• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China Academy of Building Research yaanza upembuzi yakinifu mradi wa upanuzi Taasisi ya Moyo ya JKCI Mloganzila

  (GMT+08:00) 2019-09-17 09:54:38

  Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

  UJUMBE wa wawakilishi kutoka China Academy of Building Research wamefika nchini kwa ajili ya kupata taarifa zinazohusiana na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), awamu ya pili katika eneo la Mloganzila Jijini Dar es Salaam.

  Mradi huo ni miongoni mwa matunda ya ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa aliyoifanya China mwaka jana.

  Kupitia mradi huo serikali imejizatiti kuboresha na kupanua miundombinu ya JKCI ili kuifanya taasisi hiyo kuwa mahiri ya tiba ya magonjwa ya moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara.

  Ujumbe huo umetembelea Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, kupata taarifa zinazohusu eneo litakapojengwa jengo jipya kwa ajili ya upanuzi wa taasisi hiyo.

  Ofisa Mipango wa JKCI, Vida Mushi aliwaeleza kuwa kwa sasa taasisi ina ufinyu wa eneo, ukilinganisha na idadi ya wagonjwa wanaopata matibabu katika taasisi hiyo.

  "JKCI inaona wagonjwa kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, ujenzi wa upanuzi wa jengo jipya la JKCI katika eneo la Mloganzila umelenga kuifanya JKCI kuwa taasisi mahiri ya tiba ya magonjwa ya moyo Kusini mwa Jangwa la Sahara," anasema Mushi.

  Aidha, anasema kwa sasa JKCI imewapokea wawakilishi kutoka China Academy of Building Research, waliokuja kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu eneo la Mloganzila ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa jengo jipya la JKCI.

  Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori anaipongeza serikali kupitia JKCI, kuhakikisha matibabu ya magonjwa ya moyo, yanapewa kipaumbele ukizingatia magonjwa ya moyo ni magonjwa yanayokua kwa kasi.

  Anasema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu ya watu wenye magonjwa ya moyo nje ya nchi hivyo , huduma hizo kusogezwa karibu na wananchi ni jambo la neema na itasaidia wananchi wengi kutokulazimika kutumia gharama nyingi kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nje ya nchi.

  Makori anasema Manispaa ya Ubungo imewapokea wataalamu kutoka China Academy of Building Research kupata taarifa zinazohusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa upanuzi wa JKCI wa awamu ya pili eneo la Mloganzila na kutoa ushirikiano kwa kuwapatia taarifa zilizojitosheleza ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

  "Baadhi ya taarifa walizotaka kufahamu wakati wa upembuzi wa eneo la Mloganzila ni pamoja na miundombinu iliyopo katika eneo la Mloganzila, upatikanaji wa maji, upatikanaji wa umeme na vibali vyote vinavyohusika na ujenzi, tutaendelea kutoa ushirikiano katika hatua zote za ujenzi wa mradi huo kwani ni mradi wa maendeleo kwa nchi yetu katika utoaji wa huduma za afya," anasema Makori.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako