• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yaweka rekodi kwa kutokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa miaka mitatu

    (GMT+08:00) 2019-08-23 15:08:29

    Na Theopista Nsanzugwanko

    China, nchi inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu duniani, ikiwa na watu zaidi ya bilioni 1.4, huku ikiwa nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, imefanikiwa kwa miaka mitatu kuhakikisha hakuna maambukizi ya malaria nchini humo, na itafikia malengo ya milenia ya kutokomeza maambukizi ya ugonjwa huo hadi kufikia mwaka 2020.

    Kutokana na takwimu za Shirika la afya duniani WHO, katika miaka ya 1940 kulikuwa na maambukizi milioni 30 na vifo 300,000 kutokana na malaria nchini China, lakini sasa ugonjwa huo ni historia, na kinachofanywa sasa ni kudhibiti kuingia kwa maambukizi hususan katika maeneo ya mipaka na nchi zenye maambukizi makubwa, na kuweka mikakati kusaidia kudhibiti ugonjwa huo kwa nchi husika.

    Kwa takwimu hizo, kwa nchi zenye idaidi kubwa ya vifo na maambukizi ya ugonjwa huo, inaonekana ni vigumu kufikia malengo hayo. Lakini kwa kutumia njia, mikakati, program pamoja na ushirikiano baina ya serikali kuu, serikali za mitaa pamoja na wananchi, inawezekana kufanikisha hilo katika nchi mbalimbali duniani.

    "Wakati nilizaliwa kijijini, ugonjwa wa malaria ulikuwa ni mkubwa, ambapo katika kizazi cha baba yangu, ndugu zake wawili walikufa kutokana na ugonjwa huo." Anasema profesa Yang Henglin, ambaye kwa sasa ni mshauri mwandamizi katika Taasisi ya vimelea vya magonjwa.

    Profesa Yang amejumuisha mikakati ya kudhibiti malaria kwa miaka mingi akifanya kazi ya kumaliza maambukizi ya ugonjwa huo huko Yunnan, mkoa wa mpakani uliopo kusini magharibi mwa China, na kusaidia kupunguza maambukizi hayo kwa kiasi kikubwa kutoka maambukizi 400, 000 kwa mwaka 1953 mpaka kutokuwa na maambukizi mwaka 2016.

    Inaelezwa kuwa, mwaka 1955, China ilianzisha Programu ya Taifa ya kudhibiti Malaria, kupitia uhamasishaji wa jamii katika kilimo cha umwagiliaji, kupunguza mazalia ya mbu, kutumia dawa za kuua mbu na vyandarua wakati wa usiku, huku mamlaka za afya zikielekezwa kuweka mikakati kuzuia maambukizi.

    Baada ya mkakati huo, mwisho wa mwaka 1990, maambukizi ya malaria nchini China yalishuka kufikia 117,000, na vifo kutokana na magonjwa yanayoendana na ugonjwa huo vikipungua kwa asilimia 95.

    Kwa kushirikiana na Shirika la Global Fund linalolenga kupambana na magonjwa ya ukimwi, kifua kikuu na malaria, kuanzia mwaka 2003, China ilipiga kasi kwa kutoa mafunzo, kuajiri watumishi, vifaa vya maabara, madawa na mikakati ya kudhibiti mbu ili kugundua haraka wagonjwa walioambukizwa malaria, kuwatibu na kuzuia maambukizi. Chini ya ushirikiano huo, dola za kimarekani milioni 100 zilitumika kwa zaidi ya miaka 10 kusaidia kumaliza malaria katika wilaya 762 ambapo maambukizi kwa wakati huo yalipungua na kufikia chini ya 5,000 kwa mwaka.

    Profesa Yang Henglin anasema, katika miaka ya hivi karibuni, China imewekeza vya kutosha katika mikakati ya kitaifa kuondoa malaria. Tangu mwaka 2014, nchi hiyo imekuwa ikitenga fedha kutoka pato la ndani katika program ya kuondoa malaria. Kwa kufanya hivyo serikali imeonesha dhamira yake ya kutokomeza kabisa maambukizi ya ugonjwa huo.

    Ili kufikia malengo hayo, China imekuwa na mkakati mwingine wa "1-3-7" ambao kabla ya kuendelea kwa maambukizi katika siku 1, maambukizi yoyote lazima yatolewe taarifa, katika siku 3 kituo cha wilaya cha kukinga na kukabiliana na magonjwa lazima kuhakikisha na kuchunguza maambukizi na kuangalia madhara yake, na katika siku 7 kituo hicho kimechukua hatua kuhakikisha hakuna maambukizi kwa kuwapima wananchi wa eneo husika lilipotokea maambukizi.

    Mwaka 2010, China iliweka mkakati wa kuwa na muda maalumu kuhakikisha inaondoa ugonjwa huo itakapofika mwaka 2020, ili kwenda sambamba na malengo ya maendeleo ya milenia ya kudhibiti ugonjwa huo. China iliweka mikakati kwa kushirikisha wizara 13 ikiwemo afya, elimu, fedha, utafiti na sayansi, maendeleo, usalama wa umma, jeshi, polisi, biashara, teknolojia ya mawasiliano na viwanda, vyombo vya habari na utalii ambazo ziliungana kuondoa madhara ya ugonjwa huo nchini.

    "Tuligundua kuwa ni muhimu kushirikiana na idara zote muhimu na kujumuisha jamii ili kufanikisha malengo haya katika malaria." Anasema naibu mkurugenzi wa idara ya kinga na udhibiti wa magonjwa ya wizara ya afya ya China Bw He Qinghua.

    Katika wilaya ya Mengla, iliyoko mpakani na nchi ya Laos, ni rahisi kuona jinsi sera ya kitaifa imekuwa ikitekelezwa katika majimbo, wilaya, miji, mpaka vijiji, kwani sera inapotungwa kila mamlaka inafuata. Naibu mkurugenzi wa Halmashauri ya kudumu ya Bunge la umma la wilaya hiyo Bibi Yi Yue anatoa ufafanuzi, kwamba kila mwaka wanaandaa mkutano wa kazi na idara tofauti wilayani ikiwemo ya afrya na fedha, na kujadili maendeleo ya kazi hiyo, changamoto zilizopo na mpango wa kazi kwa mwaka ujao, kwani njia hiyo inawezesha kufikia malengo ya kumaliza malaria.

    Tangu mwaka 2010 China iligawa wilaya zake 1,355 za bara zenye matatizo ya malaria katika makundi kulingana na mzigo wa ugonjwa huo, na kila mwaka kundi la kwanza na la pili (wilaya zilizokumbwa na maambukizi ya malaria katika miaka mitatu iliyopita) iliweka mikakati kupambana na ugonjwa huo.

    Mwaka 2016 kulikuwa na maambukizi matatu yaliyoripotiwa nchini humo, mwaka 2017 na mwaka 2018 hakukuwa kabisa na maambukizi, na mpaka sasa bado hakuna maambukizi yaliyotangazwa.

    Ili kuhakikisha ugonjwa huo haurejei nchini humo, mkoa wa Yunnan unaopakana na nchi tatu zenye maambukizi ya malaria za Laos, Myanmar na Vietnam, umekuwa na mikakati kuhakikisha hakuna maambukizi mapya yanaingia nchini kwa kuwa na timu inayotoa mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na maambukizi mapya yakitokea kwa kutumia njia ya "1-3-7".

    Mkoa huo una vituo 68 vya kujikinga na malaria vyenye wafanyakazi na vifaa vya kupima damu, na kutoa taarifa kama kuna maambukizi, huku China ikipeleka wataalamu wa afya kwa nchi majirani za Laos na Myanmar ili kuzisaidia kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo.

    Profesa Yang amesema, ili kuhakikisha ugonjwa huo haurejei China, mikakati yote waliyotumia inaendelea huku kukiwa na tishio la kurejea tena kwa maambukizi kama hatua za kuondoa ugonjwa huo zisipoendelea .

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako