• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Juhudi za kampuni moja za kupambana na umaskini zazaa matunda Kusini Magharibi mwa China

    (GMT+08:00) 2019-09-27 14:29:55

    Na Eric Biegon - GUIZHOU, CHINA

    Kwa miaka mingi, umaskini uliokithiri ulidhihiri hali mbaya ya kiuchumi ya maeneo kadhaa ya kusini magharibi mwa China. Jimbo la Guizhou lililojaa milima, kwa mfano, limekuwa nyumbani mwa mamilioni ya watu masikini.

    China hata hivyo kwa sasa inagonga vichwa vya habari kwa sababu ya kuwaondoa mamilioni ya raia wake kutoka maisha ya uchochole. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, China, ambayo imeendelea na kuwa uchumi mkubwa wa pili duniani, imeandikisha maendeleo ya ajabu katika miaka 40 yaliyopita baada ya kuwakwamua zaidi ya watu 800,000,000 kutoka kwa minyororo ya ufukara.

    Kwa maneno ya Rais Xi Jinping mwenyewe, "hakuna mtu yeyote ambaye ataachwa nyuma katika juhudi za kuboresha viwango vya maisha ya watu na hali zao" katika juhudi za kutokomeza janga la umasikini ifikapo mwaka 2020.

    Kutokana na ndoto hii, maeneo ya mbali na mashinani nchini China, kama vile wilaya kadhaa katika mkoa wa Guizhou, kwa sasa yanashuhudia mabadiliko makubwa.

    Muda unayoyoma na serikali inashirikisha mikakati mbalimbali ya kufikia lengo hili. Mojawapo wa juhudi hizo ni ushirikiano unaoendelea baina ya serikali na kampuni ya kibinafsi ya Evergrande Group katika kampeni za kupambana na umasikini kusini magharibi mwa China.

    Kampuni hiyo iliitikia mwito wa utawala wa chama cha kikomunisti nchini humo mwaka 2015 na kuanzisha miradi mbalimbali za kiuchumi katika kaunti saba zilizoko eneo la Bijie, na kuwekeza jumla ya yuan 11,000,000,000 kama sehemu ya mipango yake ya kutoa msaada kwa jamii.

    Serikali ya jimbo hilo linasema takriban majina ya watu 600,000 kutoka eneo hilo yameondolewa kutoka kwenye orodha ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini.

    Kampuni hiyo ya China inasema inawalenga watu wengine 444,400 katika eneo la Bijie pekee ambao wamepangiwa kukombolewa kutoka kwa maisha ya umaskini kufikia mwaka ujao.

    Wakati kampuni hiyo ya Evergrande Group ilitua katika jimbo hilo, ilizindua utaratibu maalum wa kupunguza umaskini kama vile kuweka viwanda, uhamisho watu maskini, pamoja na utoaji wa elimu na ajira kwa wenyeji kama njia ya kupambana na tishio hilo.

    Mwanzo, kampuni hiyo iliwekeza Yuan 4,800,000,000 ili kujenga maeneo mawili makubwa zaidi ya kukuza mboga na matunda katika sehemu hiyo. Pia ilianzisha kituo kikubwa cha uzalishaji wa ng'ombe katika eneo hilo.

    "Hadi sasa, tumewasaidia takribani watu 1,000,000 maskini kupitia maendeleo ya mashamba ya mboga, makundi ya ng'ombe, na upanzi wa dawa za Kichina na ukulima wa matunda." Mojawapo wa wakurugenzi wa Evergrande Group Lu Xianwu alisema

    Wakati huo huo, sekta ya nyama ilikuwa inaendelea kupanuka. Kampuni hiyo ilianzisha shamba la uzalishaji ambapo ng'ombe 100,000 ya aina ya Angus kutoka Australia zilihifadhiwa, wakati ng'ombe wa nyama 500,000 walikuwa wananoneshwa, pamoja na maendeleo ya sehemu 100,000 za uzalishaji.

    Wakati shughuli za kiuchumi ziliendelea kupata sura katika maeneo ambayo yalikaliwa na umaskini, kampuni hiyo ilianzisha mradi wa kuwahamisha walioathirika. Kampuni hiyo iliwekeza mabilioni ya pesa kujenga jamii 12 za wahamiaji ambapo iliwapa makazi mamia ya maelfu ya watu walioondolewa kutoka sehemu ya milima.

    Evergrande baadaye ilisonga mbele na kujenga vituo vya elimu na kibiashara. Wote waliohamia hapa wameajiriwa katika maeneo haya.

    Aidha, kampuni hiyo iliwasajili watu masikini kwa mpango wa mafunzo ya kiufundi katika jitihada za kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa maelfu ya wenyeji.

    "Tumeisaidia mji huu kwa kutoa mafunzo kwa watu 112,714, na kupendekeza watu 75,456 kutoka hapa kupata ajira kwingineko." Alisema

    Bila kukoma, kampuni hiyo iliendelea kuanzisha shule za chekechea, za msingi, na Chuo cha ufundi ambacho kwa sasa kinatumika. Taasisi hiyo kwa sasa imetia saini ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tsinghua hili kuendeleza juhudi hizi.

    Huduma za afya ni sehemu muhimu na hivyo kampuni hiyo pia ilijenga eneo la uuguzi na taasisi ya ustawi wa watoto kando na hospitali ambayo tayari inawahudumia wenyeji kikamilifu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako