• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Bijie: Mji uliotangazwa eneo hatari kuishi ulivyojipanga kumaliza umaskini 2020

  (GMT+08:00) 2018-08-20 08:52:59
   

  Oswero, Bijie

  Umaskini ni hali ya ukosefu wa mahitaji ya msingi ya binadamu kama vile chakula, maji salama, huduma za afya, mavazi na nyumba kutokana na kukosa uwezo wa kuvinunua.

  China pamoja na kuwa nchi ya pili kwa kuwa na uchumi mkubwa duniani, baada ya Marekani, imepitia katika hali ngumu ya maisha na wananchi wake katika baadhi ya maeneo bado wanaishi katika umaskini.

  Inakadiriwa kuwa hadi sasa watu takribani milioni 30 bado wapo katika umaskini huku serikali ikiweka mpango wa kuhakikisha ndani ya miaka mitatu (hadi 2020) umaskini unakuwa ni historia.

  Bijie ni mji wenye wakazi wapatao milioni 9.2 na unapatikana katika jimbo la Guizhou, Kusini Magahribi mwa China.

  Kwa miaka ya nyuma haikuwa na sifa yoyote zaidi ya kujulikana kuwa na wakazi wanaoshi katika lindi kubwa la umaskini.

  Hali ya umaskini uliokithiri uliochangiwa na hali mbaya ya mazingira ulisababisha mji huu kutangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kama moja ya maeneo hatari yasiyofaa kwa makazi ya binadamu.

  Katika miaka ya 1980, mji huu ulighubikwa na hali ngumu ya kiuchumi, mabadiliko ya tabia nchi yaliyoathiri mazingira pamoja kuongezeka kwa idadi ya watu, hali iliyofanya hali kuwa mbaya zaidi.

  Kutokana na hali hii, baraza la serikali ya China iliazimia kujenga ukanda maalum wa majaribio wa Bijie kwa malengo makuu matatu --kupunguza umaskini kwa kutekeleza mipango na miradi mbalimbali ya maendeleo, kujenga na kudumisha ekolojia pamoja na kudhibiti idadi ya watu.

  Baada ya miaka 30 ya mradi huu, kutokana na jitihada, utayari, juhudi na mapinduzi ya kifikra miongoni mwa wakazi wa mji huu, tatizo la umaskini umepungua kwa asilimia kubwa na sasa watu wana uwezo wa kupata huduma zote muhimu za kibinafsi na kijamii.

  Kwa sasa wananchi hawa hofu juu ya nini cha kuvaa, nini cha kula wala pakulala na wala hawana hofu juu ya huduma za afya, elimu na hata miundo mbinu ya barabara zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa.

  Miradi mbalimbali iliyoanzishwa ili kuweza kukwamua wananchi wa eneo hilo kutoka katika dimbwi la umaskini, ni pamoja na, mashamba ya kisasa ya mboga na matunda, ufugaji wa kisasa wa ng'ombe wa maziwa na nyama pamoja na kuhakikishiwa miundombinu muhimu na masoko kwa ajili ya mavuno.

  Pamoja na hatua hii, serikali pia ilianza kutoa ruzuku kwa wananchi mbalimbali wa eneo hili na kutoa ushauri wa namna bora ya kutumia ruzuku hiyo kujikwamua na kuondokana na umaskini wa kipato na mahitaji muhimu ya kila siku.

  Hadi kufikia mwaka 2015, watu waliokuwa bado wanaishi kwenye umaskini katika mji wa Bijie ulifikia milioni moja.

  Kwa mujibu wa taarifa wa maafisa wa serikali katika eneo hilo, serikali ilitoa jumla ya RMB bilioni 11 kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali ya uzalishaji na inategemewa kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka huu 2018, jumla ya watu 180,000 watakuwa wamefikiwa na kusaidiwa kuagana na umaskini.

  Katika malengo yao hadi kufikia mwaka 2020, wakazi wote wa mji wa Bijie watakuwa wameondolewa katika lindi la umaskini na watakuwa na uwezo wa kipato na wa kumudu mahitaji ya msingi ya kila siku ya maisha.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako