• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Bunge la China Katika Jicho la Mwanahabari wa Afrika

    (GMT+08:00) 2019-03-05 08:39:07

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    CHINA ni nchi yenye jumla ya watu takribani bilioni 1.4, inayopatikana Asia ya Mashariki na inabaki kuwa nchi yenye siasa za kipekee duniani.

    Kama ilivyo nchi zote, Bunge ni chombo muhimu cha uwakilishi wa wananchi.

    Ndicho chombo cha kutunga sheria, kuidhinisha na kupitisha bajeti na kujadili masuala mbalimbali ya nchi.

    Mwaka jana, 2018, nilikuwa miongoni mwa wanahabari zaidi ya 3,000 waliohudhuria, kuandika na kuripoti habari zote za mkutano huu muhimu kwa Jamhuri ya Watu wa China.

    Pamoja na uzoefu wangu wa kushiriki shughuli za Bunge nchini Tanzania ulionifanya nifikirie kuwa ninao uzoefu wa kuripoti shughuli za Bunge lolote duniani, nchini China mambo yako tofauti.

    Tofauti na nchi nyingi ulimwenguni, Bunge la umma la China linakaa mara moja tu kwa mwaka na huwa linaketi mwezi wa tatu kwa muda usiozidi wiki mbili.

    Mikutano Miwili au "Two Session" kama inavyojulikana kwa Kiingereza, chombo hiki huwa na wawakilishi kutoka majimbo yote ya China na huwa linapokea utendaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za serikali kwa kipindi cha mwaka mzima na pia hujadili na kupitisha mipango na shughuli za serikali kwa mwaka unaokuja wa fedha.

    Kwa uzoefu wangu, na kwa kupitia katika ripoti mbalimbali za uendeshwaji wa mabunge mbalimbali duniani, Bunge la Umma China linabakia kuwa moja kati ya ile ambayo inafatiliwa sana ndani na nje ya nchi hiyo.

    Mbali na waandishi wa habari wa ndani, wanahabari wa kimataifa ambayo idadi yao hufikia karibia 1,000 wanashiriki kuripoti taarifa za Bunge hili.

    Ni kweli kuwa ikiwa ni nchi ya pili kwa utajiri duniani lazima mambo yake yavutie dunia na kufatiliwa kwa ukaribu lakini upekee wa siasa zake na namna ya ufanyaji wa mambo yake pia yanaipa China upekee kiasi kwamba hata vyombo vya habari vya kimataifa hupata shauku ya kufatilia na kuripoti shughuli zake.

    Mwaka jana, nikiwa nashiriki kwenye kuripoti shughuli za Bunge la Umma la China, nilipata pia kuripoti marekebisho ya katiba yaliyoondoa ukomo wa urais lakini pia shughuli za kuchaguliwa kwa rais na viongozi wakuu wa nchi hiyo iliyofanywa na Bunge hili.

    Hili la Bunge kushiriki kuchagua viongozi wakuu wa nchi ni moja ya mambo ambayo inaipa China upekee katika duru za siasa.

    Hili ni jambo ambalo kabla ya kubahatika kuwa miongoni mwa wanahabari 1,000 wa kimataifa waliopata mwaliko maalum kuripoti shughuli hizo sikuwa ninalijua.

    Macho yote duniani kwa sasa yameelekezwa katika matukio makubwa ya kisiasa yanayoendelea jijini Beijing, sababu kubwa ikiwa ni kuwa taifa hili ni miongoni mwa mataifa makubwa yanayogusa moja kwa moja mustakabali wa ustawi wa nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea.

    kwa sababu hiyo, maamuzi yote ya kisiasa yanayofanyika lazima yafatiliwe kwa ukaribu na mataifa yote.

    Tumezoea kuona kote duniani, shughuli za uchaguzi hasa kwa nafasi kubwa na juu kama ya Urais huambatana na maandalizi ya awali ikiwemo shughuli za kampeni na shamrashamra zingine.

    Lakini, kwa nchi ya China hali ni tofauti. Wawkilishi wa wananchi kupitia Bunge lao ndio hufanya shughuli ya kumchagua rais pamoja na viongozi wengine.

    Huu ni uzoefu wa pekee na uelewa niliyopata baada ya kushiriki kwenye shughuli hizi za Bunge maalum la China, mwaka jana 2018.

    Huwa linaanza kukaa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa na hufuatiwa na Bunge la Umma ambacho ndicho chombo kikuu kabisa cha kikatiba cha kufanya maamuzi yote yanayohusu taifa.

    Hiki ndicho chombo kinachochagua rais, serikali, kamati kuu ya kijeshi na mwanasheria mkuu.

    Vilevile, kama ilivyokuwa na uwezo wa kuwateua hao ndivyo ambavyo pia kimepewa madaraka ya kuwafukuza kazi maramoja pale inapothibitika kwenda kinyume na maslahi na matakwa ya taifa.

    Nini kinafanya siasa za China kuwa za kipekee? Ni swali la kawaida lakini zito, kwanza pamoja na kuwa taifa hili linaongozwa na chama cha Kikomunisti, lakini pia kuna vyama vingine vya kidemokrasia vinane. Hivi vyama vyote ni sehemu ya maamuzi na vinaunga mkono chama tawala cha Kikomunisti.

    Kwa siasa za Afrika, ni ngumu kukuta chama kisichokuwa madarakani kuunga mkono juhudi za chama tawala isipokuwa pale tu kunapotokea kutoelewana na kulazimika kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

    Hali kama hii ilishawahi kutokea katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya na Zimbabwe ambapo kulitokea hali ya kutoelewana baada ya uchaguzi na ili kulinda umoja na amani, serikali za umoja wa kitaifa ziliundwa.

    Lakini upekee mwingine katika siasa hizi ni namna bunge lilivyopewa madaraka makubwa sana. Kwa nchi hii, bunge ni mamlaka na mamlaka ni bunge.

    Kama hili halitoshi, kutofautisha bunge, chama na serikali siyo kazi rahisi.

    Bunge la umma la China, kiuhalisia, maazimio yake yote ni utekelezaji tu wa maazimio ya uongozi wa chama cha kikomunisti ambacho ndicho chama tawala.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako