• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Juhudi za Kenya za kuuza parachichi kwenye soko la China zashika kasi huku wakaguzi kutoka Beijing wakitua Nairobi

    (GMT+08:00) 2019-04-03 08:37:21

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    WAKAGUZI kutoka China hatimaye wametia nanga jijini Nairobi kwa ajili ya ukaguzi wa ubora wa mazao ya kilimo, na kuweka Kenya katika nafasi nzuri ya kuwa mojawapo wa nchi ambazo zinasafirisha mazao yao ya kilimo nchini China.

    Wakaguzi hao wawili wa parachichi kutoka China, wakiongozwa na mshauri wa kiuchumi na kibiashara katika ubalozi wa China nchini Kenya Guo Ce, walielekea moja kwa moja hadi kwenye ubalozi wa China ambako walipokelewa na balozi Wu Peng.

    "Mapema asubuhi, wakaguzi wawili walitembelea afisi ya Katibu wa kudumu katika wizara ya biashara bwana Chris Kiptoo wakiwa wameandamana na bwana Guo Ce, pamoja na Mkurugenzi mkuu wa Kephis Esther Kimani na wadau wengine." Ilisema taarifa kutoka Ubalozi wa China

    Hii ni hatua mojawapo ya kutimiza makubaliano yaliyotiwa saini mwaka jana jijini Beijing ambayo yatawawezesha wakulima wa Kenya kuuza mazao yao kwenye soko la China.

    Makubaliano hayo yanaorodhesha masharti kuhusu viwango ambavyo Kenya lazima itimize kabla ya kuanza kusafirisha mazao yake China.

    "Pande zote mbili zimeahidi kutoa msaada kwa wakaguzi watakapoendelea na shughuli zao nchini Kenya na kusisitiza umuhimu wa kufungua soko la China kwa kuwawezesha wakulima wa Kenya kusafirisha parachichi nchini humo." Taarifa hiyo ilibainisha.

    Ama kwa Kweli, taarifa kutoka kwa afisi ya mkuu wa mawasiliano na vyombo vya habari katika ubalozi wa China Zhang Gang ilibainisha kwamba wataalamu hao wawili wamo nchini kufanya uchambuzi wa uwezekano wa itilafu yoyote huku wakitembelea mashamba ya mimea hiyo kwani huu ni msimu wa kuvuna parachichi.

    "Wakaguzi kutoka China waliofika hapa wana jukumu la kufanya uchambuzi wa mazao ya parachichi na kuhakikisha kwamba taratibu zinazohitajika kwa ajili ya usafirishaji wa mazao ya kilimo kuelekea China zimetimizwa." Taarifa hiyo iliongeza.

    Hatua hii pia inaonekana kama njia moja ya kuinua uwiano wa kibiashara kati ya Kenya na China. Kauli hii pia ilifichuliwa siku za karibuni na mshauri wa uchumi kwenye ubalozi wa China Guo Ce.

    "Ili kushughulikia malalamishi ya Kenya kuhusu usawa wa kibiashara kati ya pande zote mbili, tutakuwa tukitumia fursa zaidi kupigia upatu usafirishaji wa bidhaa kutoka Kenya," Guo alisema.

    Wataalamu hao kutoka China pia wameratibiwa kutembelea mashamba ya parachichi katika Kaunti za Murang'a, Kiambu, Embu, Uasin Gichu na Trans Nzoia.

    Lakini shughuli yao nchini Kenya haitakuwa imekamilika kwani wawili hao wanatarajiwa kuzuru kituo cha ukaguzi wa mazao hayo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kuangalia operesheni.

    Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo ya Kenya, ambayo inaongoza harakati hizi, ufunguzi wa soko ya China kwa mazao kutoka Kenya itaashiria mwamko mpya kwenye mahusiano yanayonawiri kati ya nchi hizo mbili.

    "Kama soko hili litafunguliwa, itakuwa ya kufana kwani China ina watu wengi. Wakulima wetu watakuza mimea zaidi na matokeo yake ni mapato zaidi,"alisema waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri.

    Mbali na parachichi, Kenya inanuia kuuza maembe yake na korosho katika soko kuu la China.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako