• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Kampuni ya CHICO kujenga barabara ya kuunganisha Tanzania, Kenya

    (GMT+08:00) 2019-08-01 09:07:21

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    KAMPUNI ya ujenzi ya China Henan International Corporation Group Co. Ltd (CHICO) Jumatano, Julai 31, 2019 wilayani Pangani, Mkoa wa Tanga imetiliana saini na Serikali ya Tanzania kutekeleza mradi wa ujenzi wa kipande cha barabara itakayounganisha Tanzania na Kenya.

    Mkataba huo utahusisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 50 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 66.8 za Tanzania.

    Barabara hiyo ni mradi mkubwa wa Afrika mashariki baina ya Tanzania na Kenya ambapo utajumuisha barabara za kuanzia Malindi-Mombasa-Lungalunga nchini Kenya hadi Horohoro mpakani.

    Mkataba huo ulisainiwa kati ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Bw. Patrick Mfugale kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na na Bw. Xiang Gang kwa niaba ya kampuni ya CHICO na kushuhudiwa na Waziri wa Ujenzi, Usafirishaji na Mawasiliano Isack Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martin Shigella.

    Bw. Mfugale alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utachukua miezi 24 na watahakikisha unaisha kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.

    "Mradi huo ni wa kimkakati katika nchi zetu hizi mbili za Afrika ya Mashariki, tutausimamia vizuri kuhakikisha unakamilika kwa wakati," alisema Mfugale.

    Kwa upande wake Waziri Kamwelwe alisema kuwa mbali na ujenzi wa barabara hiyo, Serikali ya Tanzanzania pia imepata Shilingi Bilioni 350 toka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa ajili ya ujenzi wa Daraja katika mto Pangani lenye urefu wa mita 525.

    Aliongeza pia kuwa ufadhili huo kutoka AfDB utagharamia ujenzi wa barabara ya Pangani-Makunge wenye urefu wa kilomita 120.

    Barabara hiyo inayounganisha Tanzania na Kenya, kwa upande wa Tanzania inaanzia Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo pamoja na ujenzi wa madaraja ya Mto Pangani na Mto Wami.

    Vilevile mradi huo, utahusisha ujenzi wa barabara zinazoingia hoteli za Kitalii zilizopo ufukoni mwa pwani ya bahari ya Hindi kwa wilaya za Pangani ambazo ni Mwarongo, Ushongo, Kipumbwi na barabara za mjini Pangani na Tanga.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako