• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Ahadi ya China ya kutekeleza miradi Afrika kupitia mpango wa Ukanda Mmoja na Njia Moja

    (GMT+08:00) 2018-05-28 10:54:26

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Mpango wa mkanda mmoja njia moja unaadhimisha mwaka mmoja mwezi huu wa Mei tangu kuzinduliwa kwake rasmi kwa ulimwengu katika sherehe iliyofana jijini Beijing mwaka 2017. Halfa hiyo ilihudhuriwa na marais na viongozi wa serikali mbalimbali ambao baadaye waliidhinisha mpango huo na hatimaye kutia saini kuthibitisha uanachama wao katika mpango huo mkuu wa China ya kuunganisha dunia.

    Mpango huu, uliopendekezwa na Rais wa China mwaka 2013, imekuwa ya manufaa makubwa, hasa katika nchi zinazoendelea, na kwa hiyo imekuwa mradi wa maono makuu na cha kiwango cha juu mno.

    Ingali mapema, lakini matunda itokanayo na "Mradi huu wa karne" yameanza kuonekana katika maeneo ambayo nyayo zake zimekanyaga katika Afrika. Kenya na Ethiopia yana ushahidi wa kutosha katika suala hili. Mataifa kama vile Djibouti, Misri, Namibia, Tanzania na Msumbiji, kutaja tu baadhi, yanaonekana kufuata nyayo zao.

    Baadhi ya taasisi mashuhuri duniani kama vile Baker McKenzie na Knight Frank yametaja mpango huo kama kichocheo cha maendeleo huku yakiratibu fursa zinazopatikana kutokana na mpango wa mkanda mmoja njia moja.

    Eneo la Afrika Mashariki lilichukua nafasi ya kwanza kujiorodhesha katika mpango huo, kisha likafanyika kiungo muhimu ndani ya mpango huo wa OBOR. Mataifa katika ukanda huu yamefaidika kutokana na ujenzi wa miundombinu kama vile reli za kisasa, barabara, bandari, viwanja vya ndege au maeneo ya viwanda yanayofadhiliwa na China.

    Kwa nasibu, mwezi huu pia ni wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja tangu uzinduzi wa reli ya kisasa maarufu kama SGR nchini Kenya ambayo ilianza shughuli zake Mei 31 2017. Reli hiyo ya Mombasa-Nairobi ni kipengele mahususi ya ushirikiano uliopo kati ya Beijing na Nairobi.

    Mradi wa SGR uliofadhiliwa na kujengwa na China, unakadiriwa kuwa hadi sasa umezalisha nafasi za ajira zaidi ya 46,000 kwa raia wa Kenya, na kupunguza gharama pamoja na muda wa usafiri kati ya Mombasa na Nairobi karibu kwa nusu, huku ukiongeza Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia moja.

    Tangu uzinduzi wake mwaka uliopita, treni ya abiria, maarufu kama Madaraka Express, imesafirisha zaidi ya abiria milioni moja, huku treni ya mizigo ikibeba zaidi ya tani 300,000 ya bidhaa kwa muda huo. Shirika la reli nchini Kenya limelazimika kuagiza treni zaidi ili kutimiza mahitaji zaidi ya raia wanaotaka huduma zake.

    Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hivi karibuni alizindua mpango wa kiuchumi unaoitwa "Big Four Agenda." Mpango huu unalenga kutoa chakula cha kutosha, nyumba za bei nafuu, huduma za afya ya kuridhisha na mafanikio viwandani. Makampuni ya kichina yameahidi kuhakikisha utekelezaji wake kikamilifu.

    Takwimu zilizoko kwenye ubalozi wa China jijini Nairobi zinaonyesha kwamba makampuni ya Kichina yamewekeza milioni 100 dola za Marekani kuanzisha eneo la viwanda ya utafiti, maendeleo na uzalishaji, millioni 80 dola za Marekani kujenga kampuni kubwa zaidi Afrika Mashariki ya ufinyanzi ya Twyford, na milioni 480 dola za Marekani kwa kujenga jumba la biashara almaarufu Nairobi Global Trade Center.

    Aidha, makampuni haya yamewekeza rasilimali za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa maeneo ya viwanda katika miji mikuu ya Eldoret na Mombasa.

    Juhudi hizi, chini ya mpango wa mkanda mmoja njia moja kwa vyovyote vile zitainua uwezo wa Kenya kutekeleza maendeleo binafsi, kuongeza kasi ya nchi hiyo kuafikia ndoto ya viwandani na kupiga jeki mchakato wa kubuni nafasi za ajira.

    Chini ya mpango huu, serikali ya China pia inafadhili masomo kwa mamia ya wanafunzi kutoka Kenya kila mwaka kusoma nchini China. Na ili kukuza uhusiano wa karibu katika ya watu kutoka mataifa hayo mawili, serikali ya China imekuwa ikihamasisha wananchi wake kuzuru kenya kama eneo la utalii.

    Juhudi hizi zinaonekana kuzaa matunda kwani mwaka 2017 pekee, idadi ya watalii kutoka China waliozuru Kenya ilizidi elfu 60.

    Ethiopia ni taifa pekee barani Afrika ambalo limejaribu kutekeleza mfumo wa uchumi sawia na ya China. Kwa kuwekeza na kubuni ukanda wa maendeleo unaoiga mafanikio ya China, nchi hiyo ya Afrika Mashariki imekuwa ikitekeleza mpango kabambe wa kujenga maeneo ya viwanda.

    Kipengele muhimu katika suala hili ni eneo la viwanda la Hawassa, ambalo serikali ya Ethiopia inazingatia kuwa mfano kwa ujenzi wa kanda nyingine za viwanda nchini kote. Kiwanda hiki, kilichojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) imeonekana kufanikiwa baada ya kuvutia makampuni ya nguo na mavazi yenye tajiriba kuu.

    Kulingana na mpango uliopo, ifikiapo mwezi Juni, jumla ya maeneo 15 ya viwanda yaliyojengwa kupitia uwekezaji na utaalamu kutoka China yatakuwa yakiendesha oparesheni kikamilifu.

    Lakini Serikali ya Ethiopia inaamini kuwa ndoto yake ya kuwa kitovu cha viwandani barani Afrika itafaulu pia kwa kupitia maendeleo ya miundombinu bora ili kuwezesha mauzo ya nje kutoka viwandani.

    Takriban nusu ya viwanda hivyo viko kando kando mwa reli ya kisasa ya Addis Ababa-Djibouti ambayo pia imefadhiliwa na China. Reli hiyo imerahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka maeneo ya viwanda hadi kwenye bandari ya nchi jirani ya Djibouti.

    Reli hiyo yenye uwezo wa umeme wenye urefu wa kilomita 756, iliyoanza shughuli za biashara karibuni, imefupisha muda wa kusafirisha bidhaa kutoka Ethiopia hadi kwenye bandari ya Djibouti kwa kiasi kikubwa kwani hawali ilichukua masaa 48 ikilinganishwa na takriban masaa 10 kwa sasa.

    Bila shaka, hii itainua matarajio ya Ethiopia ya kuwa kitovu cha viwandani katika Afrika kufikia mwaka 2025.

    Aidha, makampuni ya Kichina kwa sasa yanatekeleza miradi 379 yanayoendelea au tayari kukamilika nchini Ethiopia.

    Bandari Mpya Tanzania

    Nchini Tanzania, kazi ya ujenzi wa mradi wa bandari ya Bagamoyo itakayogharimu takriban bilioni 10 dola za Marekani inatarajiwa kuanza karibuni. Serikali za Tanzania na China hatimaye zimeafikia makubaliano ambayo yatatoa fursa ya kungoa nanga kwa mradi huo ambao umekumbwa na masumbufu yaliyoikwamishwa.

    Kampuni kutoka China ya China Merchants Holdings International (CMHI) na State General Reserve Fund (SGRF) kutoka Oman yanaungana na serikali ya Tanzania kujenga kile ambacho wengi wanaamini kitakuwa bandari kubwa mno katika Afrika.

    Katika ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia mwaka 2016, shughuli ya wastani katika bandari ya Dar es Salaam imegharimu Tanzania na majirani zake bilioni 2.6 dola za marekani kila mwaka.

    Mradi wa nishati ya jua Misri

    Nchini Misri, kampuni ya nishati kutoka China imezindua ujenzi wa mradi mkubwa zaidi wa nishati ya jua katika Afrika ya Kaskazini. Mradi huo, unaotarajiwa kuzalisha megawati 186 ya nishati, unatazamiwa kukamilika mwaka ujao.

    Punde tu utakapozinduliwa, mradi huo wa vituo vinne vya nishati ya jua, utazalisha hadi gigawati 2 ambayo itatoa huduma kubwa zaidi kutokana na nishati ya jua.

    Miradi yanayotekelezwa kupitia mpango wa mkanda mmoja njia moja pia yanaonekana kuchukua sura katika sehemu ya Kusini mwa Afrika.

    Nchini Namibia, makampuni ya Kichina yanasaidia taifa hilo kutambua malengo yake ya kuwa kitovu cha utaratibu na usafirishaji wa watu na bidhaa. Kampuni ya China Harbour Engineering inajenga kituo kipya cha makasha au kontena na jeti la mafuta katika bandari yake huku nchi hiyo ikitazamia kutumia hili kama lango la kuingia eneo la kusini mwa Afrika.

    Nchini Msumbiji, daraja linalojengwa na China la Maputo litazinduliwa mwezi Juni. Taifa hilo lililoko kusini mwa Afrika linaamini kuwa mradi huo litafungua lango la kimataifa litakaloliunganisha na Afrika Kusini.

    Hali ya sasa katika mataifa tuliyoangazia ni thibitisho kuwa mpango huo wa mabilioni ya pesa unatoa nafasi bora kwa Afrika kupigana na changamoto za kimsingi kama vile miundombinu mbovu, ukosefu wa ujuzi na fedha za kutosha za kufadhili miradi, ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia hali ya umaskini na maendeleo hafifu barani.

    Ama kwa kweli China imeweka umuhimu mkubwa kwa mpango huu baada ya kuikita katika katiba yake. Kwa mujibu wa wataalam, utaratibu wa sasa wa mpango wa mkanda mmoja njia moja unaweza kusaidia Agenda 2063 ya Umoja wa Afrika inayolenga ukuaji, maendeleo endelevu na mabadiliko ya teknolojia barani Afrika.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako