• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Chuo cha Wanyamapori Tanzania chatakiwa kuanza kufundisha Kichina

    (GMT+08:00) 2019-07-22 10:29:32

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    CHUO cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi iliyoko Mkoani Mwanza, Tanzania kimetakiwa kuanza kufundisha lugha ya Kichina chuoni hapo ili kuwezesha Waongoza watalii kuwasiliana kirahisi na watalii kutoka nchini China.

    Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Bw. Constantine Kanyasu akizungumza jana Jumamosi, Julai 20, 2019 katika mahafali ya 54 ya Chuo hicho, alitaka Uongozi wa wa Chuo kuangalia namna ya kuanzisha programu ya lugha ya Kichina katika kozi zake.

    "Hatua hii itasaidia chuo hiki kutoa wataalamu watakaofanya kazi za kuongoza watalii wanaoweza kufanya mazungumzo kwa lugha ya Kichina," alisema Bw. Kanyasu.

    China kwa sasa ni moja kati ya nchi ambazo wananchi wake wanatembelea Tanzania kuangalia vivutio mbalimbali vikiwemo mbuga za wanyama na fukwe za bahari.

    Mwaka huu, 2019, Tanzania imendelea kupokea watalii kutoka nchini China ambapo mwezi Mei, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokea watalii wapatao 340 wakiwamo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Zhejiang, China.

    Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa 10,000 wanaotarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu.

    Sekta ya utalii nchini Tanzania imeajiri takriban watu 500,000 na wengine zaidi ya milioni moja wakijiajiri wenyewe hivyo kuchangia asilimia 17.5 katika pato la Taifa (GDP) hivyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayochangia pakubwa kwenye uchumi wa nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki.

    Kauli ya Naibu Waziri imekuja siku chache baada ya Serikali ya nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki kutangaza kuwa kwa mara ya kwanza wanafunzi wa shule 16 za Sekondari nchini humo wanaotarajia kufanya mitihani yao ya kidato cha nne mwaka huu, 2019, watafanya mtihani wa lugha ya Kichina.

    Dhamira ya Serikali ya Tanzania ni kuhakikisha kuwa nchi hiyo yenye mahusiano mazuri na China ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa, inakuwa na wataalamu wa lugha hiyo.

    Vilevile, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya Tanzania ilisema kuwa inakusudia kukiteua Chuo cha Ualimu cha Marangu kilichopo mkoani Kilimanjaro kufundisha kozi la lugha ya kichina kwa walimu tarajali ili baadaye waweze kufundisha somo hilo katika shule mbalimbali za Sekondari za Serikali humo.

    Hii ni hatua nzuri ya kukuza mahusiani na ushirikiano katika nyanja ya utamaduni. Nchini China lugha ya Kiswahili inayozungumzwa na zaidi ya watu milioni 100 barani Afrika tayari ilishaanza kufundishwa katika baadhi ya vyuo vikuu.

    Nchini Tanzania, mbali na wanafunzi wa sekondari wa kidato cha nne kuanza kuufanyia mtihani lugha ya Kichina mwaka huu, vyuo mbalimbali chini ya Taasisi ya Confucius vilishaanza pia kufundisha lugha hiyo ya Kichina ambayo huzungumzwa na watu zaidi ya bilioni moja duniani.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako