• Idhaa ya Kiswahili
  • Uchumi
  • Michezo
  • Facebook
  • ChinaABC
  • Sayansi
  • Afya
  • Virusi vya corona vinavyoathiri sekta ya michezo

    (GMT+08:00) 2020-05-14 07:55:25


    Nchi mbalimbali duniani zikiwa bado zinaendelea kupambana na ugonjwa wa Covid-19 ambao tayari umesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuzorotesha uchumi wa nchi, sekta ya michezo nayo imeshuhudia pigo kubwa katika historia.

    Katika mwaka ambao ulitarajiwa kuwa na pilikapilika nyingi za michezo ya kitaifa na kimataifa pamoja na kalenda ya michezo iliyosheheni mashindano mengi, yakiwemo ya Olimpiki ya Tokyo, Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake, Kombe la Klabu bingwa Ulaya, Mabingwa wa Riadha Afrika, mashindano ya CHAN, Formula one, na hata Raga, badala yake zimekuwa wiki na miezi isiyo na chochote baada ya shindano moja baada ya jingine kuahirishwa au kusogezwa mbele. Kusitishwa kuoneshwa moja kwa moja kwenye televisheni kwa mashindano mbalimbali duniani inamaanisha kuwa wachezaji, makocha, klabu na mashirikisho yanaigia kwenye ukata.

    Jambo hili kwa Afrika limeleta changamoto kubwa. Wengi wanafahamu kuwa soka ni maisha, shughuli za soka zinaposimama tu, basi ni sawa na maisha kusimama pia. Kwa mujibu wa KPL, ambayo ni moja ya ligi ya juu ya Afrika Mashariki, asilimia 50 ya wacheza soka wake wanapata mshahara wao kwa wastani wa dola 200 kwa mwezi. Hii inawafanya wachezaji wengi kutegemea bonasi za mechi, posho za kusafiri na bonasi za ushindi. Hivyo bila ya kuchezwa mechi, wachezaji hawataweza kupata posho hizi.

    Achilia mbali posho na mishahara midogo wanayopokea baadhi ya wachezaji, hivi sasa klabu nyingi zimekuwa zikishauri wachezaji wao kuwapunguzia mshahara wao kwa asilimia kadhaa. Kuna baadhi ya wachezaji waligomea hatua hii hadi kufikia kufukuzwa kazi huku wengine wakikubali kwa shingo upande ili kuendana na hali ya kiuchumi iliyoigubika sekta ya michezo kutokana na mlipuko wa virusi vya corona.

    Mbali na kupunguziwa mishahara yao mfukoni, wachezaji wa Afrika pia wanakabilaiana na matatizo ya afya ya kiakili kutokana na wasiwasi wa kupata pesa za kuhudumia familia zao na tatizo kubwa la virusi vya corona.

    Lakini hata kwenye ligi kubwa za soka duniani, wachezaji nao pia hawakuachwa kwenye mkumbo wa kupunguziwa mshahara. Klabu kama za Premier League, Serie A ya Italia, La liga, Bundesliga nazo zimewataka wachezaji wapunguziwe mshahara. Hata hivyo kutokana na makali ya athari za ugonjwa wa Covid-19, nchi, mashirika, klabu na hata mtu mmoja mmoja wamekuwa wakichukua hatua chanya, ili kukabiliana na athari za mlipuko na kupunguza makali yake. Shirikisho la Soka Duniani FIFA lilitangaza kusaidia klabu zinazokumbwa na matatizo ya kiuchumi kwa kuzipatia pesa kutoka kwenye mfuko wake wa dharura. Mashirikisho mengi tayari yameshaanza kupata ruzuku hii kutoka FIFA. Changamoto hii ya virusi vya corona ambayo haikuitarajiwa imeporomosha sana uchumi wa klabu na mashirikisho mengi. Hivyo kwa sasa wadau wote wanatakiwa kuelewa athari iliyopo katika sekta ya michezo na kujua nini watafanya ili kutatua changamoto zilizopo pamoja na kulinda nafasi zao michezoni.

    Webradio
    Sauti
    6:00-7:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 1
    12:00-13:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 2
    20:00-22:00 (Afrika Mashariki)
    • FM 3A
    • FM 3B
    Maoni yako