• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Uwekezaji China Afrika kuongezeka 2018

  (GMT+08:00) 2018-05-31 10:31:51

  Na Majaliwa Oswero

  Uwekezaji wa China barani Afrika ukiwa umefika jumla ya dola za Kimarekani bilioni 170 mwaka jana, Wizara ya Biashara ya China imesema kwa mwaka huu wa 2018, inategemea uwekezaji huo kuongezeka.

  China ni mbia mkubwa wa biashara na uwekezaji barani Afrika, na kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Biashara, uwekazaji wa China barani humo umeongezeka mara kumi na tano katika kipindi cha mwaka 2000 na 2017.

  Vilevile, rekodi zinaonyesha kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini China kutoka nchi za bara la Afrika hadi kufikia mwaka jana, zimeongezeka kwa asilimia zaidi ya 30.

  Baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini China, kutoka barani Afrika ni pamoja na kahawa, kokoa, pamba, matunda, madini, karanga na mihogo.

  Bidhaa zinazosafirishwa kutoka China kwenda Afrika ni pamoja na nguo, vyombo vya nyumbani, samani na vifaa vya kielektroniki.

  Pamoja na China --nchi ya pili kwa uchumi bora duniani, kusafirisha bidhaa zilizokwishatengenezwa, lakini pia imewekeza barani Afrika kwa kuanzisha viwanda vinavyotengeneza bidhaa mbalimbali zinazouzwa barani humo.

  Akizingumza na waandishi wa habari kutoka Afrika walio katika programu maalum ya mafunzo nchini China, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Asia Mashariki na Afrika katika Wizara ya Biashara, Bw. Jiang Wei, alisema mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika unazidi kuimarika siku hadi siku.

  Alisema pande hizo mbili zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kibiashara uliojengwa katika misingi ya undugu, kuaminiana na kunufaishana, huku Serikali ya China ikiendelea na azma yake ya kuimarisha uwekezaji zaidi katika nyanja mbalimbali barani Afrika

  "China na Afrika wamekuwa zaidi ya wabia katika biashara. Pande hizi mbili kwa sasa ni ndugu na uhusiano wao umetawaliwa na urafiki wa hali ya juu kiasi cha kufanya uwekezaji kati yao kuongezeka na kuimarika zaidi," alisema Bw. Jiang.

  Aliongeza kuwa, pamoja na kwamba hadi nwaka jana uwekezaji wa China barani Afrika ulifika dola bilioni 170 za Kimarekani, ni mategemeo yao kuwa kwa mwaka huu wa 2018, uwekezaji wao utaongezeka na kuendelea kunufaisha pande zote mbili.

  Bw. Jiang alisema kuwa kila mwaka, uwezekezaji wa moja kwa moja barani Afrika unafika kiasi cha dola za Kimarekani bilioni tatu.

  Alisema kuwa pia wameweza kubainisha maeneo mbalimbali kwa ajili ya ukanda maalum wa viwanda takribani 20 barani Afrika, huku wakiendelea kushirikiana na serikali za nchi za Afrika katika kuangalia maeneo mapya muhimu na bora kwa ajili ya uwekezaji na uendelezwaji.

  Hadi mwaka 2016, kwa mujibu wa Bw. Jiang, China imeweza kuwekeza jumla ya dola za Kimarekani bilioni 40 barani Afrika kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali ili kurahishisha uwekezaji wao barani humo.

  "Pia tunaweka kipaumbele katika kuhakikisha miundombinu barani Afrika kama barabara na reli zinaboreshwa. Tunaamini kuwa ukitaka kuwa tajiri anza kwa kujenga barabara na kuboresha miundombinu kwa ujumla," alisisitiza Bw. Jiang.

  Mkurugenzi Jiang alisema kuwa Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika, FOCAC, unaojumuisha nchi 52 za Afrika zenye uhusiano wa kidiplomasia na China pamoja na Umoja wa Afrika (AU), umezidi kuboresha na kuchochea uwezekaji wa China barani Afrika.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako