• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Taifa la China halikwepeki katika maendeleo -Spika Ndugai

    (GMT+08:00) 2019-11-22 16:22:25

    Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

    SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema katika dunia ya sasa Taifa la China halikwepeki katika masuala ya ushirikiano wa kiuchumi, hivyo akaishauri Serikali ya Tanzania kutumia fursa hiyo kunufaika kiuchumi.

    Amesema mbali ya kuwa China sasa ni miongoni mwa mataifa makubwa yanayoongoza kiuchumi duniani, lakini pia lina udugu wa muda mrefu na Tanzania, hivyo ni fursa nzuri katika kujenga ushirikiano wa kiuchumi.

    Alitoa kauli hiyo hivi karibuni bungeni wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Mipango likijadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2020/2021.

    Akichagizwa na michango ya wabunge mbalimbali akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM), Spika Ndugai anasema Taifa la China halikwepeki kwa sasa kama nchi inataka kufaidika na maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyofikiwa na taifa hilo lenye watu wengi duniani, likitokea barani Asia.

    "Kama hufanyi kazi na China ni sawa na kupishana na gari la mshahara," alisema Spika Ndugai baada ya mchango wa mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini aliyeigusa China katika mchango wake bungeni .

    Kama hiyo haitoshi, baada ya mchango wa Mbunge wa Makete, Profesa Norman Sigalla (CCM) ambaye pia aliizungumzia China kimaendeleo ya kiuchumi, Spika Ndugai aligongelea msumari akisema kwa sasa huwezi kuikwepa China kama unataka kupiga hatua kiuchumi.

    Spika Ndugai alitoa ushuhuda wa ziara yake nchini China miezi mitatu iliyopita na kueleza kuwa ni lazima kutumia udugu wa Tanzania na China kufaidika kiuchumi.

    "Miezi mitatu iliyopita nilikuwa China...hii ilikuwa ziara ya kwanza rasmi ya Spika wa Bunge la Tanzania nchini China tangu Uhuru. Kule China watu saba ndio wanaoongoza nchi. Hawa tulikuwa katika nafasi sawa kiuchumi huko nyuma, lakini sasa ni matajiri kuliko sisi.

    "Wakaniambia tunajua ninyi ni ndugu zetu...wanakumbuka jinsi Mwalimu Nyerere alivyowasaidia. Na Mwalimu Nyerere alifanya safari China mara 13," alisema Ndugai.

    Aliongeza, "kuna watu wa Marekani, Western, Europe wana mambo ya lobbying (kufanya ushawishi), hawa wakoloni waliotutawala bado wanataka tuendelea kuwa nao, lakini ukweli China huwezi kuikwepa."

    Alisema serikali lazima iangalie namna ya kushirikiana kiuchumi na China na kwamba muhimu ni kuwa na watu wenye uwezo wa kufanya majadiliano ya kibiashara na taifa hilo ili kunufaika na maendeleo yao ya kiuchumi.

    Tanzania imekuwa na ushirikiano wa kidugu na China tangu enzi za Mwalimu Nyerere pamoja na Kiongozi wa China, Mao Tse Tung mwanzoni mwa miaka ya 1960.

    China ndiyo iliyojenga Reli ya Tazara inayotoka Dar es Salaam hadi Kapiri Mposhi nchini Zambia katika miaka ya 1970, na imekuwa ikishiriki katika ujenzi wa majengo na miundombinu mingine kama barabara nchini Tanzania.

    Kwa sasa, China ni Taifa la pili kwa ukubwa kiuchumi duniani baada ya Marekani na inafuatiwa na Japan. Pato la Taifa la China ni Dola za Marekani trilioni 13.41, wakati Marekani ni Dola za Marekani trilioni 20.49.

    Katika mchango wake, Serukamba alisema lazima taifa lijifunze kutokana na hatua ilizozipga nchi kama China, Malaysia, Thailand na Singapore, na katika kutumia watu pamoja na teknolojia ili kufaidika kiuchumi.

    Alitoa mfano wa kusuasua kwa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo akisema kama taifa limezungumza na watu wa madini wa Barrick Corporation na kufanikiwa, kwa nini isiwe hivyo kuhakikisha ujenzi huo unafanyika.

    Naye Profesa Sigalla alisema uchumi wa Tanzania unaweza kuendelea kuimarika kwa kuiga mfano wa China na kuitumia nchi hiyo katika kushirikiana nayo kiuchumi.

    Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) alisema mbali ya China, Tanzania inaweza kutumia fursa za ushirikiano na nchi za Urusi na Uturuki ambazo zimekuwa na uchumi mkubwa na kugeukia masoko ya nchi hizo.

    Pia Mbunge wa Nkasi, Ally Kessy (CCM) alitaka kutumiwa kwa fursa ya kupakana na nchi kadhaa ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuimarisha bandari ya Kigoma ili kuvutia soko la nchi hiyo ambao ni miongoni mwa nchi za Afrika zenye uchumi mkubwa.

    Mbali ya kugusia maeneo hayo, wabunge pia walizungumzia miradi ya Gesi Asilia (LNG) mkoani Mtwara pamoja na miradi ya chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma, wakieleza kutoridhika na kasi inayoihusu miradi hiyo ambayo ingesaida katika ukuaji wa uchumi hasa wakati huo wa Tanzania ya viwanda.

    Kutokana na michango hiyo ya wabunge, Spika Ndugai ameiagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuzungumza na serikali kufahamu kwa kina nini kinakwamisha utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako