• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Tanzania, kampuni mbili za China zatiliana saini mradi wa Daraja Ziwa Victoria

  (GMT+08:00) 2019-08-05 09:00:47

  Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

  SERIKALI ya Tanzania, Jumatatu, Julai 29, 2019 jijini Dar es Salaam imetiliana saini na kampuni za China Civil Engineering Construction Corporation na China Railway 15th Bureau Group kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi katika Ziwa Victoria mkoani Mwanza.

  Daraja hilo litakuwa na urefu wa kilomita 3.2, na utagharimu jumla ya fedha za kitanzania Bilioni 592.

  Utiaji saini huo ulifanywa na Mhandisi Patrick Mfugale, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Bw. Zhan Jang kwa niaba ya makampuni ya China Civil Engineering Corporation na China Railway 15th Bureau Group.

  Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema mradi huo utatekelezwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania bila kutegemea fedha za wafadhili.

  "Serikali hii ikiamua jambo inalivalia njuga na inahakikisha linakamilika kwelikweli, huu ni mkonga wetu watanzania na haijawahi hata siku moja mkonga ukamshinda tembo hivyo tunafanya na tutafanikiwa kwa sababu tunatumia fedha zetu wenyewe ili hao waliotukatisha tamaa washangae" alisema Waziri Kamwelwe.

  Amesemakuwa ni wakati sasa kwa watanzania kutembea kifua mbele kwani sasa kodi zao zinatumika ipasavyo katika kuwaletea maendeleo, ndio maana mradi huo mkubwa unaanza kutekelezwa, sambamba na miradi mingine kama ya umeme wa mto Rufiji pamoja na kuendelea kununua ndege mpya ili kuimarisha shirika la ndege.

  Amesema wahisani wengi walikuwa na masharti kwamba wakikuletea fedha wanakuletea na mkandarasi wao, hivyo amesema kwa Tanzania ya sasa haitakubalika kwani kuna mgawanyo wa majukumu na wataalam wa mikataba, kuna wataalam wa manunuzi na hata washauri katika miradi mbalimbali hivyo serikali iko makini sana hasa katika masuala ya mikataba ili wasiingie mikataba ambayo itakuja kuwa kifungo kwa watanzania.

  Waziri Kamwelwe amesema wakati wa ujenzi wa daraja kutakuwa na ajira za kudumu zaidi ya elfu moja na ajira zisizo za kudumu zaidi ya elfu kumi, kwakua fedha ni za watanzania ni wajibu wa serikali kuhakikisha fedha zinawanufaisha watanzania.

  Hafla ya utiaji saini mkataba wa Ujenzi wa Daraja la Kigongo Busisi ulihudhuriwa pia na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jafo , wakuu wa mikoa ya Mwanza na Geita, wabunge kutoka katika mikoa hiyo pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako