• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yatoa Sh. Bilioni 19.4 kujenga chuo cha ufundi Kagera

    (GMT+08:00) 2019-12-02 10:22:36

    Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

    SERIKALI imezindua ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma cha mkoani Kagera kilichofadhiliwa na Jamhuri ya Watu wa China kwa Shilingi bilioni 19.4.

    Kitakapokamilika chuo hicho kitatoa mafunzo ya fani za useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, ufundi bomba na kuchukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi

    Ufadhili wa serikali ya China utagharimu fedha za kitanzania sh bilioni 19.4 zinajumuisha usanifu, upembuzi ya kinifu na ujenzi.

    Waziriwa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua ujenzi huo na kusema ujenzi wa chuo hicho ni muendelezo wa jitihada za serikali kuhakikisha kunakuwa na vyuo vya ufundi stadi vya mikoa na wilaya.

    Alisema chuo hicho kinajengwa na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu tulionao na kwamba pindi ujenzi utakapokamilika vijana wengi wa kitanzania watapata fursa ya kusoma katika chuo hicho na kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazofundishwa.

    "Kama nilivyosema Tanzania na China ni marafiki na rafiki yako anaangalia mahitaji yako, waswahili husema akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli. China imeona Tanzania inajenga uchumi wa viwanda ikiwa ni azma ya serikali nao wakaamua watuunge mkono katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi ili kuandaa vijana wenye ujuzi watakaofanya kazi katika viwanda. Nikuombe Balozi tufikishie shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa msaada huu mkubwa na wa kihistoria," aliongeza.

    Waziri Ndalichako alisema ujio wa mradi huo utaongeza ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwa wazawa 400 wataajiriwa katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kupata ujuzi kulingana na kazi watakazokuwa wakizitekeleza.

    "Vijana watakaofanya kazi eneo la mradi pamoja na kufanya kazi watapata na mafunzo, kwa hiyo ujuzi wao wa kiufundi utaimarishwa kupitia kazi ambazo watakuwa wakifanya katika mradi," alisema.

    Waziri Ndalichako aliitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kupitia upya fani zilizopangwa kutolewa katika chuo hicho ili ziendane na mazingira halisi ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

    "Nimepitia fani ambazo zimeanishwa kutolewa katika chuo hiki pindi kitakapokamilika, nikiangalia eneo ambalo chuo kinajengwa ni eneo la ziwa na watu wa Kagera au wazazi wa hapa ni wavuvi lakini sijaona kozi ya uvuvi sasa tunawaletea mambo ya uchomeleaji, ufundi bomba, useremala, upakaji rangi kwenye bahari, nilitegemea kuwe na fani ya uvuvi pia tuweke fani zinazoendana na mazingira," alisema Waziri Ndalichako.

    Balozi wa China nchini Tanzania, BiBi Wang Ke alisema Rais wa Tanzania amezingatia maboresho ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwaongoza watanzania kuelekea dira ya maendeleo 2025 hivyo China iko tayari kuchangia maendeleo katika sekta ya elimu ili kufikia malengo ya elimu ambayo serikali ya tanzania imejiwekea.

    Nae Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti amewataka wanakagera hasa vijana kushiriki vizuri katika kazi za ujenzi zitakazofanyika katika mradi huo ili kupata ujuzi wa ufundi ambao utawasaidia kushirikia katika kazi za ujenzi zitakazojitokeza katika Mkoa wa Kagera mara baada ya mradi kukamilika

    Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kinajengwa katika eneo lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Burugo wilayani Bukoba na lina ukubwa wa hekta 40. 5 sawa na hekari 100.

    Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho pindi kitakapokamilika kitatoa fani za useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, ufundi bomba na kitachukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako