• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wawekezaji China wazidi kumiminika Tanzania

    (GMT+08:00) 2019-03-05 08:40:15

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    CHINA na Tanzania zimezidi kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji baada ya makampuni 13 toka nchi hiyo ya Asia ya Mashariki kutembele Tanzania na kusema wanataka kuanzisha uwekezaji mpya wenye dola za kimarekani milioni 167.

    Maeneo watakayowekeza ni pamoja na kuanzisha kiwanda cha mabehewa ya treni, betri za magari na kiwanda cha vifungashio.

    Wawakilishi wa makampuni hayo 13 ya China wamezuru katika nchi iyo ya Afrika Mashariki miezi michache baada ya wengine 17 kutembelea nchi hiyo na kufanya mazungumzo na Kituo cha Uwekezaji Tanzania, TIC, juu ya namna bora ya kuanzisha na kuendeleza uwekezaji katika sekta mbalimbali.

    Kwa mujibu wa taarifa za TIC, China inaendelea kuongoza kwa kuweka mitaji mikubwa nchini Tanzania kwa zaidi ya dola bilioni 5.8 duniani katika uwekezaji kuanzia mwaka 1990 mpaka 2017.

    Ushirikiano wa Tanzania na China katika sekta mbalimbali unazidi kuimarika kila mwaka katika kuhakikisha nchi hizo mbili kila moja inanufaika.

    Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, uwekezaji wa China nchini Tanzania umeongezeka mara kumi katika kipindi cha miaka sita kutoka dola za Kimarekani 672.6 milioni hadi dola bilioni 6.7.

    Wawakilishi wa makampuni hayo 13 wamekutana na Kituo Cha Uwekezaji Tanzania pamoja na uongozi wa Mkoa wa Pwani ambapo wanataka kuanzisha uwekezaji huo, unaotarajiwa kuongeza ajira kwa Watanzania na kufanikisha azma ya Rais John Magufuli ya kuimarisha uchumi wa viwanda.

    Uwekezaji huo utafanyika katika eneo la uwekezaji la Kiluwa Free Processing Zone, mkoani Pwani, nje kidogo ya jijini la kibiashara la Dar es Salaam.

    Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo aliwahikishia wawekezaji hao walioletwa nchini na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni za Kiluwa Group, Bw Mohamed Kiluwa kuwa uongozi wake utashirikiana na wafanyabiashara hao kuhakikisha shughuli zao mkoani humo zinafanyika vizuri kwa maslahi ya Tanzania na China.

    "Kwa kuzingatia fursa zilizopo hapa nchini hususan hapa mkoani, wameamua kuja kuwekeza hapa na wapo tayari kufanya hivyo muda wowote baada ya kupata ardhi. Wana mtaji na teknolojia ya kutosha.

    Baada ya wiki moja au mbili tutakuwa tumeshawapa majibu juu ya upatikanaji wa eneo ili waanze shughuli zao mara moja," alisema Mkuu wa Mkoa wa Pwana Bw. Ndikilo.

    Aliongeza kuwa kati ya wawekezaji hao 13, sita tayari wameshaingizia nchini vifaa na mashine mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa shughuli hizo za uwekezaji.

    "Lazima tuwape ushirikiano wa hali ya juu wawekezaji wanaokuja kuunga mkono jitihada za nchi yetu kufikia Uchumi wa Viwanda," alisisitiza.

    Kwa upande wake, Bw. Kiluwa alishukuru Kituo Cha Uwekezaji Tanzania kwa kuweka mifumo na namna bora ya kuhimiza na kulete wawekezaji, hali iliyomsaidia kufanya mazungumzo na makampuni hayo ya China na hatimae kukubali kuingia nchini kufanya makubaliano ya kuanza uwekezaji.

    Aliongeza kuwa tayari ameshaweka kila kitu sawa ikiwepo miundombinu muhimu kwa ajili ya shughuli hizo huku akiomba serikali iharakishe taraibu za kuwakabidhi ardhi kwa wawekezaji hao.

    Bw. Lu Xiaoqiang, Naibu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sinoma East Africa Limited, akizungumza kwa niaba ya wawekezaji hao, alisema wanataka kushirikiana na Tanzania kufanya shughuli mbalimbali za uwekezaji.

    Alisema kampuni yake itawekeza katika viwanda vya plastiki na betri za magari.

    "Tuna mipango mikubwa kwa siku za baadae, tunataka kuendeleza mambo mengi na wazawa wa hapa kwa faida ya pande zote mbili," alisema Bw. Lu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako