• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Makampuni ya Kichina nchini Kenya yaahidi kuyapa kipaumbele ustawi wa wafanyakazi wao

  (GMT+08:00) 2019-05-02 10:22:32

  Na Eric Biegon – Beijing

  Makampuni ya Kichina yanayoendesha shughuli yao nchini Kenya yameahidi kuzingatia zaidi ustawi wa wafanyakazi wao wa ndani. Yakiongozwa na kampuni ya China Road and Bridges Corporation (CRBC), makampuni hayo yalisisitiza haja ya kusaidia kupunguza mzigo kwa wafanyakazi wao hasa wale wanaopeleka watoto wao shuleni.

  Ni kutokana na hali hii ambapo makampuni hayo yatatilia mkazo hali ya watoto wa wale wanaowafanyia kazi yanapotoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Jamii maskini.

  Naibu mkuu wa kiuchumi katika kampuni ya CRBC Xie Tienzhu alifichua haya wiki iliyopita wakati kundi la wafanyakazi bora wa Kenya katika makampuni ya Kichina nchini humo walipozuru makao makuu ya kampuni hiyo jijini Beijing.

  "Tunataka kuipa kipaumbele ustawi wa wafanyakazi wetu hasa katika kuwaelimisha watoto wao." Xie alisema

  Akiwahutubia wafanyakazi kutoka makampuni mbalimbali ya Kichina nchini Kenya, Bwana Xie alibainisha kwamba suala la uwajibikaji kwa jamii ni la umuhimu mkubwa kwa makampuni yao ya kimataifa hasa wakati ambapo yanajitahidi kuboresha maisha katika mataifa wanamohudumu.

  Alisema CRBC, kwa mfano, tayari imeanzisha hazina ya kushughulikia mahitaji ya wafanyakazi wake ambao wanakabiliwa na changamoto za kulipa ada kwa ajili ya watoto wao shuleni.

  Ni hapa ambapo Cosmas Beliti Duwe, ambaye ni mwajiriwa wa zaidi ya miaka 20 katika CRBC na ile ya kampuni ya mawasiliano ya China Communications and Construction Company (CCCC) alifungua moyo wake, na kufichua kwamba kulipa ada ya shule kwa mwanaye katika Chuo Kikuu haijakuwa rahisi. Alitaka kujua iwapo mwanaye wa kiume angeweza kunufaika kwa ufadhili wa masomo zinazotolewa na makampuni ya Kichina.

  "Mwanangu anasomea shahada ya takwimu katika chuo kikuu kimoja nchini Kenya. Yeye hakufaulu kupata mkopo wa serikali kumwezesha kuendelea na masomo yake na hii imekuwa mzigo kwangu kwa sababu ya majukumu mengine mengi mikononi mwangu." Alisema

  Akijihisi mwenye furaha baada ya kukutana na viongozi wa kampuni yake jijini Beijing, Duwe alisema "wakati niligundua kampuni yangu inashughulikia masuala ya masomo kwa watoto masikini nchini, niliamua kufuatilia jambo hilo na usimamizi. Niliuliza kama mwanangu ambaye yuko chuo kikuu angeweza kufaidika kwa programu hiyo."

  Maombi yake yalionekana kujibiwa kwani Bwana Xie alimuhakikishia kuwa kampuni yake itashughulikia swala hilo kwani "wewe ni mmoja wetu."

  "Kama mtu ambaye amefanya kazi pamoja nasi kwa muda mrefu, tunaamini kusaidia mtoto wako kupata masomo haiwezi kuwa tatizo." Alisema

  Xie alisema atashirikisha wenzake jijini Nairobi ili suala hilo lipewe kipaumbele na kushughulikiwa upesi. Alisema kampuni yake, itaharakisha mchakato wa kusaidia mwana wa Duwe na wengine walio katika hali hiyo kumaliza masomo ya chuo kikuu.

  "Tunataka kusonga mbele na jambo hili kwa haraka na kukupa majibu chanya kuhusiana na hilo haraka iwezekanavyo." Alisema

  Duwe hakuweza kuficha furaha yake kutokana na ahadi hii ya afisa wa kampuni. Kwake, ndoto yake kubwa ni kuona mwanaye akimaliza masomo yake na baadaye kupata kazi nzuri.

  "Nitashukuru sana iwapo kampuni itanisaidia katika suala hili. Kama mwanangu atakamilisha masomo yake, yeye huenda hata akapata kazi na moja ya makampuni ya Kichina ambayo itageuka kuwa maisha bora kwetu siku za baadaye." Alisema

  Wakati huo huo, Mchumi huyo wa CRBC alifichua kuwa makampuni yote ya Kichina yanayohudumu nje ya nchi yamepewa maagizo kuharakisha kipindi cha mpito hadi viwango vya juu vya usimamizi kwa wafanyakazi wenyeji wanaofanya kazi katika makampuni hayo.

  Alisema hii ni njia mojawapo ya kuwahamasisha wafanyakazi wao hata wanapojaribu kuboresha hali ya kazi ya wafanyakazi katika nchi hizo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako