• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yawa nchi ya kwanza kufungua ofisi za ubalozi Dodoma

    (GMT+08:00) 2019-04-16 14:11:22

    Na Majaliwa Christopher

    JAMHURI ya Watu wa China imekuwa nchi ya kwanza duniani kufungua ofisi za ubalozi katika jiji la Dodoma, miezi michache baada ya serikali ya Tanzania kuhamisha shughuli zake kutoka jijini Dar es Salaam.

    Hii imekuwa ni hatua nzuri kwa nchi hiyo ya Asia ya Mashariki katika kuunga mkono juhudi ya serikali ya Tanzania--kuhamisha makao yake kwenda jijini Dodoma.

    Vilevile serikali ya China kupitia kwa ubalozi wa wake nchini Tanzania imeendelea Kuipongeza nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki kwa juhudi zake katika kupambana na rushwa na kuboresha maisha ya wananchi.

    Hatua ya China kufungua ofisi za ubalozi jijini Dodoma inakuja siku chache baada ya nchi hizo mbili kufikia hatua za mwisho za kuanza safari za ndege moja kwa moja toka jijini Dar es Salaama kwenda Mjini Guangzhou kwa lengo la kuinua biashara na utalii katika nchi hizo mbili.

    Akizungumza jijini Dodoma baad, Balozi wa China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke alisema nchi yake imeamua kufungua ubalozi mdogo ikiwa ni kuitikia mwito wa serikali ya Tanzania kuhamia Dodoma.

    "Mwaka jana wakati wa hafla ya mabalozi, Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alikabidhi hati za viwanja, ikiwa ni njia ya kuzialika nchi zetu kuhamia Dodoma, China tumeona umuhimu wa hilo, hivyo tumeamua kufungua ubalozi mdogo hapa Dodoma ambao pamoja na mambo mengine utatumika kuratibu shughuli mbalimbali za Mahusiano na ushirikiano kati yetu na Tanzania," alisema Bi. Wang.

    Aidha, Wang aliipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa kupambana na rushwa na kuboresha maisha ya wananchi wake

    Aidha, Ke ameishauri serikali ya Tanzania kutumia fursa ya kijiografia ya mji wa Dodoma katika kuimarisha uhusiano uliopo na kupiga hatua kwenye maendeleo ya kijamii na uchumi.

    Balozi Wang alisema China imeialika Tanzania kushiriki katika majukwaa ya kibiashara, ikiwamo maonesho ya kimataifa ya mazao ya bustani yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili.

    Jukwaa la biashara la China-Afrika litafanyika Juni mwaka huu katika mji wa Changsha na maonesho makubwa ya China International Import Expo yatakayofanyika Novemba mwaka huu jijini Shanghai.

    China ni nchi yenye uwekezaji mkubwa Tanzania ikiwa na miradi ya uwekezaji 723 yenye thamani ya dola bilioni 5.9, ikizalisha ajira takribani 87,126.

    Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Tanzania na China zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na kuwa uanzishwaji wa safari ya ndege hautasaidia Tanzania pekee katika kuimarisha utalii na biashara lakini pia bara la Afrika.

    Pia Profesa Kabundi aliipongeza China kwa hatua yake ya kufungua ubalozi wake jijini Dodoma na alisema serikali ipo tayari kutoa msaada.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako