• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Afrika ikitumia vizuri Mikopo ya China, Hofu Mtego wa Madeni Utakosa Nguvu

    (GMT+08:00) 2019-03-12 09:07:41

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    AFRIKA kwa miaka mingi imekuwa nyuma kimaendeleo. Umaskini wa bara hili lipo Katika sura kuu mbili--mioundombinu mibovu na huduma za kijamii zilizo chini ya viwango vya kimataifa.

    Barabara za kisasa, bandari, reli na viwanja vya ndege ni baadhi tu ya miundombinu muhimu inayotakiwa kuwepo ili shughuli nyingi za kiuchumi na maendeleo ziweze kufanyika kwa ufasaha.

    Kwa miaka ya hivi karibuni nchi za Afrika zimeanza kuamka. Zimeamka baada ya kugundua kuwa hakuna maendeleo yoyote yataweza kufikiwa iwapo uwekezaji mkubwa hautafanyika katika kujenga na kuboresha miundombinu.

    Kwa ujumla, ili kujenga miundombinu bora ya kisasa, teknolojia, nguvukazi na fedha nyingi zinahitajika kwa sababu vitu hivi kwa pamoja ni gharama sana.

    Ikiwa na shauku ya kuweka haya mambo sawa, nchi za bara hili zimekuwa zikipokea mikopo kutoka kwa nchi wahisani, mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha za kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia na mabenki mbalimbali ya biashara.

    China ni moja ya nchi ambayo kwa sasa mataifa mengi ya Afrika yanakimbilia kupata mikopo kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yake mbalimbali ya maendeleo—ikiwemo ujenzi wa miundombinu.

    Pamoja na kuwa China siyo nchi pekee inayotoa mikopo kwa nchi za bara la Afrika, lakini kumekuwa na mitazamo mbalimbali, mingi ikionya na kutadharisha kuwa mpango wa nchi hiyo ya Asia Mashariki kutoa mikopo kwa Afrika utakuwa na athari kubwa kwa chumi za nchi hizo za Afrika.

    Hii hutokana na utegemezi wa mikopo ya China katika kutekeleza miradi mingi ya maendeleo katika nchi za bara hilo.

    Kwa mujibu wa Taasisi ya China Africa Research Institute iliyo chini ya Chuo Kikuu cha John Hopkins cha nchini Marekani, mikopo ya China kuelekea Afrika imekua ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

    Kwa ujumla, China imekopesha nchi za Afrika Dola za Kimarekani Bilioni 136 kutoka mwaka 2000 mpaka 2017. Angola ndiyo nchi inayoongoza kwa kukopa kutoka China amabapo katika miaka 17 iliyopita imepokea jumla ya Dola Bilioni 42.

    Kwanini China kwa sasa imekuwa kimbilio la nchi nyingi za Afrika? Kwa ujumla, ukiacha sababu za kihistoria na urafiki wa muda mrefu, China haina masharti makubwa katika utoaji wake wa mikopo kwa Afrika kama ilivyo kwa nchi zingine ambazo mikopo kama hiyohiyo huja na masharti magumu.

    Hii ni moja ya sababu kubwa kwanini sasa nchi za Afrika hukimbilia mikopo kutoka China, lakini pia, pamoja na kutokwepo na masharti, mikopo hiyo huwa ni nafuu na wakopaji wanapewa muda mrefu wa kuanza kuirejesha.

    Hapa labda suala kubwa liwe kwa wakopaji --Afrika, je mikopo hiyo inatumika katika malengo yaliyokusudiwa na hayo malengo yaliyokusudiwa yana uwezo wa kuzalisha na kurudisha fedha iliyowekezwa?

    Hayo ni mambo ya msingi ambayo kabla ya Afrika kufanya maamuzi ya kukopa kutoka nchi yoyote lazima lijiulize. Kwa miradi ambayo ni dhahiri kuwa itazalisha na kurudisha mtaji siyo shida hata mabilioni ya dola za kimarekani yakikopwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

    Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kimarekani ya Center for Global Development (CGD) na kuandikwa na Bw. Gyude Moore unaonyesha kuwa China sio nchi kiongozi kwenye mikopo kwa Afrika na wala siyo nchi inayosababisha matatizo makubwa ya madeni kwa nchi za Afrika.

    Bw. Moore anasema kuwa hii dhana ya China kuelemea Afrika inazungumzwa zaidi kwenye nchi za magharibi na Marekani kwa sababu msingi wake ni 'wasiwasi' kuhusu China kuwa Taifa lenye nguvu duniani.

    Yote kwa yote, Afrika lazima ipige hatua ya kimaendeleo. Lazima ikope China ama kutoka nchi nyingine yoyote ambayo iko tayari kutoa mikopo hiyo kwa masharti nafuu na kwa riba ndogo. Kuacha kukopa inamaanisha bara hili liendelee kuwa maskini.

    Hivi karibuni, kufatia kuenea kwa hizi tuhuma za kuwa China inataka kuzidhoofisha nchi za Afrika kupitia madeni na misaada mbalimbali, Waziri wa Mambo ya Nje Bw.Wang Yi, alisema China imekua na ushirikiano mzuri na Afrika hasa katika ujenzi wa miradi mingi ya maendeleo kama vile miundombinu, huduma za kijamii, biashara na masuala ya kidiplomasia, na kwamba wanatarajia mahusiano hayo yaendelee kwa manufaa ya pande zote.

    Alisisitiza kuwa nchi hiyo haina lengo la kuzitawala nchi za Afrika kupitia misaada ambayo imekua ikiitoa, bali kuzisaidia nchi zinazoendelea katika kuinua pato la taifa pamoja na kuondokana na umaskini.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako