• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Afrika yapaswa kufwatilia kwa karibu matukio katika mikutano miwili ya kisiasa nchini China

    (GMT+08:00) 2019-03-04 08:44:25

    Na Eric Biegon – NAIROBI

    Kila mwaka, vyombo vikuu vya kisheria nchini China huitisha mikutano kwa kile ambacho ni kongamano lenye shughuli nyingi hasa katika kuweka ajenda ya mwaka unaofuata. Hii ni pamoja na ajenda ya Rais kwa China na ulimwengu.

    Desturi hii ya kila mwaka, inajulikana kama Mikutano Miwili au Two Sessions, na ni wakati ambapo bunge la China, maarufu kama kongamano la watu la kitaifa (NPC), hukutana kwa wakati mmoja na Baraza la Mashauriano la Kisiasa nchini humo (CPPCC).

    Kwa muda mrefu, mkutano huu wa kila mwaka haukuwa na mvutio kutoka kwa mataifa ya nje, hasa katika bara la Afrika. Hii kwa kiasi kikubwa ilitokana na Beijing kutojihusisha na masuala ya dunia kama inavyofanya kwa sasa. Hali ya sasa imebadilika mno na kila mmoja Afrika lazima aipe kipaumbele matukio nchini humo.

    Ushawishi wa China barani Afrika umeongezeka pakubwa na idadi kubwa ya wachanganuzi wa masuala ya kisasa barani humo wanasadiki kwamba Afrika haiwezi tena kufumbia jicho matukio katika Beijing.

    Swala kuu wakati huu ni mawazo ya Rais Xi Jinping kuhusu sifa za ujamaa za Kichina kwa zama mpya. Hii ni muhimu hasa kwa Afrika kwani inaelezea itikadi ya Kichina kwa mapana na marefu. Itikadi hii inapendekeza njia mbadala ya kuongoza mataifa, njia mbadala kwa ajili ya kutekeleza maendeleo ya kiuchumi, pamoja na mtindo tofauti wa kushiriki maendeleo na dunia.

    Ingawa ni njia moja ya raia wa China kutoa usemi katika masuala ya uongozi nchini mwao, kiongozi wa China Rais Xi Jinping anatumia mkutano huu wa kila mwaka kusisitiza vipaumbele vya serikali yake kwa Wachina na mataifa ya nje. Sera zitakazopewa kipaumbele wakati wa Mikutano Miwili zitasaidia kuweka wazi iwapo China itabadilisha mikakati yake ya hivi karibuni juu ya Afrika.

    Kwa mfano, wakati wa mkutano wa mwaka uliopita, serikali ilitangaza kuanzishwa kwa mashirika mapya ya kuratibu misaada ya kimataifa hasa katika Afrika. Uamuzi huo bila shaka unashawishi jinsi na namna China inahusiana na mataifa Afrika. Pia unadhihirisha haja kubwa ya China kushiriki katika masuala yanayoghusia ustawi wa bara.

    Itakumbukwa kwamba mwenyekiti wa 9 wa Baraza la CPPCC Wang Yang alifanya ziara ya nchi tatu za Afrika mwezi Juni mwaka jana. Bwana Wang alitembelea Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alipokuwa Kenya, kwa mfano, Wang alitoa ahadi kwamba serikali ya China itatoa fedha kufadhili shughuli za utafiti na uvumbuzi zaidi katika jitihada za kuongeza maendeleo ya kiuchumi katika bara la Afrika.

    Akizungumza katika Kituo cha Utafiti cha pamoja cha China na Afrika yenye makao yake katika chuo kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta, Wang alisisitiza haja ya Wakenya na Waafrika kwa jumla kubadili mwelekeo wao na kuukumbatia ubunifu, kwani hii ni injini inayosukuma uchumi katika nchi zilizoendelea. Ni hapa alikotoa ahadi kwamba China itasaidia katika juhudi hizi.

    Inawezekana kwamba Wang aliwasilisha ushauri wake juu ya njia bora ya kusaidia Afrika kuafikia malengo yake ya maendeleo na kuna uwezekano kuwa swala hilo litajadiliwa wakati wa mkutano huo wiki ijayo.

    Bila shaka mpango maksusi wa Ukanda Mmoja Njia Moja utajadiliwa pia kwani kwa sasa umejikita kikamilifu katika katiba ya chama tawala cha CPC. Kupitia mpango huu, nchi nyingi za Afrika zilipata jukwaa la ushirikiano mbadala na serikali ya China. Marekebisho yoyote kwa mpango huu bila shaka yataathari sera za China kwa mataifa ya kigeni.

    Kwa sasa, Afrika bado inasukuma mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC). China imekuwa mstari wa mbele kupiga jeki shinikizo kutoka Afrika kuwa na uwakilishi wake katika baraza hilo. Swala hilo huenda likajadiliwa katika vikao hivyo.

    Si siri kwamba China imepanua juhudi zake za kijeshi duniani. Kwa sasa idadi kubwa ya majeshi yake yanalinda usalama nchini Djibouti. Huenda swala kuhusu msaada wa usalama barani Afrika likajadiliwa na wajumbe wakataoudhuria kongamano hilo.

    Swala la uchumi bila shaka litapewa umuhimu mkubwa miongoni mwa wajumbe zaidi ya 3000 watakaoshiriki mikutano hiyo ya wiki mbili. Lakini huku kukiwa na matarajio mbalimbali, China imesisitiza kwamba uhusiano wake na mataifa ya nje, zikiwa ni pamoja na zile za Africa, kamwe hazitakwamishwa na hali yake ya kiuchumi, na kuahidi kutimiza ahadi zake kwa bara.

    Mikutano hiyo bila shaka yana umuhimu mkubwa kwa bara la Afrika, kama vile mataifa mengine ulimwenguni, na hayawezi kupuuzwa.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako