• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Wakandarasi China kukamilisha gati bandari ya Mtwara mwisho wa mwaka

    (GMT+08:00) 2019-06-18 09:30:07

    Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

    WAKANDARASI wa kampuni toka nchini China, China Railway Construction Engineering Group (CRCEG) na China Railway Major Bridge Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) wanaojenga gati namba mbili katika bandari ya Mtwara watakamilisha ujenzi mwishoni mwa mwaka huu.

    Ujenzi huo wa gharama ya Sh bilioni 137.4 zinazotolewa na serikali, wakandarasi hao wanafanya kazi chini ya mhandisi msimamizi ambayo ni Kampuni ya Inros Lackner ya Ujerumani.

    Gati hilo linalojengwa lina urefu wa mita 300 na ujenzi umefikia asilimia 52, likikamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye ukubwa wa tani 65,000 ikilinganishwa na gati la awali lenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa tani 45,000, lakini pia litakuwa na eneo la kuhifadhia mizigo lenye ukubwa wa mita za mraba 79,000 na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni moja kwa mwaka.

    Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) kupitia Bandari ya Mtwara mara baada ya kukamilika kwa ujenzi itahudumia tani zaidi ya milioni moja za mizigo kwa mwaka kutoka tani 400,000 za sasa.

    Mhandisi wa bandari hiyo, Norbert Kalembwe, anasema bandari hiyo ambayo ni lango kuu la biashara au uchumi kwa ukanda wa kusini mara baada ya kukamilika kwa gati hiyo, imejipanga kuwahudumia sio tu wateja wa ndani ya nchi bali na wa nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji.

    Meneja wa Bandari ya Mtwara, Juma Kijavara anasema kukamilika kwa ujenzi wa gati namba mbili kutaifanya bandari hiyo pia kuwa na uwezo wa kuhudumia tani zaidi ya milioni mbili kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

    Anasema bandari hiyo tangu ijengwe enzi za ukoloni mwaka 1953, ilivunja rekodi kwa kusafirisha tani 377,590 za mizigo katika Mwaka wa Fedha wa 2016/2017, huku mwaka 2018/19 ilisafirisha tani 363,286 na mwaka 2014/15 ilisafirisha tani 296,577.

    Tofauti na gati zingine zilizopo nchini na nchi jirani, gati namba mbili linalojengwa katika Bandari ya Mtwara lina kina cha asili cha mita 13 maji yanapokupwa, jambo linaloifanya bandari hiyo kuwa bora katika ukanda wa kusini ikilinganishwa na kina cha mita 9.5 cha bandari za nchi jirani.

    Kijavara anasema shehena kubwa ya mizigo inayohudumiwa na bandari hiyo ni zao la korosho ambalo ndiyo zao kuu la biashara kwa mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Shehana zingine ni saruji inayozalishwa na kiwanda cha Dangote.

    Pamoja na kuhudumia shehena za mafuta yanayokuja kwa ajili ya mikoa ya Lindi na Mtwara, Meneja huyo alisema bandari yake pia imejipanga kusafirisha tani 500,000 za makaa ya mawe kwa mwaka, tani zaidi ya 50,000 za jasi na tani zaidi ya 300,000 za saruji kwa mwaka inayozalishwa na kiwanda cha Dangote.

    Naye Ofisa Utekelezaji wa bandari hiyo, Ibrahim Ruzuguma, alisema Bandari ya Mtwara inapokea wastani wa meli tatu za mizigo kwa wiki, hivyo kwa mwezi inapokea meli 12 ikiwemo meli moja ya mafuta kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambayo inakuja bandarini hapo kila mwezi.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako