• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Mazungumzo mradi wa Bagamoyo "kurejea"

    (GMT+08:00) 2019-07-17 08:58:30

    Na Majaliwa Christopher

    SERIKALI ya Tanzania na Kampuni ya China Merchants Holdings International ya zinategemea kurudi katika meza ya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa mradi wa Bagamoyo utakaogharimu Dola za Marekani Bilioni 10, imeelezwa.

    Mazungumzo hayo yalisitishwa baada ya Serikali ya Tanzania kudai kuwa masharti yaliyowekwa na mwekezaji huyo kuwa magumu na hayakujali maslahi ya nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.

    Balozi wa Tanzania nchini China Bw. Mbelwa Kairuki, Julai 11 akiwa Hong Kong alinukuliwa akieleza waandishi wa habari kuwa mazungumzo hayo yatasaidia kuweka sawa hali itakayofanya mradi huo uwe na faida na maslahi kwa pande zote mbili.

    Balozi Kairuki alikaririwa akisema kuwa kuna vipengele zaidi ya 20 ambayo bado hayajashughuliwa kikamilifu ambayo minne inahitaji hatua za Kibunge hasa katika vipengele vya kisheria.

    "Mradi huu (Bagamoyo) bado upo kwa sababu majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania yanatarjiwa kuendelea. Baadhi ya masharti aliyoweka mwekezaji hayana maana… tunategemea kupitia kwa majadiliano hayo tutafikia makubaliano mazuri," alisema Balozi Kairuki.

    Aliongeza kuwa; "Uzuri ni kwamba mwekezaji yuko tayari kwa majadiliano, Serikali ya Tanzania pia iko tayari."

    Hivi karibuni, Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa imesitisha utekelazaji wa mradi huo kwa sababu ya kutozingatia maslahi mapana ya nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.

    Baada ya kutangazwa kwa hatua hiyo, wabunge wa Bunge la Tanzania waliitaka serikali ya Tanzania kukamilisha mazungumzo na kampuni hiyo ya China ili uwekezaji huo uweze kuanza.

    Mradi huo mkubwa ulikuwa ugharimu takribani Dola za Kimarekani Bilioni 10, ambayo ni sawa na shilingi trilioni 23 za Tanzania.

    Walisema kwamba kushindwa kukamilika kwa mazungumzo hayo kwa sababu zilizoelezwa kwamba ni kwa manufaa ya taifa, haziridhishi.

    Wakichangia katika hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano iliyowasilishwa jijini Dodoma mwezi Mei mwaka huu, 2019, wabunge hao walisema ni muda muafaka sasa serikali ikachukulia suala hilo kwa uzito unaostahili.

    Akiwasilisha hotuba ya Wizara hiyo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema mradi huo ulisimama kwa sababu ya masharti yaliyowekwa katika kufikia mkataba huo.

    Masharti hayo ni pamoja na kuachiwa jukumu la tozo katika bandari na pia suala la uanzishwaji wa viwanda katika eneo la Bagamoyo na Tanga kuachiwa kampuni hiyo ya China.

    Wakati wa majadala huo, baadhi ya wabunge walitaka chombo hicho kiunde kamati maalum ya kuishauri serikali na pia kuwa na nafasi kujadili uamuzi wa serikali inapoachana na miradi mikubwa ya kimkakati.

    Wabunge hao walisema kwamba bandari ya Dar es Salaam kwa sasa pamoja na upanuzi wote, imefikia mwisho na haiwezi tena kubeba meli mpya za kizazi cha nne na kuendelea.

    Mbunge wa Malindi, Ally Saleh alisema inafaa Bunge na wananchi kuihoji serikali pindi inapoacha miradi mikubwa yenye tija kwa taifa kama mradi wa Bandari ya Bagamoyo.

    "Kwanini kama nchi tunaacha mradi kama huu..." alisema Bw. Ally na kuongeza kuwa mradi wa bandari haikuwa ujenzi wa bandari pekee, bali kutengeneza ukanda maalumu wa uchumi wa Bagamoyo ambao ungeleta ajira kwa nchi.

    Alisema bandari hiyo ambayo ingekuwa kubwa katika Afrika na ya pili kufuatia bandari ya Rotterdam, Uholanzi, ingeneemesha uchumi wa nchi kutokana na idadi za meli zilizokuwa zikitakiwa kutia nanga.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako