• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Rais wa Zanzibar aahidi kuendelea kuthamini uhusiano na China

    (GMT+08:00) 2019-11-07 14:38:01

    Na Majaliwa Christopher

    ZANZIBAR itaendelea kuthamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na China sambamba na Chama chake cha Kikomunisti cha (CPC).

    Rais waa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alitoa kauli Hiyo Jumamosi, Oktoba 26, katika Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CPC, Bw. Guo Yezhou.

    Dkt. Shein alisema kuwa huwezi kuzungumzia maendeleo ya Zanzibar bila ya kuihusisha Jamhuri ya Watu wa China kupitia chama hicho, hiyo ni kutokana na uhusiano na ushirikiano mwema na wa kihistoria ulipo baina yao

    Rais Shein alisema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imeifanyia mambo mengi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa uungaji mkono wake katika kuimarisha sekta za maendeleo.

    Akitoa ushuhuda jinsi ya Jamhuri ya Watu wa China ilivyoisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo afya, elimu, viwanda, kilimo, sekta ya habari, miundombinu, michezo na mengineyo Rais Dk. Shein alisema kuwa nchi hiyo ni marafiki wa kweli kwani imeanza ushirikiano mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964.

    Aliongeza kuwa mbali ya Serikali ya China kusaidia sekta hizo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Sukari Mahonda, Kiwanda cha Sigareti Maruhubi, Viwanda vyenginevyo pia, nchi hiyo imeleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu kwa kutoa nafasi nyingi za masomo nchini mwake.

    Alieleza kuwa kubwa kuliko yote hayo ni ukarabati mkubwa wa Hospitali ya Abdalla Mazee Mkoani Pemba, Ukarabati wa uwanja wa Mao Zedong pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege Terminal III.

    Aidha, Rais Dkt. Shein alimueleza kiongozi huyo haja ya kukuza ushirikiano uliopo kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) pamoja na Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kama ulivyofanywa na waasisi wake Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong.

    Alieleza kuwa ushirikiano huo ulianza tokea mwanzo wa vyama vya ASP, TANU na hatimae kuja kwa CCM na kueleza urafiki mzuri uliooneshwa na viongozi wa pande mbili hizo kwa kutembeleana ambao umekuwa ukiendelezwa hadi hivi leo.

    Sambamba na hayo, Rais Dkt. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani zake kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kupitia CPC kusaidia ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Julius Nyerere kinachojengwa Wilaya ya Kibaha Mkoni Pwani.

    Dkt. Shein alitoa pongezi na salamu kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China na Mwenyekiti wa CPC Xi Jinping kwa kuendelea kuiunga mkono Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

    Kwa upande wake, Bw. Guo Alisema kuwa miongoni mwa lengo la ujio wake ni kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar huku na yeye akitumia fursa hiyo kutoa salamu za Rais Xi Jinping kwa Rais Dkt. Shein.

    Kiongozi huyo alimueleza Rais Dkt. Shein kuwa kutokana na China kuthamini juhudi za Tanzania ilizozichukua katika kuiunga mkono nchi hiyo ndipo Rais Xi Jinping alitoa tunzo kwa Waziri Mkuu Mstaafu Dkt. Salim Ahmed Salim hivi karibuni ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika kuiwezesha China kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa (UN).

    Pia, Kiongozi huyo alimuhakikishia Rais Dkt. Shein kuwa China itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo na kupongeza miradi ambayo tayari imeshakamilika huku akisisitiza kuwa bado nchi hiyo itaendeleza hatua zake za kuisaidia Zanzibar ikiwemo kuleta wataalamu wakiwemo madaktari kutoka Jimbo la Jiangsu.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako