• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Bunge Tanzania lataka mazungumzo na kampuni ya China kuhusu mradi wa Bagamoyo ukamilishwe

  (GMT+08:00) 2019-05-15 09:11:22

  Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

  WABUNGE wa Bunge la Tanzania wamaitaka serikali ya nchi hiyo kukamilisha mazungumzo na kampuni ya China inayotaka kuwekeza katika Bandari ya Bagamoyo kwa manufaa ya taifa hilo la Afrika ya Mashariki.

  Mradi huo mkubwa ulikuwa ugharimu takribani Dola za Kimarekani Bilioni 10, ambayo ni sawa na shilingi trilioni 23 za Tanzania.

  Wawakilishi hao wameonyesha kutoridhishwa na kasi ya mazungumzo hayo ambayo yamechukua takribani miaka saba sasa.

  Walisema kwamba kushindwa kukamilika kwa mazungumzo hayo kwa sababu zilizoelezwa kwamba ni kwa manufaa ya taifa, haziridhishi.

  Wakichangia katika hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyowasilishwa jijini Dodoma, wabunge hao walisema ni muda muafaka sasa serikali ikachukulia suala hilo kwa uzito unaostahili.

  Akiwasilisha hotuba ya Wizara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema mradi huo ulisimama kwa sababu ya masharti yaliyowekwa katika kufikia mkataba huo.

  Masharti hayo ni pamoja na kuachiwa jukumu la tozo katika bandari na pia suala la uanzishwaji wa viwanda katika eneo la Bagamoyo na Tanga kuachiwa kampuni hiyo ya China.

  Wakati wa majadala huo, baadhi ya wabunge walitaka chombo hicho kiunde kamati maalum ya kuishauri serikali na pia kuwa na nafasi kujadili uamuzi wa serikali inapoachana na miradi mikubwa ya kimkakati.

  Wabunge hao walisema kwamba bandari ya Dar es Salaam kwa sasa pamoja na upanuzi wote, imefikia mwisho na haiwezi tena kubeba meli mpya za kizazi cha nne na kuendelea.

  Mbunge wa Malindi, Ally Saleh alisema inafaa Bunge na wananchi kuihoji serikali pindi inapoacha miradi mikubwa yenye tija kwa taifa kama mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

  "Kwanini kama nchi tunaacha mradi kama huu..." alisema Bw. Ally na kuongeza kuwa mradi wa bandari haikuwa ujenzi wa bandari pekee, bali kutengeneza ukanda maalumu wa uchumi wa Bagamoyo ambao ungeleta ajira kwa nchi.

  Alisema bandari hiyo ambayo ingekuwa kubwa katika Afrika na ya pili kufuatia bandari ya Rotterdam, Uholanzi, ingeneemesha uchumi wa nchi kutokana na idadi za meli zilizokuwa zikitakiwa kutia nanga.

  Spika wa Bunge la Tanzania Bw. Job Ndugai alihoji kuna nini bandari ya Bagamoyo, akisema kuwa kwa jinsi walivyopewa maelezo nchini China wakati wa moja ya ziara nchini humo, mradi huo ni mkubwa mno na haiwezekani kuuachia hivi hivi tu.

  Alisema walipofanya ziara Shenzen, Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki aliwafikisha Makao Makuu ya kampuni--China Merchant Holdings International.

  "Sijui kuna nini... ukisikiliza presentation (maelezo) utaunga mkono," alisema Spika Ndugai, akisisitiza kuwa haelewi nini kimekwamisha mradi huo muhimu.

  Wabunge wengi waliochangia walisema kwamba ujenzi wa bandari hiyo na mji wake wa kiviwanda ungesaidia kurejesha kwa haraka gharama za ujenzi wa reli ya kisasa nchini humo.

  Vile vile wajenzi hao walikuwa wanajenga reli ya kisasa kuanzia Bagamoyo na kuiunganisha na reli ya Tazara.

  Mbunge wa Bagamoyo, Dkt. Shukuru Kawambwa alisema mradi huo mkubwa wa kielelezi ambao ulihusisha ujenzi wa bandari, viwanda na kuwa eneo maalumu la kiuwekezaji likiwa na viwanda vikubwa 190 baada ya mazungumzo na kutia saini hati mbalimbali kushindwa kujengwa ni hasara kwa taifa.

  Alisema wakati Tanzania inaendelea kuzungumza katika kipindi hicho hicho cha kuanzia mwaka 2012 kampuni hiyo ya China imejenga bandari za kisasa katika nchi za Djibouti, Togo, Nigeria na Sri Lanka.

  Naye Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alitaka kujua sababu za kusimamisha mradi huo ambao ungeliingiza nchini dola za Marekani bilioni 10 na kuiweka Tanzania katika ushindani.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako