• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Shirikia la Ndege Tanzania, China wasaini mkataba wa watalii zaidi ya 10,000

    (GMT+08:00) 2019-03-14 09:23:13

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    TANZANIA kupitia Shirika lake la Ndege, (ATCL), imesaini mkataba wa makubaliano ya kuanza maongezi ya kibiashara ya kusafirisha watalii zaidi ya 10,000 kutoka nchini China.

    Watalii hao kutoka nchi hiyo ya Asia Mashariki wanatarajiwa kuingia nchini Tanzania mwaka huu wa 2019 na Kampuni ya Touchroad International Holdings Group ya China (TIHG)

    Awali, TIHG ilisaini mkataba na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ya kuleta watalii hao 10,000.

    Utiaji saini wa mkataba huo na ATCL ni mwendelezo wa kuanza kwa utekelezaji wake ambapo kampuni hiyo itapeleka Tanzania watalii kutoka China kisha watalii hao watatumia ndege za Shirika la ATCL kuelekea maeneo mbalimbali kutazama vivutio tofautofauti vya utalii.

    Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumanne Machi 12, 2019, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Jaji Thomas Mihayo alisema katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa na mchango mkubwa katika uchumi, Bodi hiyo imeanza kutekeleza makubaliano ya kuleta watalii 10,000 kutoka China.

    "Hivyo leo tutakuwa na tukio la kusaini mkataba wa kuingia makubaliano ya maongezi ya kibishara kati ya ATCL na kampuni hii ya China ya namna watakavyofanya biashara ya kusafirisha watalii kuwatoa China na kuwaleta hapa nchini, "amesema.

    "Tunatarajia kuanza kupokea watalii 300 kuanzia mwezi Mei mwaka huu, kundi hili la watalii litakuwa la watu maarufu nchini China wakiwamo waandishi wa habari wakubwa, wafanyabiashara wakubwa na wasanii mbalimbali, na tunatarajia kupata watalii 260 kila wiki mpaka hapo watakapokamilika watalii 10,000," amesema.

    Meneja Mauzo na usambazaji wa ATCL, Edward Mkwabi alisema shirika hilo limejipanga kufanya kazi hiyo ya kubeba watalii na kwamba makubaliano yaliyofanyika ni ya kuingia kwenye mawasiliano ya namna gani biashara itafanyika.

    Naye, Mwenyekiti wa Kampuni ya TIHG, He Liehu amesema kampuni hiyo pia imejipanga vyema kufanya biashara ya kuleta watalii nchini kupitia ndege zake.

    Kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka China kutembelea Tanzania ni matokeo ya jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na TTB.

    Mwaka jana Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa Tanzania, Dkt. Aloyce Nzuki, alifungua mkutano wa wadau wa watalii nchini China, ambapo zaidi ya washiriki 200 walijitokeza zikiwemo kampuni za utalii, mawakala wa usafirishaji, mashirika ya ndege na vyombo vya habari.

    Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii, Devotha Mdachi alitoa mada maalum kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.

    Aidha, kampuni za utalii kutoka Tanzania nazo pia zilipata fursa ya kuelezea huduma zao kwa ujumla (packages)wanazotoa katika utalii mahsusi kwa soko la China.

    PICHA:

    Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania Jaji Thomas Mihayo (aliyesimama kulia) pamoja na Makamu Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Touchroad International Holdings Group, Fu Wei wakishuhudia utiaji saini kati ya Mwenyekiti wa Touchroad Group, He Liehui na Meneja Mauzo na Usambazji wa Shirika la Ndege Tanzania, Edward Nkwabi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako