• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Licha ya marufuku kutoka Marekani, itakuwa vigumu kumaliza mahusiano katika ya Huawei na Afrika

    (GMT+08:00) 2019-06-17 09:09:54

    Na Eric Biegon - NAIROBI

    Serikali ya Marekani hivi karibuni ilitangaza vikwazo dhidi ya kampuni ya Huawei na kuzuia kampuni hiyo kutumia programu mbalimbali za kampuni ya Google.

    Baada ya kutangaza marufuku hiyo, utawala wa Rais Donald Trump aidha ilitaka mataifa ya Afrika kuwa makini yanapojihusisha na kampuni ya Huawei kutokana na uhusiano wake na Chama cha Kikomunisti cha China. Pia ilitaja tuhuma kwamba Huawei ilihusika katika jitihada za ujasusi dhidi ya makao makuu ya Umoja wa Afrika kutoka kwa serikali ya China. Madai hayo hata hivyo bado hayajadhibitishwa.

    Nyanja zote za operesheni za kampuni ya Huawei barani Afrika zinaonyesha kwamba umuhimu wake katika maendeleo ya sekta ya teknolojia ya habari barani humo ni mkubwa mno.

    Kwa muda wa miaka kumi yaliyopita, kampuni hiyo imejenga sehemu kubwa ya Afrika ya miundombinu. Kila kitu, kutoka mtandao, muunganisho wa kihamisha-data ya kasi hadi vituo vipya vya data ya mawingu yametekelezwa na kampuni hiyo. Karibuni kulikuwa na makala yaliyofichua kuwa katika miaka 10-15 yaliyopita, karibu asilimia 70 ya Afrika nzima mtandao wa 4G ulijengwa na Huawei.

    Kampuni hiyo pia imeshiriki katika biashara ambayo inajumuisha kazi na serikali nyingi za Afrika. Kwa muda mrefu, Huawei imekuwa ikijenga mitandao ambao ni uti wa mgongo wa serikali kama vile vituo vya data pamoja na kutoa suluhisho katika sekta za uchukuzi, afya, elimu na mambo mengine yanayohusisha mawasiliano.

    Ingawa wadau katika Afrika wanakiri kwamba masuala ya usalama wa mtandao yanayoibuliwa ni muhimu, kampuni ya Huawei pamoja na wengi katika bara hilo wanaamini hili si suala kuu kwa sasa. Badala yake, wanashikilia kwamba upatikanaji wa mawasiliano nafuu, uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano na ubunifu wa kazi ni masuala ya kupewa kipaumbele.

    Sio siri kwamba kuna shauku kubwa ya kuwa mtandaoni Afrika. Huawei ni mtoaji mkubwa wa internet na ni maarufu katika shughuli kama kupitisha nyaya za mawasiliano baarini hadi kwenye simu za rununu na hiyo barani Afrika ina umuhimu mkubwa sana.

    Mkurugenzi wa masuala ya umma katika kampuni ya Huawei nchini Kenya Adam Lane anasema kwamba kampuni hiyo imejikita katika sekta ya mawasiliano barani Afrika. Kulingana na bwana Lane, kipengele muhimu katika biashara ya mawasiliano ni ufahamu kwamba ni biashara ya kutekeleza kwa muda mrefu. Anabainisha kwamba Huawei inahusika katika mradi wa biashara hadi biashara ambayo ina maana kuwa lazima wafanye kazi kwa pamoja na makampuni ya mawasiliano ya Afrika kama vile ya Safaricom, Telkom, MTN, Airtel kwa miongo kadhaa.

    "Hii inamaanisha unaanzisha biashara sahihi, ofisi sahihi, vyombo vya kisheria, unawaajiri wafanyakazi wa ofisini, na kujenga vituo vya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wako na wateja, na ni lazima uwe mmoja wa wenyeji ili ufanye kazi na makampuni haya kwa muda mrefu." Anasema Lane

    Kwa mujibu wa Lane, makampuni haya ya ndani hayako tayari kuingia kwenye mikataba ya kazi na makampuni ya nje kama Huawei ili kuwasilisha vifaa ambavyo hawawezi kuzipea huduma miezi mitatu baadaye, au ni kuziboresha miaka miwili baadaye. Kama kampuni ya biashara, Lane anasema Huawei inataka kutoa huduma hizi na kadhalika zinapohitajika.

    Bila shaka, imefahmika kuwa makampuni ya mawasiliano ya simu Afrika sasa yanategemea vifaa vya Huawei, na kufanya kampuni hiyo ya Kichina kama moja ya kutopuuzwa katika uendeshaji wa bishara ya mtandao.

    Lane anasisitiza kwamba utamaduni wa kazi katika kampuni ya Huawei na shughuli inayotekeleza barani Afrika ni ya kusisimua. Anaangazia hii kama sababu kuu ya Marekani kujaribu kupanda mbegu za shaka juu ya utendakazi wake kwa mataifa na makampuni yanayofanya kazi kwa karibu pamoja na kampuni hiyo.

    Anasema kampuni hiyo ilifanya uamuzi kuanzisha shughuli zake barani Afrika wakati ambapo hakuna kampuni nyingine iliyothubutu kufanya hivyo. Kulingana naye utamaduni huu wa kutaka kufanya jambo ambalo hakuna mwingine amejaribu imejikita katika wafanyikazi wake tangu kuanzishwa kwa Huawei.

    Lane anashangaa ni kwa nini Marekani ina wasiwasi wakati hakuna chombo kingine ambacho kimelalama kuhusu inavyoendesha shughuli zake.

    "Sisi tumekuwa tukifanya kazi hapa kwa miaka 20, hakuna mteja hata mmoja aliye na tatizo lolote nasi hadi sasa, iwapo kungekuwa na tatizo basi tuna washindani wetu na wangekuwa wamekimbilia hao. Kwanza ni tishio kwamba kama tuna tatizo, wateja watakumbatia makampuni mengine na bila shaka tutapoteza biashara." Anasema.

    Kampuni hiyo inadokeza kwamba watu wengi hawaelewi ukubwa wa Huawei katika suala la uwepo wake. Nchini Kenya kwa mfano, kampuni hiyo inadokeza kuwa ina wafanyakazi zaidi ya 400 wa moja kwa moja na wafanyakazi 2500 wa ziada walioajiriwa kupitia wanakandarasi wadogo wadogo.

    "Katika mitandao ya mawasiliano ya simu, hatufanyi kazi zote wenyewe, tunajaribu kufanya kazi na makampuni ya ndani iwezekanavyo. Hivyo sisi tunaweza kuwauzia vifaa na kuwapa mafunzo juu ya jinsi ya kutumia na kisha wanakandarasi hao wanaendeleza biasharaka iliyosalia kama kuzipeleka mikoani na vijijini." Anasema Lane

    Kampuni ya Huawei inasisitiza kwamba sifa zake ni msingi wa mafanikio ya biashara zake ambazo inasema zinafanya serikali za Afrika na taasisi mbalimbali kuwa tayari kufanya kazi nayo.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako