• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Balozi Wang aitaka Tanzania kutumia vizuri Mkutano wa Mawaziri wa FOCAC

    (GMT+08:00) 2019-06-24 15:35:56

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    BALOZI wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke ameitaka nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki kutumia vizuri Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) kuimarisha ushirikano wake na nchi hiyo ya Asia ya Mashariki.

    Katika mkutano huo unaofanyika jijini Beijing kati ya tarehe 24 na 25 mwezi huu wa Juni, ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof Palamagamba Kabudi.

    Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa China nchini Tanzania, Jumapili tarehe 23 mwezi Juni, ulieleza kuwa waziri Kabudi anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Bw. Wang Yi.

    Mazungumzo hayo yatajikita katika mambo mbalimbali yanayohusu ushirikiano wa nchi hizo mbili.

    Prof Kabudi pia anategemewa kuhudhuria maonesho ya Kimataifa ya Horticulture Expo ambayo yatajumuisha hafla maalum ya kutangaza kahawa ya Tanzania katika soko la China.

    Waziri Kabudi pia anatarajiwa kushiriki kwenye uzinduzi wa Maonesho ya China-Africa Economic and Trade Expo yatakayofanyika katika mji wa Changsha. Tanzania ni miongoni mwa nchi sita zenye hadhi ya mgeni maalum katika maonyesho hayo.

    Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Balozi Wang alisema anaamini kuwa ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo muhimu utatoa fursa nyingine ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na china

    Alisema Tanzania na China zimefanikiwa kulinda uhusiano wao kwa muda mrefu huku zikijitahidi kutekeleza kwa pamoja makubaliano na maazimio yaliyofikiwa katika Jukwaa la FOCAC la 2018.

    Aliongeza kuwa kuanzia mwaka jana pande hizo mbili zimeshuhudia ziara za viongozi mbalimbali zenye malengo ya kuimarisha ushirikiano huo.

    "Mwaka jana, tumeona Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Waziri wa Ujenzi Isack Kamwelwe na viongozi wengine wa nyadhifa mbalimbali wakitembelea China.

    Huku pia viongozi mbalimbali wa chama na serikali wa China wakifanya ziara nchini Tanzania," alisema balozi Wang.

    Aliongeza pia kuwa mwezi ujao wa Julai , Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Zubeir Ali Maulid wanategemewa kutembelea China.

    Alieleza kuwa ziara hizo za viongozi mbalimbali wa nchi hizo mbili zinasaidia kuimarisha ushirikiano na urafiki katika nyanja zote za kiuchumi, kijamii na kisiasa ambayo ni nguzo muhimu katika maendeleo.

    Balozi Wang alibainisha kuwa mwaka uliopita China iliandaa mikutano mbalimbali muhimu ikiwamo Jukwaa la pili la Ukanda Mmoja, Njia Moja na FOCAC ambapo Tanzania ilituma viongozi wake na kushiriki katika makubaliano na maazimio mbalimbali yenye tija kwa nchi hizo na kwa bara zima la Afrika.

    Alisema nchi yake iko katika mstari wa mbele kuhakikisha kuwa mahusiano yake na Tanzania yanazidi kuwa imara katika sekta zote ikiwemo sekta ya biashara na uwekezaji.

    Alisema China inabakia kuwa mbia mkubwa wa Tanzania katika uwekezaji na biashara ambapo mwaka jana biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.974.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako