• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China, Tanzania watiliana saini ushirikiano sekta ya habari, mawasiliano

    (GMT+08:00) 2019-07-23 09:24:18

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    SERIKALI ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China siku ya Jumamosi, Julai 20, 2019, jijini Dar es Salaam wametiliana saini hati ya makubaliano kwa ajili ushirikiano katika sekta ya habari na mawasiliano.

    Hati hiyo ya makubaliano imetiwa saini na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Hassan Abbasi, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali kwa niaba ya Tanzania na Mkuu wa Shirika la Habari la Xinhua –Ofisi ya Dar es Salaam Bw. Li Sibo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.

    Hafla hiyo pia ilishuhudiwa na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke, Mhariri Mkuu wa Xinhua Bw. Hen Ping na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Dkt. Harrison Mwakyembe.

    Makubaliano hayo yaliyosainiwa mwisho wa wiki, yanalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya habari na mawasiliano pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa dhima ya kuboresha mahusiano kati ya nchi hizo mbili yaliyodumu kwa miaka zaidi ya 50 sasa.

    Kupitia kwa makubaliano hayo nchi hizo mbili pia zitakuwa katika mstari wa mbele katika kubadilishana habari sahihi na kwa wakati ambayo ni nguzo ya msingi kwenye shughuli za maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

    Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe alisema ushirikiano wa Tanzania na China umekuwepo kwa miaka mingi katika nyanja mbalimbali na sasa nchi hizo zimekua kama ndugu.

    Dkt. Mwakyembe alisema yapo mambo mengi yalioacha alama kwenye ushirikiano wa kindugu kati ya China na Tanzania, ikiwemo reli ya TAZARA.

    "Nafurahi kuona leo wenzetu wa Idara ya Habari Maelezo wanatiliana saini mkataba wa ushirikiano kati yao na Xinhua, hii inadhihirisha kukomaa kwa urafiki kati ya Tanzania na China na imeongeza wigo wa maeneo ambayo nchi hizi mbili zinashirikiana" Alisema Waziri Mwakyembe.

    Aliongeza kuwa ushirikiano mpya uliosainiwa kati ya Xinhua na Idara ya Habari utaimarisha zaidi sekta ya habari nchini Tanzania na pia utasaidia kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari na mawasiliano kwa ujumla.

    Kwa upande wake mhariri Mkuu wa Shirika la Xinhua ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha ukombozi cha watu wa China CPC Bw. He Ping, alisema amekuja Tanzania kuimarisha uhusiano wa kindugu ulioasisiwa na waanzilishi wa mataifa haya mawili, na pia kushuhudia utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya Idara ya Habari Maelezo na shirika la Habari la Xinhua.

    Alisema tangu mwaka 1969 Xinhua imekua ikipeleka wanahabari wake kufanya kazi katika nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki, lakini ushirikiano mahsusi kama ulioanzishwa kati ya Shirika hilo na Idara ya Habari, utasaidia katika upatikanaji wa habari nyingi za maendeleo.

    Dkt. Abbasi kwa upande wake, alisema habari ni maendeleo na ushirikiano huo ulioanzishwa utaendelea kuleta chachu ya maendeleo baina ya Tanzania na China.

    Mkataba huo una lengo la kuimarisha uhusiano katika kubadilishana habari na taarifa mbalimbali, kupitia magazeti na majarida lakini pia kupitia mitandao ya kijamii.

    Aidha katika Ushirikiano huo Idara ya Habari Maelezo italisaidia shirika la Xinhua katika kupanga na kufanya mahojiano na viongozi wa serikali, Taasisi na wakala mbalimbali pamoja na kuwawezesha waandishi wa Shirika hilo kufanya kazi zao kwa wepesi zaidi nchini Tanzania.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako