• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Tanzania ina fursa ya kuuza mazao zaidi ya 11 China, Utafiti wabaini

    (GMT+08:00) 2019-04-19 13:51:38

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    TANZANIA inayo fursa ya kufanya biashara ya mazao zaidi ya 11 na nchi ya China, Utafiti umebaini.

    Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) kwa kushirikiana na China Centre for Agriculture Policies (CCAP) umebainisha kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki inazalisha mazao mengi ambayo yana soko kubwa nchini China.

    Utafiti huo wa mazao ya kilimo cha biashara ambao pia ulifanyika nchini Ethiopia umebaini kuwa bado wakulima wa nchi hizo mbili za Afrika wanahitaji elimu ya kutosha ili kuweza kunufanika na soko la mazao hayo huko nchi ya Asia ya Mashariki.

    Hayo yalibainishwa katika kikao cha wadau wa kilimo kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania katika warsha ya uwasilishaji wa utafiti wa awali juu ya namna ya kuwashirikisha wakulima wadogo katika biashara ya mazao China.

    Kiongozi wa utafiti huo, Dkt. Hoseana Lunogelo alisema kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu kwa wakulima kuongeza tija kibiahara lakini pia kufahamu soko la China na aina ya uhitaji wa mazao hayo ya kibiashara.

    Dkt Lunogelo aliongeza kuwa kwa sasa mazao mengi yanayozalishwa nchini Tanzania yakiwemo muhogo, mahindi, mwani, korosho, choroko na alizeti soko lake limekuwa mara saba China ikilinganishwa na namna soko hilo lilivyo nchini Tanzania, hatua inayohitaji muamko kutoka kwa wakulima.

    Mwaka 2017, Tanzania na China walitiana saini mkataba wa kuuza bidhaa za muhogo katika nchi hiyo ya Asia ya Mashariki.

    Mkataba huo ulisainiwa jijini Beijing kati ya Balozi wa Tanzania nchini humo Bw. Mbelwa Kairuki kwa niaba ya serikali ya Tanzania na Naibu Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya udhibiti na ukaguzi wa mazao wa China Bw. Li Yuanping kwa niaba ya serikali yake.

    Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya ESRF Dkt. Tausi Kida alisema utafiti huo ni muhimu kwa wakulima nchini Tanzania kwa kuwa utwawasaidia kubaini hatua za kukuza kilimo kutimiza malengo ya nchi ya kuelekea uchumi wa kati wa viwanda.

    Akizungumzia mfano faida ambazo wakulima hao Wanaweza kunufaika nazo, Dkt. Kida alisema mwaka 2017 pekee kwa mujibu wa takwimu zilizopo, China ilitumia Dola za Kimarekani Bilioni 27 kununua mazao mbalimbali kutoka nchi za Afrika, kiasi ambacho ni kikubwa na kinaonesha wazi mahitaji ya mazao kwa taifa hilo ambalo ni la pili kwa kuwa na uchumi mkubwa na imara duniani.

    Akiwasilisha mada ya utafiti wa soko la mazao kutoka China, Mtafiti kutoka Chuo cha CCAP Prof. Jikun Huang alisema kuna faida nyingi kwa wakulima wa bara la Afrika kutumia fursa za biashara nchini China kutokana na kuwepo kwa soko kubwa na imara.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako