• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • CHINA: Hatuna mpango wa kuitawala Afrika

    (GMT+08:00) 2019-03-08 17:58:28
    Na DEOGRATIUS KAMAGI, Beijing

    China imefafanua kwamba haina lengo la kuzitawala nchi za Afrika kupitia misaada ambayo imekua ikiitoa, bali kuzisaidia nchi zinazoendelea katika kuinua pato la taifa pamoja na kuondokana na umasikini.

    Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa na waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika hapa jijini Beijing.

    Amesema kwa muda mrefu, China imekua na ushirikiano mzuri na nchi za Afrika hasa katika ujenzi wa miradi mingi ya maendeleo kama vile miundombinu, huduma za kijamii, biashara na masuala ya kidiplomasia, na kwamba wanatarajia mahusiano hayo yaendelee kwa manufaa ya pande zote.

    Kauli ya Bwana Wang imekuja kufuatia tetesi ambazo zimekua zikienea katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuripotiwa na vyombo kadhaa vya habari barani Afrika kwamba misaada mingi ambayo taifa hilo la pili kwa uchumi duniani limekua likiitoa, ina lengo la kudhofisha nchi zinazoendelea.

    "Nchi za Afrika ni marafiki wetu wakubwa ambao tumekuwa tukishirikiana nao kwa kipindi kirefu, sio kweli kwamba China inataka kutawala Afrika, lengo kubwa ni kuleta ushirikiano wenye tija kwa manufaa ya Afrika na nchi ya china," alisema.

    Wang, ambaye alitumia muda mwingi kupokea na kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari aliongeza kuwa ni muhimu kwa mataifa yote kuendelea kushirikiana ili kuleta maendeleo ya kweli.

    Alisema "Tunahitaji maendeleo ya kweli na hayo yatafikiwa endapo tu sote tutajizatiti na kufanyia kazi malengo tuliyojiwekea ikiwemo uekelezaji wa miradi ya Ukanda Mmoja, Njia Moja ambao utaleta mapinduzi katika sekta ya biashara na usafirishaji".

    Mwanadiplomasia huyo mzoefu aliongeza kwamba moja ya mipango ya mwaka huu ni kuhakikisha maazimio yote nane yaliyofikiwa mwaka jana katika mkutano wa jukwaa la ushirikiano kati ya Afrika na China yanafikiwa.

    Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alisema ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika umekuwa na tija kubwa huku akiunga mkono kauli ya waziri Wang kuwa misaada ya China kwa nchi zinazoendea haina nia hasi.

    "Hizo zote ni propaganda zinazoenezwa na mataifa yasiyozitakia mema nchi za Afrika, hawataki Afrika iendelee," alisema.

    Aliongeza "Ukiangalia kwa undani utaona kwamba nchi zinazoeneza propaganda hizo ndio zenyewe ziko mstari wa mbele kufanya biashara na China, hii inashangaza".

    Katika hatua nyingine, Waziri Wang alisema China itaendelea kuyaunga mkono makampuni ya ndani ambayo yanakumbwa na misukosuko mbalimbali, akitolea mfano kampuni ya simu ya Huawei ambayo imeshitakiwa na Marekani.

    "Kwa vyovyote vile lazima tuwe upande wa kampuni yetu ya Huawei, tunajua ni kampuni nzuri ambayo inafanya kazi kubwa katika kukuza teknolojia," alisema na kuongeza kwamba wanaamini kesi hiyo itaisha salama.

    Huawei ambayo ni moja ya kampuni kubwa za mawasiliano na usambazaji wa simu duniani, hivi karibuni ilifunguliwa mashitaka na serikali ya Marekani kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha, kuzuia utekelezaji wa haki na wizi wa teknolojia.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako