• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China inavyohimiza ushirikiano wa kiutamaduni kupitia utengenezaji, unywaji wa chai

    (GMT+08:00) 2019-09-09 14:01:26

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    KATIKA jitihada zake za kueneza utamaduni wake barani Afrika, China --nchi yenye idadi kubwa ya watu duniani, imeanza kutangaza na kueneza 'utamaduni wa unywaji chai' nchini Tanzania.

    Chai, kwa nchi nyingi na jamii nyingi duniani, ni kinywaji tu cha kawaida na mara nyingi hunywewa wakati wa asbuhi kama sehemu ya kifungua kinywa.

    Zaidi ya hapo, wengine hupenda kunywa chai ili kudhibiti hali ya baridi. Lakini, nchini China, hali ni tofauti. Chai ni sehemu ya utamaduni. Hunywewa asbuhi, mchana, jioni na hata usiku.

    Mgeni yeyote, wakati wowote anapotembelea familia yoyote nchini China, baada ya salamu, kifuatacho ni chai. Huu ni utamaduni wao. Wanaupenda na wanaudumisha.

    Pamoja na kuchangamsha mwili kwa ladha ya kipekee, Wachina wanaamini kuwa chai ina faida nyingi kiafya, kiasi cha kuifanya kuwa kinywaji cha muhimu na cha lazima.

    Nchini Tanzania, China kupitia Ubalozi wake jijini Dar es Salaam inasisitiza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano wake wa kiutamaduni na nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki kwa kubadilishana ujuzi wa namna ya kutengeneza chai ya Kichina.

    Mkurugenzi wa Utamaduni katika Ubalozi wa China nchini Tanzania Bw. Gao Wei jijini Dar es Salaaam hivi karibuni katika semina maalum ya utengenezaji wa chai ya kichina, alisema kuwa utengenezaji na unywaji wa chai ni moja ya nguzo kubwa na muhimu ya jamii ya China, hivyo basi wanafurahi kuona utamaduni huo ukiigwa na marafiki na ndugu zao kutoka Tanzania na maeneo mengine ya bara la Afrika.

    "Tunataka kuwafundisha Watanzania namna ya kutengeneza chai ya Kichina. Kupitia kwa mafunzo haya, washiriki watajua namna ya kuandaa kinywaji hiki na umuhimu wake katika kudumisha utamaduni," anasema Bw. Gao.

    Historia inaonyesha kuwa chai kwa miaka ya nyuma ilikiwa inatumika kwa matambiko mbalimbali nchini China na majani ya chai yalikuwa yakiliwa kama mboga au dawa kwa ajili ya kutibu maradhi mbalimbali.

    Lakini kwa sasa, hali imekuwa tofauti. Unywaji chai nchini China imekuwa ni utamaduni na sehemu ya maisha ya kila siku.

    Serikali nchini humo imeenda mbali zaidi na kujenga maeneo maalumu, kimsingi, kwa ajili ya kuhakikisha utamaduni huu unadumishwa na kuendelezwa.

    "Tunaamini kabisa kuwa wapenzi wa chai wanastahili kinywaji bora chenye kuchangamsha na kuburudisha ambacho kimsingi ni nzuri kwa afya," anasisitiza Bw. Gao, na kuongeza kuwa wanaamini ushirikiano wa kiutamaduni kati ya China na Tanzania utazidi kuimarishwa zaidi kupitia kwa utamaduni huu wa chai.

    Prof Zhou Ling kutoka Jimbo la Yunnan anasema kuwa chai ina faida nyingi kiafya lakini pia inahitaji mfumo mzuri wa maisha kwa ujumla.

    "Chai ina mchango mkubwa kwenye historia ya China. Pia ina nafasi ya kipekee katika Mahusiano ya kiutamaduni katika ya China na nchi zingine," anasema Prof Zhou na kuongeza kuwa ni miaka 5,000 sasa imepita tangu nchi hiyo ya Asia ya Mashariki ianze matumizi ya kinywaji hicho muhimu kwa afya.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako