• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Rais Xi aikaribisha Burkina Faso FOCAC

  (GMT+08:00) 2018-05-28 10:56:22

  Na Majaliwa Oswero

  Rais wa China Xi Jinping amemualika rasmi Rais wa Burkina, Faso Roch Marc Christian Kaboré, kushiriki mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika, FOCAC, utakao fanyika mwezi Septemba jijini Beijing.

  Kupitia kwa FOCAC, nchi za bara la Afrika na China zinajadili na kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo endelevu kati ya pande zote mbili.

  China imesema Burkina Faso, ambayo imevunja ushirikiano wa kidiplomasia rasmi na Taiwan wiki hivi karibuni, inayo nafasi kubwa kushirikiana na wenzake wa Afrika kupitia kwa jukwaa hilo linalolenga kuimarisha ushirikiano kati ya bara hilo na China.

  Tangu mwaka 1994, Burkina Faso imekua na uhusiano wa kidiplopmasia na Taiwan.

  Lakini kwa mujibu wa wachambuzi wa mambo ya kisiasa na kidiplomasia, changamoto mbalimbali za kidunia, kiuchumi na kijamii zimechangia Burkina Faso kufikiria upya msimamo wao.

  Tangu Rais Tsai Ing-wen aingie madarakani mwezi wa tano 2016, Burkina Faso imekuwa nchi ya tano kuvunja ushirikiano wake wa kidiplomasia na Taiwan ikitanguliwa na Jamhuri ya Dominica, Gambia, Sao Tome na Principe na Panama.

  Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Kisiwa cha Taiwan hadi sasa kimebaki na ushirikiano wa kidiplomasia na nchi 18 tu duniani.

  Akizungumza muda mfupi baada ya kubadilishana hati za makubaliano za kurejesha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya China na Burkina Faso, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Bw. Wang Yi, alisema wanayo furaha kuikaribisha nchi hiyo ya Afrika ya Magharibi katika 'familia yao'.

  Bw. Wang alimwambia mwenzake wa Burkina Faso kuwa Rais Xi amemuagiza amfikishie mwaliko wake kwa Rais Kaboré kushiriki mkutano wa FOCAC hapo mwezi wa tisa.

  "Tukio la leo linafungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina ya Burkina Faso na China. Ni tukio la kihistoria lenye maana kubwa sana...Rais Xi anamualika Rais Kaboré kuhudhuria mkutano wa FOCAC ili kujadiliana namna ya kushirikiana katika mambo mbalimbali kati ya nchi hizi mbili," Bw. Wang alisema.

  Alisema uamuzi wa Burkina Faso kuvunja ushirikiano wake na Taiwan ni sahihi na China inaunga mkono hatua hiyo itakayotoa nafasi kwa nchi hizo mbili kuanzisha ushirikiano mpya kwa ajili ya maendeleo endelevu.

  "Tunafurahi kuwa na mwanachama mpya katika familia yetu, tunatumaini tutakuwa na ushirikiano mzuri wenye uaminifu kama tunavyofanya na nchi zingine za bara la Afrika," aliongeza Bw. Wang.

  Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Bw. Alpha Barry nchi yake ilichukua uamuzi wa kuvunja ushirikiano na Taiwan kwa nia njema ya kutetea maslahi ya Burkina Faso na raia wake katika mzunguko mzima wa mataifa na kujenga ushirikiano bora katika kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuwezesha miradi ya kikanda.

  Aliongeza kuwa kuna China moja tu duniani na lazima wawe pamoja ili kuanzisha ushirikiano mpya huku akikaribisha makampuni na wawekezaji kutoka China kutembelea Burkina Faso kujionea fursa za biashara na uwekezaji kwa faida ya pande hizo mbili.

  Bw. Barry pia aliipongeza China kwa hatua kubwa ya kimaendeleo iliyopiga inayoifanya kuwa moja ya mataifa makubwa yenye uchumi bora duniani.

  Kutokwepo na maelewano mazuri kati ya China na Taiwan ni matokeo ya mivutano ya tofauti za mitazamo ya kisiasa ya wafuasi wa vuguvugu la utaifa (Nationalist ) wenye kupendelea mfumo wa uchumi wa Kibepari dhidi ya wafuasi wa sera za kiuchumi za kijamaa (Communist).

  Hata hivyo serikali zote mbili ziliweka msimamo wa kuitambua China moja tu, hivyo basi ziliweka sharti kwa mataifa mengine kuwa hayaruhusiwi kuwa na uhusiano rasmi na serikali zote mbili kwa pamoja kwa madai kuwa kufanya hivyo kunachochea mgawanyiko wa China.

  Hivyo kama nchi fulani itakuwa na uhusiano rasmi na Jamhuri ya China (Taiwan) italazimika kuvunja uhusiano rasmi na Jamhuri la watu wa China au kinyume chake.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako