• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Afisa wa ngazi ya juu wa UM asifu miradi ya China Afrika huku akiomba Beijing kusaidia kuangamiza jinamizi la ufisadi barani

  (GMT+08:00) 2019-03-28 09:09:47

  Na Eric Biegon – NAIROBI

  Katibu Mkuu wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na maendeleo, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi ametoa wito kwa serikali ya China kusaidia Afrika kushinda vita dhidi ya rushwa iwapo bara hilo linataka kufanikisha ajenda yake ya maendeleo.

  Afisa huyo wa ngazi ya juu katika UM alisikitikia kile alichokitaja kuwa ongezeko la idadi ya maafisa wa serikali kutoka nchi mbalimbali za Afrika ambao wanatumia vibaya nafasi zao kwa kudai hongo kutoka kwa mfanyabiashara yeyote wa Kichina anayenuia kuwekeza katika bara la Afrika.

  Kwa mujibu wa Kituyi, desturi hii ya kuitisha rushwa imekuwa kizingiti cha maendeleo katika Afrika. Anasema China inaweza kusaidia vita dhidi ya wahusika wakuu katika juhudi za kuangamiza uovu huo.

  Kituyi anadumisha kuwa wote wanaoendesha shughuli hiyo haramu lazima wadhibitiwe ili ushirikiano unaoendelea kati ya China na Afrika ushamiri vizuri kwa manufaa ya watu. Iwapo hawatadhibitiwa, Kituyi anaonya kuwa kundi hilo litaendelea kupaka tope sifa za China barani Afrika.

  "Katika mkutano wa Ukanda Mmoja Njia Moja jijini Beijing mwaka uliopita, nilizungumzia suala hili na maafisa kutoka serikali ya China. Niliwaambia kwa sababu China inatekeleza vita dhidi ya ufisadi nyumbani kwa ufasaha, kama mshirika wa maendeleo ni muhimu zaidi kwa China kusaidia kufichua maafisa kutoka mataifa ya Afrika wanaoendeleza ufisadi katika miradi zinazoendeshwa na serikali ya China." Alisema

  Yeye alielezea Imani yake kwamba hii inawezekana kutokana na rekodi nzuri ya utawala wa Rais Xi Jinping ambayo hadi sasa imefanikiwa kukandamiza ufisadi kwa kuwaadhibu vikali wanaolishiriki.

  "China inawaadhibu wakosaji kule kwao, wanapaswa pia kutusaidia kuwaadhibu wetu wenyewe. Watu hawa wanaipa serikali ya China jina mbaya." Kituyi alohoji

  Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Kenya, Kituyi ambaye alihudumu kama Waziri wa biashara na viwanda katika utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki, alisema serikali ya China inatekeleza shughuli muhimu barani ambayo hatimaye itazaa maendeleo mahsusi Afrika.

  "Uwekezaji wa China unaweza kuwa chemichemi ya msingi wa mabadiliko chanya nchini Kenya na Afrika nzima. China imechangia zaidi ya asilimia 10 ya upanuzi wa pato la Taifa nchini Ethiopia katika muda wa miaka 10 iliyopita." Alisema Kituyi

  Kituyi alizimiminia sifa kochokocho makampuni ya Kichina ambayo alisema yametoa ushindani mkubwa na kusaini mikataba barani Ulaya, Amerika na Asia kwa ujumla, na hivyo ni lazima kuzikumbatia katika enzi hii ya maendeleo.

  "Kwanza kabisa, China kwa sasa imeweka pamoja rasilimali nyingi mno za kuwekeza nje ya mipaka yake kote ulimwenguni. Leo mtiririko mkubwa wa FDI mahali popote ulimwenguni inatoka China." Kituyi alikiri

  Alipuuzilia mbali madai kuwa China imevamia Afrika kwa maslahi yake binafsi. Kwa mujibu wa Kituyi, dunia ya leo inaelekeza macho yake Mashariki. Alisema Kenya na Afrika zitafanya vyema kukubaliana na hali hii.

  "Kenya bado inahitaji miundombinu, Kenya inahitaji reli za kisasa (SGR) zingine, kufungua rasilimali ya nchi hii, Kenya inahitaji huduma ya reli ya usafiri wa kasi jijini Nairobi na miji mingine. Haya yote yatatekelezwa na China." Alisema

  Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kwamba serikali za Afrika lazima zijitwike jukumu kubwa la kuwang'oa maafisa walaghai ambao wanatafuta fursa ya kudai rushwa kwenye miradi nzuri ambayo yanayofadhiliwa na China kwa manufaa ya jamii.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako