• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kampuni ya Sichuan Saifei Travel ya China kuwekeza $ 200m Tanzania

    (GMT+08:00) 2019-07-22 10:27:16

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    KAMPUNI ya Sichuan Saifei Travel Company Limited ya China imetenga Dola Milioni 200 za Marekani, sawa na Shilingi Bilioni 460 za Tanzania, kwa ajili ya uwekezaji katika wilaya ya Karatu, Mkoani Arusha, Kaskazini mwa Tanzania.

    Fedha hizo, pamoja na maeneo mengine, zitaelekezwa kwenye ujenzi wa hoteli ya nyota tano yenye vyumba 300.

    Uwekezaji huo mkubwa unatarajiwa kuanza mwezi wa tano mwakani, 2020, kwa mujibu wa Afisa Uendeshaji wa Kampuni hiyo kutoka nchini China, Bw. Richard Ma.

    Akiongea na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa Tanzani, Prof Adolf Mkenda, siku ya Jumamosi, Julai 20 wilayani karatu, Bw. Ma alisema kampuni yake imeiomba mamlaka ya wilaya hiyo kuipatia ardhi yenye ukubwa wa hekari 1,750 kwa ajili ya uwekezaji huo.

    "Karatu, kijiografia ni eneo la kimkakati. Ukaribu wake na kreta ya Ngorongoro imetushawishi kufikia uamuzi wa kuanzisha uwekezaji huu wa kujenga hoteli hapa," alieleza Bw. Ma.

    Mwekezaji huyo kutoka nchini China pia alieleza kuwa kampuni yake itajenga viwanja viwili vya kisasa vya mchezo wa gofu na kiwanja cha ndege kwa ajili ya kuwahudumia wageni wanaotembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

    "Shughuli zetu hapa siyo tu kwamba zitazalisha ajira kwa ajili ya wakazi wa eneo hili bali pia itasaidia kuvutia watalii wengi kutoka nchini China kuja Tanzania," alisema.

    Aliongeza kuwa uamuzi wao wa kuwekeza katika mradi wa hoteli Karatu unasababishwa pia na hatua ya hivi karibuni ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutaka kuanzisha safari ya moja kwa moja ya anga kutoka Dar es Salaam kwenda mji wa Guangzhou ifikapo mwezi Oktoba, mwaka huu.

    Kampuni hiyo ya Sichuan Saifei Travel yenye makao yake jimboni Chengdu, inasifika kimataifa kwa kutoa huduma za usafirishaji ndani na nje ya China.

    Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Bi. Theresia Mahongo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Bw. Rashid Taka alimhakikishia mwekezaji huyo kuwa Serikali imetenga hekari 2,100 wilayani humo kwa ajili ya uwekezaji.

    Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda, alisema kuwa uamuzi huo uliofikiwa na kampuni hiyo utawezesha Tanzania kuboresha sekta ya utalii na kuendelea kuvutia wageni wengi zaidi kutoka China na sehemu zingine duniani.

    "Huu ni mradi mkubwa kutoka China ambayo ni nchi yenye idadi kubwa ya watu ulimwenguni. Uwepo wa hoteli hii na uwekezaji mwingine utafanya watalii wengi kutoka nchi hiyo ya Asia ya Mashariki kumiminika hapa nchini kwetu," alisema Prof Mkenda.

    China inabakia kuwa mbia mkubwa wa Tanzania katika uwekezaji na biashara ambapo mwaka jana, 2018, thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia Dola za Kimarekani Bilioni 3.974.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako