• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yataka Afrika kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji

    (GMT+08:00) 2018-05-31 10:34:00

    Na Majaliwa Oswero

    China imetoa changamoto kwa bara la Afrika kuhakikisha linazidi kuweka mazingira mazuri ikiwemo sera rafiki ili uwekezaji wake barani humo uzidi kuboreka kwa manufaa ya pande zote mbili.

    Utawala bora, amani na utulivu pamoja na sera bora na sheria nzuri za kodi zitaiwezesha bara hilo kuvutia uwekezaji zaidi kutoka China, Wizara ya Biashara nchini humo imesema.

    Akizungumza na waandishi wa habari kutoka barani Afrika jana jijini Beijing, Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya bara la Asia Mashariki na Afrika kutoka wizara ya Biashara Bw, Jiang Wei, alisema pamoja na China kuweka azma ya kuendelea kuimarisha uwekezaji wake barani humo, mazingira hayo wezeshi ni muhimu kuzingatiwa.

    Bw. Jiang alisema bara la Afrika lina kila kitu muhimu kwa uwekezaji ikiwemo malighafi, soko linalotokana na idadi kubwa ya watu pamoja na uhitaji, hivyo si budi serikali za nchi za bara hilo kuongeza kasi katika kusawazisha maeneo machache yanayoweza kuonekana kama kikwazo katika biashara na uwekezaji.

    China ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na uwekezaji mkubwa barani Afrika, na imeazimia kuwa uwekazji wake barani humo utazidi kuongeza kila mwaka kutokana na kuimarika kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili.

    Hadi kufikia mwaka jana 2017, uwekezaji wa China barani Afrika ulifika dola za Kimarekani bilioni 170, ikiwa ni ongezeko zaidi ya mara kumi na tano kutoka mwaka 2000.

    Bw. Jiang alisema kuwa kila wanapokutana na viongozi wa nchi za Afrika kujadiliana kuhusu namna ya kuboresha na kuhimarisha uwekezji wao barani humo, wamekuwa wakiwaeleza viongozi hao changamoto hizo ili waweze kuzifanyia kazi.

    "Tumeona Afrika bado ni sehemu sahihi na bora kwetu sisi kuwekeza. Yapo tu maeneo machache ambayo yakifanyiwa kazi, uwekezaji wetu utaongezeka maradufu na nchi zetu zitanufaika zaidi kuliko sasa," alisema Mkurugenzi Jiang.

    Bw. Jiang aliongeza kuwa uwekezaji na biashara zinahitaji sera nzuri, mazingira rafiki, utawala bora na amani na utulivu --vitu ambavyo ni changamoto kwa baadhi ya nchi za Afrika.

    Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika, FOCAC, uwekezaji wa China barani Afrika umekuwa ukiongezeka na kuwa imara zaidi.

    Kwa mujibu wa Bw. Jiang, ni jukumu la wizara ya Biashara hasa kitengo cha Masula ya Afrika kuhakikisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Afrika na China unaimarika na pande hizo mbili zinanufaika.

    Alisema kuwa kutokana na umuhimu wa bara la Afrika katika uwekezaji na biashara, rais wa China, baada ya kuingia madarakani, alichagua Afrika kama sehemu yake kwanza kutembelea ili kuimarisha uhusiano na kuweka msingi thabiti wa diplomasia ya kiuchumi kati ya pande hizo mbili.

    Bw. Jiang pia aliongeza kuwa China chini ya uongozi wa rais wa China imekuja na mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja, kiuhalisia, kwa nia njema ya kuunganisha bara la Afrika, Asia na Ulaya ili kurahisisha uwekezaji na biashara katika kanda hizo.

    Alisema kwa miaka tisa mfululizo, China imekuwa mbia namba moja wa uwekezaji na biashara barani Afrika, hivyo ni vyema uhusiano huo ukaendelea kujengewa mazingira mazuri ili uweze kukuwa na kuimarika maradufu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako