• Idhaa ya Kiswahili
 • Uchumi
 • Michezo
 • Facebook
 • ChinaABC
 • Sayansi
 • Afya
 • China yaipa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) magari 12

  (GMT+08:00) 2019-11-13 10:06:33

  Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

  CHINA imeahidi kuipa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) magari 12 yenye thamani ya dola za Marekani US$400,000 ili kutumika katika programu mbalimbali za kuwajengea jamii uwezo.

  Ahadi hiyo ilitolewa na mshauri wa ubalozi katika masuala ya siasa katika ubalozi wa China nchini, Liang Lin, kuwa China iko tayari kufanya kazi na EAC katika fani mbalimbali kama elimu,maendeleo ya miundombinu, biashara,kukabiliana na Ebola, ulinzi na usalama na mikakati ya kujenga uwezo.

  Liang Lin anasema China imekuwa ikifanya kazi katika miradi mbalimbali ya miundombinu inayosaidia kuunganisha nchi za kiafrika ikiwemo mtandao wa barabara na Reli pamoja na masuala ya nishati, kuunganishwa kwa mtandao wa nishati na upanuzi wa bandari.

  Anasema China pia imekuwa ikisaidia katika ujenzi wa maeneo ya viwanda katika nchi wanachama za jumuiya ya EAC, huku ikitarajia majadiliano zaidi ya kimkakati na jumuiya hiyo katika kilimo cha mianzi.

  Alieleza kuwa mikakati inaendelea katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 16 utakaotekelezwa kwa miaka mitatu katika bara la Afrika ikiwa ni ahadi iliyotolewa wakati wa mkutano wa ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka jana.

  Katika kujenga uwezo, Liang Lin anasema China inatoa ufadhili kwa wanafunzi 50,000 kwa nchi za Afrika na kutaka nchi za EAC kutumia fursa hiyo ya masomo.

  Lin,anayemwakilisha balozi wa China nchini Tanzania na jumuiya ya Afrika Mashariki, awali aliwasilisha ufadhili wa dola US$200,000 kutoka wizara ya mambo ya nje ya China kwa Katibu Mkuu wa EAC kwa ajili ya programu za kujenga uwezo.

  Kwa Upande wake, Katibu Mkuu wa EAC, balozi Liberat Mfumukeko anashukuru kwa msaada huo toka Jamhuri ya watu wa China kwa ajili ya kujenga uwezo kwa jamii.

  Balozi Mfumukeko anamtaarifu Lin kuwa mchakato wa ushirikiano kwa nchi hizo unaendelea vema katika umoja wa forodha, soko la pamoja na itifaki ya umoja wa sarafu.

  Anasema nchi wanachama wa jumuiya hiyo wamekubaliana kurahisisha sheria na taratibu mipakani na kufungua mipaka ili kurahisisha muingiliano wa kibiashara kwa nchi hizo.

  Anasema katika kurahisisha muingiliano wa watu hakuna viza kwa nchi hizo huku baadhi ya nchi wanachama wakiruhusu kitambulisho vya utaifa kuwa nakala maalum ya kusafiri na nchi hizo zimeanza kutoa hati ya kusafiria ya kimataifa kwa nchi hizo kuwezesha kusafiri katika nchi hizo na nyingine.

  Katika maendeleo ya miundombinu, anasema nchi wanachama wanashirikiana katika utekelezaji wa miradi ya pamoja waliyokubaliana.

  Katika shirikisho la kisiasa EAC, Mfumukeko anasema kabla ya mwisho wa mwezi huu wanatarajia kuzindua mashauriano ya wadau kuhusu mswada wa katiba wa shirikisho la kisiasa kwa nchi wanachama ikishiriki katika bajeti ya mchakato huo.

  Anasema kila nchi itapendekeza watalaam wawili wa kutengeneza katiba na mwanasheria mmoja kusaidia katika kutengeneza sheria za awali kupendekeza shirikisho litakavyokuwa wakati wa kipindi cha mpito kuelekea shirikisho.

  Webradio
  Sauti
  6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 1
  12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 2
  20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
  • FM 3A
  • FM 3B
  Maoni yako