa Maendeleo ya Millenia uliodumu kwa miaka 15 uliokuwa na malengo 10 yakiwemo ya kumaliza umasikini, njaa na athari za tabia nchi.

    Malengo ya Maendeleo Endelevu yako 17 ambayo ni Kukabiliana na Umasikini, Njaa, Afya, Elimu Bora, Usawa wa Jinsia, Maji safi na salama, Nishati salama, Ajira na Uchumi endelevu, Viwanda na miundombinu, Jamii salama, Uzalishaji, Tabianchi, Maisha maji, Maisha ardhi , Amani na Ushirikiano wa malengo.

    Katika hotuba yake Bi. Tania alisema Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika zinawiana pia moja kwa moja na Malengo ya Maendeleo Endelevu, hivyo nchi za Afrika lazima zifanye kazi kwa bidii na kutumia kila fursa linalopatikana kuhakikisha zinafanikiwa na kuwa na maendeleo endelevu.

    Aliongeza kuwa pamoja na kuwa kila nchi ndani ya bara hilo ina changamoto ambazo siyo lazima zifanane na nchi nyingine, umoja, ushirikiano na mshikamano ni nguzo muhimu katika utatuzi wa changamoto hizo.

    Aidha Bi. Tania alisisitiza umuhimu wa vijana na nafasi yao katika kuleta mabadiliko kwa bara la Afrika, akishauri viongozi kuweka mazingira wezeshi kwa vjana ili waweze kuwa na mchango chanya katika maendeleo endelevu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako