• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Zanzibar yanunua meli mpya ya Mafuta iliyowasili kutoka Shanghai China

  (GMT+08:00) 2019-08-09 14:34:55

  Theopista Nsanzugwanko,DAR ES SALAAM

  SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetimiza ahadi yake kwa wananchi wake ya kununua meli mpya ya mafuta MT Mkombozi II, baada ya meli hiyo kuwasili katika Bandari ya Zanzibar ikitokea Shanghai nchini China.

  Meli hiyo ya mafuta yenye urefu wa mita 86.2 na ina uwezo wa kupakia tani 3,500 za mafuta kwenye visima vinne vilivyomo katika meli hiyo na imetumia Euro milioni 14.3 kutengenezwa ambayo ni sawa na wastani wa Sh bilioni 36, ambako meli hiyo itaungana na meli ya MT Ukombozi I ambayo ipo nchini na yenye uwezo wa kupakia tani 2,400.

  Dk Shein anapata fursa ya kuiona meli ya MT Mkombozi II ikiwasili kutoka ukingoni mwa pwani ya Zanzibar jana, ikitokea usawa wa kisiwa cha Chumbe na kuelekea katika Bandari ya Malindi mjini Unguja ilipokwenda kutia nanga.

  Akiwa katika varanda ya jengo la Ikulu, Dk Shein kwa furaha kubwa aliiangalia meli hiyo ikiwasili, hasa kutokana na ahadi aliyoitoa na azma yake juu ya ujio wa meli hiyo mpya ya mafuta.

  Meli hiyo iliyotengenezwa na Kampuni ya Damen Shipyard ya Uholanzi, iliwasili katika Bandari ya Malindi Zanzibar na kupata mapokezi ya aina yake.

  Wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, viongozi wao na wafanyakazi wa taasisi nyingine za serikali na sekta binafsi, waliungana na baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria katika eneo la Bandari ya Malindi mjini Zanzibar kwa ajili ya mapokezi ya meli yao hiyo.

  Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe, alithibitisha ujio wa meli hiyo na kueleza jinsi hatua mbali mbali zilizochukuliwa kununua meli hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi kuwasili kwake nchini jana.

  Jumbe anasema meli ya MT Ukombozi II ni mpya, ambapo majadiliano ya ujenzi wake yalianza mwaka 2017 na mkuku wake uliwekwa rasmi Julai 2018 na ujenzi ulimalizika Aprili mwaka huu.

  Anasema hivi karibuni ujumbe kutoka SMZ, ulikwenda kuishuhudia meli hiyo Julai 8, 2019 ikiwa tayari imeshakamilika na ndipo wakafanya makubaliano na watengenezaji, Kampuni ya Damen Tanker Ship ya Uholanzi iliyoitengeneza.

  Jumbe anaeleza kuwa baada ya makubaliano hayo, meli hiyo ilianza safari ya kutoka Bandari ya Shanghai kwa siku 28 na kuwasili juzi katika maji ya pwani ya Zanzibar na jana iliwasili kwa makabidhiano rasmi na serikali na baada ya hapo itazinduliwa kwa ajili ya kuanza shughuli iliyokusudiwa.

  "Naomba sana kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutuamini kuisimamia kazi hiyo na hivi sasa tuko ukiongoni katika kuikabidhi meli hiyo," anasema Jumbe.

  Hizo ni juhudi za SMZ chini ya uongozi wa Rais Shein katika kuhakikisha sekta ya usafiri na usafirishaji inaimarika kwa kiasi kikubwa, ambako Desemba 2015 meli mpya ya MV Mapinduzi II iliwasili Zanzibar ikitokea nchini Korea Kusini ilikotengenezwa ikiwa ni agizo la Rais Shein la kununuliwa meli hiyo.

  MV Mapinduzi II ambayo ilitengenezwa na Kampuni ya Daewoo International ya Korea Kusini ilianza kutengenezwa Julai mwaka 2013 na hadi Desemba 2015 iliwasili Zanzibar ikiwa tayari kuanza kutumika.

  Jumla ya Dola za Marekani 30.4 zilitumika kutengenezea meli hiyo ambapo ujenzi wake hadi kukamilika ulichukua miezi 18 ikiwa na uwezo wa kuchukua abiria 1,200 pamoja na tani 200 za mizigo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako