• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais Magufuli, Museveni wafurahishwa na kampuni ya ujenzi ya China

    (GMT+08:00) 2019-09-09 14:05:12

    Na Majaliwa Christopher, Dar es Salaam

    MARAIS wa Tanzania na Uganda Dkt. John Magufuli na Yoweri Museveni wameipongeza kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE--East Africa Ltd) kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa viwango na ubora wa kimataifa.

    Jengo hilo lililojengwa na kampuni hiyo ya China ilizinduliwa rasmi na marais hao wawili wa nchi za Afrika ya Mashariki mwishoni mwa wiki, wakionyesha imani kubwa kwa kampuni hiyo kwa utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa Tanzania.

    Kampuni hiyo ya ujenzi kutoka nchi hiyo ya Asia ya Mashariki ambayo inatekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu ndani ya nchi za Afrika ya Mashariki imetimiza miaka 50 ya shughuli zake katika ukanda huo wa Afrika.

    Jengo hilo limejengwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 150 kwa ufadhili wa International Financing Corporation (IFC).

    Rais Magufuli alisema uzinduzi wa jengo hilo la Taasisi ya Mwalimu Nyerere imekuja kipindi nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki inapoelekea kuadhimisha miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

    Shughuli ya uzinduzi wa jengo hilo pia ilihudhuriwa na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke ambaye alisema kuwa jengo hilo litakuwa alama na ishara ya kumbukumbu ya hayati Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14, 1999.

    Balozi Wang aliongeza kuwa Nyerere anabakia nguzo muhimu ya kukumbukwa kwani jitihada zake ndio zilichangia kuanzishwa kwa urafiki kati ya Tanzania na China ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa.

    Jengo hilo lililojengwa na kampuni ya CRJE lina eneo la takribani mita za mraba 3,600 ambazo zinapangishwa kwa ajili ya kuipatia taasisi hiyo ya Mwalimu Nyerere mapato ya kujiendesha, litajumuisha hoteli ya kiwango cha nyota tano , ijulikanayo kama Johari Rotana na mwendeshaji wake ni Rotana Hotels corporation ya Dubai.

    Pia, jengo hilo litakuwa na ofisi za utawala, maktaba itakayokuwa na nyaraka na kumbukumbu za Baba wa Taifa zinazohusu maendeleo, amani, umoja na mfumo wa uchumi duniani na pia chuo cha mafunzo ya uongozi

    Kwa upande wake, Rais Museveni wa Uganda alisema amekuwa mfuasi wa Mwalimu Nyerere tangu mwaka 1963 kutokana na mchango wake mkubwa kwenye Ukombozi wa bara la Afrika na pamoja na mchango wake kwenye matumizi ya lugha ya Kiswahili.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako