• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • China yaahidi kusaidia kutatua changamoto uendeshwaji reli ya Tazara

    (GMT+08:00) 2019-12-23 09:46:56

    Na Majaliwa Christopher

    MIAKA zaidi ya 40 sasa baada ya China kufadhili ujenzi wa reli ya Tazara inayounganisha Tanzania na Zambia, nchi hiyo ya Asia ya Mashariki imeahidi kuwa iko tayari kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili uendeshwaji wa reli hiyo.

    Reli hiyo yenya urefu wa zaidi ya kilomita 1,800 kwa sasa inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kimiundombinu inayohitaji hatua za haraka kunusuru alama hiyo ya kihistoria kati ya Afrika na China.

    Ahadi ya kuboresha reli ya Tazara ilitolewa na Naibu Spika wa Bunge la China, Ji Bing Xuan, Jumatano, Disemba 18, wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Spika wa Tanzania, Job Ndugai.

    Naibu Spika huyo alisema kuwa katika ziara yake kwenye ofisi za Tazara aliambiwa kuwa kuna changamoto za uchakavu wa vifaa vya treni na reli na kuwa msaada unahitajika.

    Alisema China inatambua nafasi ya reli ya Tazara katika kukuza uchumi wa Tanzania na sababu Tanzania ni rafiki mkubwa wa China nchi hiyo inayowajibu wa kuiimarisha Tazara.

    "Tanzania ni marafiki zetu wakubwa wa miaka mingi, hivyo tunao wajibu wa kusaidiana hasa katika kufanikisha nchi inakuwa kiuchumi na njia mojawpao ni kuboresha ufanisi wa Tazara,

    Kwa kuwa Rais Magufuli anataka Tanzania kuwa nchi yenye uchumi bora unaotegemea viwanda, reli ya Tazara inaweza kutimiza adhma hiyo kwa kuwa itakuwa ikisaidia usafirishwaji wa bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine", alisema kiongozi huyo wa China.

    Alisema akirejea nchini kwake ataanza mchakato wa kufanikisha adhma hiyo ya kuisaidia Tazara huku pia akiahidi kusaidia sekta nyingine zikiwamo za viwanda.

    Alibainisha kuwa ziara yake imelenga kubainisha fursa za uwekezaji pamoja na kufahamu tamaduni za Tanzania na kuwa akiwa nchini alitembelea Kijiji cha Makumbusho ya Taifa, Kijitonyama na kujifunza mambo mengi ya utamaduni.

    Pia alibainisha kuwa akiwa katika ziara yake hapa nchini ameona wafanyabiashara wadogowadogo wengi mitaani wakiuza bidhaa mbalimbali na kuwa hiyo ni inshara ya kuwa nchi inapiga hatua kimaendeleo.

    Kwa upande wake Spika Job Ndugai alibainisha kuwa ugeni huo utaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Tanzania huku akimtaka Naibu Spika huyo kushiriki katika kutafuta wawekezaji kutokea China.

    Alimhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha mahusiano yake na China katika nyanja za uchumi, siasa, utamaduni na kijamii.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako