• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • Mwekezaji kutoka China atangaza nia ya kufufua kiwanda cha mshubiri nchini Kenya

  (GMT+08:00) 2019-09-10 09:55:56

  Na Eric Biegon-NAIROBI

  Mwaka 2004, kiwanda kilichogharimu mamilioni ya pesa cha aloe vera au mshubiri kilianzishwa katika eneo la Baringo. Jamii inayoishi sehemu hiyo iliona hatua hii kama baraka kwani hii ingewasaidia kujikwamua kutoka minyororo ya ufukara uliokithiri katika asilimia kubwa ya sehemu hiyo.

  Mradi huo hata hivyo ulisitishwa ghafla kwa kiasi kikubwa kutokana na bei mbaya ambayo ilisababisha kupungua kwa malighafi kwani wakulima wengi walikata tamaa.

  Licha ya hofu kwamba kiwango cha mmea huo unaozalishwa katika eneo hilo haingetosha kuendeleza mradi huo, wakulima sasa wamo mbioni kufufua upanzi wake kutokana na thamani yake ya kiuchumi.

  Kuwasili kwa mwekezaji wa Kichina ambaye ametangaza nia ya kufufua kiwanda hicho imekuwa habari ya kutia moyo kwa wenyeji ambao wanaamini hii itabadili mkondo wa maisha yao.

  Akizungumza wakati wa ziara ya kiwanda hicho, mwekezaji huyo Ching Pak alifichua kwamba mmea huo wa aloe vera unahitajika sana hasa nchini China. Kwa sababu hii, aliwahimiza wakulima kujishughulisha na biashara ya kupanda mmea huo jinsi ukulima wa chai, kahawa au pareto unavyopewa kipaumbele sehemu zingine nchini kwani soko lake liko tayari.

  Ching alibainisha kuwa kuna aina zaidi ya 100 ya mmea huo wa mshungi huku akiweka wazi mpango wake wa kujenga kituo cha utafiti ambacho kitakuwa kikipeana maarifa kwa wakulima kuhusu aina ya mmea huo unaohitajika kupandwa hasa kwa madhumuni ya kibiashara.

  Aidha, mwekezaji huyo aliahidi kuanzisha sehemu ya kukuza miche ya mmea huo ambapo wakulima watakuwa wakipata miche yao kwa urahisi.

  Mbunge wa eneo hilo Charles Kamuren alisema uamsho wa kiwanda cha aloe vera itaongeza njia za mapato miongoni mwa wenyeji ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea chakula cha msaada.

  Mbunge huyo alitoa wito kwa serikali kujenga uwezo wa wakulima katika eneo hilo kuwa na uwezo wa kuzalisha mmea huo kwa wingi hili kusaidia mwekezaji huyo kutoka China katika mipango yake ya kufufua kiwanda hicho na kupanua biashara ya mmea huo katika eneo hilo.

  Takriban hekta 10,000 za ardhi zimewekwa chini ya mmea huo kwa sasa. Wataalam wanasema mshungi una thamani ya lishe kwa mwili wa binadamu. Pia, mmea huo ni sehemu muhimu kwa viwanda vya madawa na mapambo.

  Maji yake kulingana na wataalam hutumika kutengeneza baadhi ya sabuni na bidhaa nyinginezo. Bei ya maji ya aloe vera kwa sasa imeongezeka kutoka Shilingi 35 kwa lita hadi shilingi 50.

  Kando na matumizi ya kiviwanda, majani ya mmea huu hutumika kutibu majeraha na kusaidia uponyaji wa haraka. Maji yake inatumika kuongeza hamu ya chakula bila kusahau uwezo wake wa kutibu malaria, homa ya matumbo, kuharisha, kuvimba kwa mwili, kuvuja damu, maumivu ya kichwa, nimonia, maumivu ya kifua na kutumika kama kiua viini.

  Mmea huo ni wa kipekee kwa vile unaweza kukua katika udongo duni na kustahimili ukame, na kuifanya iwe ya thamani katika nyanda za malisho.

  Ingawa wakulima walipigwa marufuku kuvuna mmea huo mwitu chini ya amri 1986 ya Rais, kuongezeka kwa thamani yake ya kibiashara kimeifanya kuwa hitaji la wengi.

  Kwa muda mrefu mmea wa mshubiri ulionekana kama kero kwa wakazi wa eneo la Baringo. Lakini mambo yamebadilika kwani mmea huo umegeuka na kuonekana kama suluhisho la umaskini.

  Wakulima kutoka katika eneo hilo ambapo kiwanda hicho kimejengwa wanaamini kwamba kufufuliwa kwake itakuwa baraka kwao na wameahidi kuongeza eneo la ardhi chini ya mmea huo.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako