• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Wakenya katika makampuni ya Kichina wasifu ushirikiano kati ya Kenya na China

  (GMT+08:00) 2019-04-19 13:54:06

  Na Eric Biegon – Beijing

  Baadhi ya wafanyakazi bora wa Kenya katika makampuni ya Kichina yanayoendesha shughuli zao nchini humo walitunukiwa nafasi ya kihistoria ya kuzuru China baada ya makampuni hizo kugharamia ziara hiyo kwa asilimia mia moja.

  Safari hiyo iliyoandaliwa na chama na kibiashara na uchumi kati ya China na Kenya KCETA au (Kenya China Economic and Trade Association) kwa kushirikiana na ubalozi wa China nchini Kenya, ilitoa jumla ya nafasi 55 kwa wafanyakazi 55 waliofanya vyema zaidi katika vituo vyao vya kazi kutembelea miji mikuu ya Shanghai na Beijing.

  Idadi ya 55 inawakilisha miaka 55 tangu Kenya na China kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia.

  Wale ambao walifanikiwa kuwa sehemu ya ziara hiyo hawakuficha furaha yao. Ama kwa kweli ilikuwa ni mara ya kwanza kusafiri nje ya nchi kwa asilimia kubwa ya kundi hilo. Katika furaha yao, waliuhusisha ziara hiyo ya kihistoria na ushirikiano unaoendelea kunawiri kati ya Kenya na China ambayo wao wanasema ina manufaa makubwa kwa pande zote mbili.

  Mmoja wa wale waliobahatika, Anthony Omweri anayehudumu katika kampuni ya Yoshin anasema makampuni ya Kichina ni waajiri wakubwa zaidi nchini Kenya kwa sasa. Wakati ambapo mahusiano kati ya Beijing na Nairobi yanaendelea kustawi, Omweri anasema makampuni haya yanajenga uwezo wa kiuchumi ya Wakenya na kusaidia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira.

  Kwa maoni yake, Omweri, ambaye ni meneja wa rasilimali ya binadamu katika kampuni hiyo, anasema China imekuwa ikiwekeza sana nchini Kenya ikilinganishwa na washirika wengine wa maendeleo. Anasema matokeo yake nchini yamekuwa chanya.

  "Naelewa maana ya kuwa na kazi. Idadi kubwa ya watu wanachukulia uwepo wa Wachina nchini Kenya vibaya. Wasilolijua ni kwamba Wachina ndio wanaotengeneza nafasi za ajira katika nchi yetu. Hii ni kweli." Omweri anasema.

  Hisia zake zilipokea uungwaji mkono kutoka kwa Wycliffe Kiharangwa ambaye ni mfanyikazi katika kampuni ya KEDA (Kenya) Ceramics Limited.

  "Nadhani safari hii inaonyesha kwamba ushirikiano katika ya Kenya na China ni muhimu sana katika nyanja mbalimbali. Mimi nina Imani kuwa Wachina watatusaidia kuafikia maendeleo yanayoonekana kama walivyofanya katika nchi yao kwa kipindi kifupi cha wakati." Kiharangwa alisema.

  Kwa mujibu wa Delila Wendy ambaye amekuwa akifanya kazi kwa kampuni ya China ya kujenga mabarabara, reli na madaraja maarufu CRBC tangu 1996, utumizi wa mamia ya maelfu ya pesa ili kufanikisha ziara hiyo inaonyesha umuhimu ambao mwajiri anashikilia kwa wafanyakazi wenyeji.

  "Wakati kitu kama hiki kinatokea, kinaonyesha kuna uhusiano mzuri kati ya mwajiri na mfanyakazi. Uhusiano kati ya pande zote mbili ni ya umuhimu mkubwa. Hii pia inaonyesha kuwa mwajiri wetu kutoka China anatuthamini sana na ndiyo sababu ya kutuleta mpaka hapa." Alisema

  Wendy ambaye ni meneja wa rasilimali katika kampuni ya CRBC pia ana mtazamo kwamba "ziara ya miradi mbalimbali ya ujenzi yanayotekelezwa na kampuni yetu mzazi katika miji mikubwa ya China imekuwa ya kutufungua macho. Viwango vya ujenzi viko katika ngazi ya juu. Hii bila shaka itatuzaidia kutia bidi zaidi katika kazi yetu."

  Kabla ya kundi la kwanza kuondoka kuelekea Beijing, mshauri wa uchumi na biashara katika ubalozi wa China nchini Kenya Guo Ce alisema ushirikiano kati ya Nairobi na Beijing umekuwa ukinawiri hasa katika jitihada zinazolenga kuboresha uchumi kwa manufaa ya watu.

  "Ushirikiano wa China na Kenya huleta faida ya pamoja inayoonekana kwa watu wa nchi zote mbili, na kusaidia kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii wa Kenya," alisema bwana Guo

  Lakini hii haikuwa tu fursa ya kuzuru China, hila ilikuwa nafasi ya baadhi ya waajiriwa wenyeji kushuhudia utamaduni wa watu wanaofanyakazi nao kwa sasa.

  "Naamini baada ya safari hii, mtakuwa na ufahamu mpana zaidi wa utamaduni wa China na Kichina, ambayo itasaidia zaidi katika kazi zenu za kila siku katika makampuni ya Kichina." Mshauri huyo wa kiuchumi alibainisha.

  Kwa kweli, Daniel Kitheka anayefanya kazi katika kampuni ya kimataifa ya Avic anasema ziara hiyo imekuwa tukio la umuhimu mkubwa sana maishani mwake. Anakiri kwamba sasa anaelewa ni kwa nini wenzake kutoka China wanatabia ya kujitolea mno kazini.

  "Kuwa sehemu ya ziara hii imenionyesha kwamba bidii inalipa. Imenipa motisha si haba. Sasa nataka kufanya vizuri na kwa kujitolea zaidi kwa mwajiri wangu. Tangu niajiriwe Avic, nimeona jinsi wanavyonithamini. Hakujakuwa na ubaguzi wa haina yoyote wakati wote." Kitheka alisema

  Kusonga mbele, Guo alisema viongozi kutoka pande zote mbili lazima waonyeshe dhamira, kufanya kazi kwa bidii na kujitolea ili ushirikiano unaoendelea kwa sasa uweze kuzaa matunda zaidi kwa watu.

  Wakiwa kwenye ziara ya siku 8, wafanyakazi hao bora waliweza kutembelea maeneo ya urithi duniani kama vile The Bund, Chinese Art Palace, na mnara wa Oriental Pearl zilizoko Shanghai. Katika Beijing, kundi hilo lilizuru maeneo kama vile, Tiananmen Square, Palace Museum maarufu kama Forbidden City, the Temple of Heaven, na makaburui ya Ming miongoni mwa mengine.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako