• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Matumaini Mapya Usawa wa Biashara China ikitangaza Mfumo wa Soko Huria wa Kisasa

  (GMT+08:00) 2019-03-07 08:47:30

  Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

  CHINA imetangaza kuboresha mazingira ya kibiashara mwaka huu. Waziri mkuu wa China Li Keqiang ameweka hili wazi katika ripoti yake ya kazi ya serikali mbele ya wajumbe wa Bunge la Umma jijini Beijing.

  Mwezi Novemba mwaka jana, katika Maonesho ya kwanza ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje yaliyofanyika Shanghai, Rais wa China Xi Jinping akifungua maonesho hayo, alisisitiza kuwa nchi hiyo itaangalia namna ya kupitia mifumo, sheria na taratibu zinazoongoza biashara na uwekezaji kati ya nchi hiyo na mataifa mengine.

  Kauli ya Waziri Mkuu Bw. Li ya kuwa China itaharakisha kujenga mfumo wa pamoja wa soko huria wa kisasa --ulio wazi na wa ushindani wenye utaratibu, na kuweka mazingira ya biashara ya kufuata sheria za kimataifa inaweka msisitizo kwa dhamira ya nchi hiyo kuhakikisha inasimamia misingi ya baishara yenye usawa duniani.

  Vilevile, sera ya Mageuzi na Ufunguaji Mlango ulioanzishwa miaka 40 iliyopita ambayo kimsingi inalenga kuweka mazingira ya kuruhusu kampuni za nje kuwekeza na kufanya biashara China itakuwa inazidi kupata msukumo mpya baada ya kutekelezwa kwa mafanikio makubwa kwa kipindi hicho cha muiongo minne.

  China nchi ya pili kwa utajiri na inayoongoza kwa idadi kubwa ya watu duniani, kwa muda imekuwa na orodha kubwa ya sekta ambazo zilikuwa zimewekewa zuio la kuingia kwenye soko huria.

  China kwa mujibu wa Shirika la Biashara Duniani, ndio inaongoza kwa uuzaji wa bidhaa nje ya nchi kuanzia mwaka 2009.

  Jana, serikali ya China imetangaza kuwa itapunguza zaidi orodha ya sekta za kuzuiliwa kuingia kwenye soko, kuhimiza utekelezaji wa kanuni ya kutoa ruhusa ya kuendesha biashara kwa kufuata sheria na kupunguza kwa kiasi kikubwa mgawanyo wa rasilimali wa moja kwa moja.

  Hatua hii itakuwa na faida kwa China lakini pia kwa dunia kwa ujumla ikizingatiwa kuwa nchi hiyo bado inaongoza kwa biashara na uwekezaji ndani na nje ya nchi.

  Nchi ambazo China inaongoza kuuza bidhaa zake ukiachilia bara la Afrika ni pamoja Marekani, Japana, India, na Vietnam.

  Ni dhahiri kuwa hatua ya China kutangaza kuharakisha kuondoa kanuni na vitendo vinavyozuia umoja wa soko na ushindani wenye usawa utakuwa ni fursa nyingine kwa dunia kushuhudia ukuaji wa biashara na uwekezaji na kuondoa msuguano usiokuwa na tija kw ustawi wa uchumi wa dunia.

  Mwaka jana, katika ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Bidhaa za Nje yaliyofanyika Shanghai, Rais wa Kenya, Bw. Uhuru Kenyatta kwa niaba ya viongozi wa Afrika, alisema kuna umuhimu wa China kuangalia namna ya kupitia ushuru kwa bidhaa kutoka barani Afrika ili kuweka sawa urari wa biashara kati ya pande hizo mbili.

  Rais Uhuru alisema kuwa China ikiendelea kuwa kinara wa biashara na uwekezaji barani Afrika, kuna haja nchi iyo ya Asia ya Mashariki kuangalia namna ya kuboresha mazingira yatakayovutia na kutoa fursa kwa wafanyabiashara na wawekezaji kutoka bara hilo pia kunufaika zaidi na fursa za biashara zilizopo China.

  Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Biashara ya China, bidhaa kutoka nchi hiyo zilizouzwa barani Afrika mwaka 2018 katika miezi saba ya mwanzo ilikuwa na thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni 59.36 ikiwa ni ongezeko la asilimia 8.8 kwa mwaka 2017.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako