• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Tanzania yashauri China kuwekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo

  (GMT+08:00) 2019-05-15 08:34:42

  Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

  SERIKALI ya Tanzania imeshauri wawekezaji kutoka nchini China kuanza kuwekeza katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kwa kuwa nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki ina utajiri mkubwa wa malighafi kwa ajili ya viwanda hivyo.

  Akizungumza na wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini China jana jijini Arusha Tanzania, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Bi. Angela Kairuki alisema idadi ya watu nchini humo watakaokuwa wanaishi mijini itapanda hadi asilimia 50 kufikia mwaka 2050, hali inayosababisha kuwepo na uhitaji mkubwa kwenye uwekezaji katika sekta hiyo.

  Waziri Kairuki aliwaambia wafanyabiashara hao kuwa kutokana na makadirio hayo ya kuongezeka kwa idadi ya watu mijini, mahitaji ya chakula pia yatapanda kiasi kwamba uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo yatakuwa na tija kubwa.

  Bi. Kairuki aliongeza kuwa Tanzania imebarikiwa utajiri mkubwa wa ardhi yenye rutuba na vyanzo vya maji vya kutosha ambayo ni muhimu kwa mazao mbalimbali yanavyotumiwa na nchi nyingi za Afrika na kote duniani.

  "Hamtalazimika kuleta malighafi nchini kwa ajili ya viwanda hivyo kwa sababu sisi kama nchi tuna uwezo wa kuzalisha vya kutosha kwa ajili ya kulisha viwanda hivyo," alisema Waziri Kairuki, na kuongeza kuwa kuna fursa mbalimbali pia katika sekta ya kuchakata samaki ambao wana soko kubwa katika nchi za Asia.

  "Uwekezaji wenu ulenge katika kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo. Soko liko tayari. Bidhaa zenu pia zinaweza kuuzwa ndani ya Jumuia ya Afrika Masharikia (EAC) na Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambayo kwa ujumla ina idadi ya watu wapatao milioni 800.

  Waziri Kairuki alieleza kuwa biashara kati ya Tanzania na China imeongezeka kutoka Dola Bilioni 3.9 miaka kadhaa iliyopita hadi kufikia Dola Bilioni saba mwaka jana, 2018.

  "Hii inaonyesha jinsi nchi hizi mbili zilivyo na ushirikiano mzuri wa kibiashara na uwekezaji. Kuwekeza katika sekta ya kuchakata mazao ya kilimo kutazidi kuimarisha ushirikiano wetu," alisema Bi. Kairuki.

  Waziri huyo pia aliongeza kuwa Tanzania ina mazingira rafiki na bora kwa uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo madini, ufugaji, ujenzi, hoteli na kadhalika.

  Wawekezaji hao wa China waliongozwa na mwenyekiti wa Touchroad International Holding Group, Bw. Zhejiang Liehui.

  Mkutano huo ulihudhuriwa na wawekezaji zaidi ya 60 kutoka China na 90 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako